KOREA KASKAZINI YATUPA KOMBORA KUBWA


Taifa la Korea Kaskazini limefanyia majaribio kombora lake la masafa marefu lililoruka juu zaidi na kombora hilo tayari limeonekana kuhatarisha usalama duniani kulingana na waziri wa maswala ya ulinzi nchini Marekani James Mattis.

Jaribio hilo la kombora mapema siku ya Jumatano lilianguka katika maji ya Japan.
Liliruka kwa urefu wa kilomita 4,500 na kusafiri umbali wa kilomita 960 kulingana na jeshi la Korea Kusini.

Ni jaribio la hivi karibuni ambalo limezua hali ya wasiwasi, Mara ya mwisho kwa taifa hilo kulifanyia jaribio kombora lake ni mwezi Septemba, Wakati huo, kombora lake la mwisho lilikuwa la sita la nguvu za kinyuklia mwezi huo.

Korea Kaskazini imeendeleza mpango wake wa kinyuklia pamoja na ule wa utengenezaji wa makombora licha ya shutuma kutoka kwa jamii ya kimataifa.

KIMENUKA TENA NYUMBANI KWA PLATINUM


Zarinah Hassan ‘Zari The BossyLady’

Mipasho! Mwanamitindo mjasiriamali, Zarinah Hassan ‘Zari The BossyLady’ ambaye aliingia katika mtafaruku wa maisha yake ya kimapenzi, kwa mara nyingine juzikati alionyesha kuwepo kwa kutoelewana kwao baada ya kuliamsha dude kwa kutoa maneno ya kumnanga mzazi mwenzake.

Awali, vyanzo vyetu vilivyo karibu na mrembo huyo mwenye watoto watano, alisema kwa sasa hana uhusiano mzuri na baba wa watoto wake wawili, kwa kile kinachosemwa kuwa ni kitendo cha mwenzake huyo kuendekeza mapenzi na wanawake wengine.

“Ni kama mchezo unaelekea mwishoni hivi sasa, maana maneno na ugomvi kati yao hauishi, jamaa anafanya kazi kubwa kuficha kuhusu huu uhusiano wake kuwa juu ya mawe, lakini ukweli ni kwamba hakuna dalili za wawili hawa kukaa tena imara kama zamani,” kilisema chanzo hicho.

Katika tukio la hivi karibuni, mwanamama huyo aliandika katika mtandao wake maneno yenye kumlenga mzazi mwenzake, akisema anaendekeza wanawake na watoto wengi na kwamba badala ya kuona anauza kazi zake nyingi za muziki, yeye amekuwa hodari wa eneo ambalo hahusiki.

Katika kumnanga huko, Zari alisema endapo mtu anatafuta ubalozi wa kondom, ambacho ni kifaa cha kinga dhidi ya magonjwa ya kuambukizwa kupitia ufanyaji mapenzi, basi hana haja ya kuhangaika kumpata, kwa kuwa tayari mtu.

TASWIRA YA MAGAZETI YA LWO TAREHE 29/11/2017

MKUU WA MKOA MOROGORO APATA AJALI

Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Dk Steven Kebwe 

Morogoro. Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Dk Steven Kebwe amepata ajali katikati ya Hifadhi ya Taifa ya Mikumi iliyopo wilayani Kilosa mkoani hapa.

Ajali hiyo ilitokea saa saba usiku wa kuamkia leo Jumatano ambapo inadaiwa gari la mkuu huyo wa mkoa lilimgonga mnyama aina ya Nyati na gari hilo kuharibika vibaya.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Urlich Matei amethibitisha kutokea kwa ajali hiyo na kueleza kuwa taarifa kamili ataitoa mara baada ya kukamilika.

Inadaiwa kuwa ndani ya gari hilo mbali na kuwepo mkuu wa mkoa pia aliambatana na mlinzi wake ambao wote kwa pamoja walitoka salama.

Mwandishi wa Mwananchi alifanya juhudi za kumtafuta mkuu wa mkoa kwa njia ya simu ili kuzungumza naye juu ya ajali hiyo lakini simu yake iliita bila kupokelewa

HATUTA WAVUMILIA WENYE TAMAA NA FEDHA ZA UKIMWI




WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amesema serikali haitawavumilia wote, wanaotumia vibaya fedha za serikali, ambazo zinapaswa kuleta maendeleo kwa wananchi zikiwemo za Mfuko wa Udhibiti Ukimwi.
Majaliwa alisema Dar es Salaam jana wakati akifungua kongamano la Kitaifa la Maadhimisho ya Siku ya Ukimwi Duniani 2017, kaulimbiu ikiwa ‘Changia Mfuko wa Udhamini wa Udhibiti Ukimwi, Okoa Maisha.”
Alisema wito wake ni kuhakikisha bodi ya mfuko huo, inasimamia vizuri fedha hizo zinazochangiwa na wadau mbalimbali ili kuwahakikishia usalama wake. “Fedha hizi zikitumika vinginevyo hatutavumiliana. Malengo ni kuhakikisha fedha hizo zinazotolewa na wadau zinatumika kama ambavyo imekusudiwa,” alisema Majaliwa.
Alisema anayo furaha kuwa Mfuko huo wa Udhibiti Ukimwi umeanza kufanya kazi, ambapo Oktoba 21, mwaka huu kwa mara ya kwanza Mfuko huo uligawa fedha kwa ajili ya shughuli za kudhibiti ukimwi nchini Sh. milioni 660, zilitolewa kwa Wizara ya Afya kwa ajili ya kununua dawa za Cotrimoxazole ambazo hutumika kutibu na kuzuia magonjwa nyemelezi kwa watu waishio na virusi vya Ukimwi.
“Aidha kiasi cha Shilingi milioni 200 zilitolewa kwa Mkoa wa Manyara kwa ajili ya kuchangia ujenzi wa Kituo cha Afya Mererani, ambacho licha ya kutoa huduma nyingine za afya, kitatumika kutoa huduma za dawa za kufubaza VVU kwa watu waishio na virusi vya Ukimwi,” alisema.
Alisema serikali itaendelea kutenga fedha za mfuko huo na kuhakikisha inahamasisha wananchi na wadau, ikiwemo sekta binafsi kuchangia mfuko huo muhimu. Alisema Serikali ya Awamu ya Tano imedhamiria kujenga Tanzania ya viwanda na ili ifikie lengo hilo ni lazima wananchi wawe na afya bora.
“Nguvu kazi kwa ajili Tanzania ya viwanda itatokana na wananchi wenye nguvu na afya bora. Hivyo serikali tutahakikisha tunaendelea kutoa huduma bora za afya ili wananchi wetu waweze kuwa na afya bora,” alisema.
Alisema watu milioni 16 ya Watanzania wote ni vijana na wanapaswa kukingwa dhidi ya magonjwa mbalimbali ikiwemo Ukimwi ili taifa liwe na nguvu kazi ya kutosha hasa kipindi hiki linapoanza mageuzi makubwa ya kiuchumi na kimaendeleo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Tume ya Kudhibiti Ukimwi Tanzania (Tacaids), Dk Leonard Maboko alisema kongamano hilo ni sehemu ya shughuli za Maadhimisho ya Siku ya Ukimwi duniani, itakayofanyika Desemba mosi hapa nchini.
Alisema maonesho ya maandalizi hayo yalianza Jumamosi, yakijumuisha huduma mbalimbali za utoaji elimu na burudani kwa wananchi ikiwemo ushauri nasaha na upimaji wa hiari wa VVU.
Alisema pia kuwa tayari wamezindua mkakati wa kitaifa wa kondomu wa miaka mitatu wa 2016 hadi 2018, na siku ya kilele cha maadhimisho hayo kutakuwa na uzinduzi wa Ripoti ya Utafiti wa Kitaifa wa Matokeo ya Ukimwi wa Mwaka 2016/17.

MEYA WA CHADEMA IRINGA APANDISHWA KIZIMBANI




MEYA wa Manispaa ya Iringa, Alex Kimbe na wafuasi wenzake watano wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), wamepandishwa kizimbani mjini Iringa, kujibu mashitaka yanayohusishwa na vurugu za uchaguzi mdogo wa udiwani Kata ya Kitwiru, Iringa mjini.
Wakati Meya huyo aliachiwa jana kwa dhamana na Mahakama ya Wilaya Iringa, baada ya kusota rumande kwa siku tatu, Mahakama ya Hakimu Mkazi Iringa iliwanyima dhamana wafuasi hao watano kwa kuwa kati ya makosa matatu, wanayotuhumiwa kuyafanya kosa moja halidhaminiki.
Mwendesha Mashtaka wa Polisi, Aristeck Mwinyikheri alisema Kimbe aliyefikishwa mahakamani hapo kwa kesi Namba 189 ya mwaka 2017, anashitakiwa kutishia kumuua mtu kwa bastola katika tukio la Novemba 26, mwaka huu katika Kata ya Kitwiru mjini Iringa, wakati shughuli ya uchaguzi mdogo wa udiwani wa kata hiyo ikiendelea.
Mwinyikheri alisema Meya huyo alitenda kosa hilo kwa Alphonce Muyinga, ambaye ni Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM), kinyume na Kifungu Namba 89 (2) (a) cha Kanuni za Adhabu.
Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Wilaya ya Iringa, John Mpitanjia alisema shauri hilo litarudi tena mahakamani hapo Desemba 12, mwaka huu. Wakati huohuo, Mahakama ya Hakimu Mkazi Iringa imewanyima dhamana Martha Robert, Leonard Kulijira, Esau Bwire, Christopher Jevas na Samwel Nyanda, wafuasi wa Chadema ambao kwa pamoja wameshitakiwa mahakamani kupitia kesi namba 190 ya mwaka 2017 kwa makosa matatu.
Mbele ya hakimu mkazi wa Mahakama hiyo, Richard Kasele , Mwendesha Mashitaka wa Mahakama hiyo Chakila Felix alisema washitakiwa hao wafuasi wa Chadema, wanatuhumiwa kujeruhi, kuteka na kufanya unyang’anyi kwa kutumia nguvu.
Felix alisema watuhumiwa hao wanatuhumiwa kumjeruhi Dick Frank na kumnyang’anya simu yake ya mkononi. Mahakama hiyo imewarudisha rumande washitakiwa hao baada ya kunyimwa dhamana kwa kuwa kosa la unyang’anyi kwa kutumia nguvu, halina dhamana na shauri lao litarudi tena mahakamani hapo Desemba 12, mwaka huu.

MABALOZI KUPANDA MLIMA KILIMANJARO

KATIKA kuendeleza juhudi za kutangaza vivutio vya utalii nchini, mabalozi tisa kati yao wanane Watanzania na mmoja Balozi wa Algeria nchini Qatar, wanapanda mlima Kilimanjaro leo, ikiwa ni sehemu ya jitihada za Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) katika kuvitangaza vivutio vya nchi yetu, ukiwemo Mlima Kilimanjaro.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini Moshi, Ofisa Habari Mkuu wa TTB, Geoffrey Tengeneza alisema wameandaa ziara hiyo ya mabalozi kwa lengo la kuwajengea uwezo na wigo mpana wa kuvitangaza vivutio vya utalii katika nchi watakazokwenda kuhudumia kama mabalozi. “Maandalizi yamekamilika na tunatarajia mabalozi na wafanyakazi wa Bodi ya Utalii na mjumbe kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na waandishi wa kutoka Clouds Media Group watapanda mlima Kilimanjaro kesho (leo),” alisema Tengeneza.
Mabalozi hao wanaopanda Mlima Kilimanjaro leo ni Balozi Aziz Mlima, Balozi Samwel Shelukindo, Balozi Luteni Jenerali Wynjones Kisamba, Balozi Pastor Ngaiza, Balozi Bernard Achiula, Balozi Alan Mzengi na Balozi Antony Cheche. Pia yumo Balozi wa Algeria nchini Qatar, Abdelaziz Sebaa.
Tengeneza alisema katika kupanda mlima huo mrefu kuliko wote barani Afrika, kuna vivutio vingi watakutana navyo hivyo kuwafanya kuwa na vitu vingi vya kusimulia kama vielelezo watakapokuwa katika maeneo yao ya kazi na kuwa mabalozi wa kutangaza vivutio vya utalii ukiwemo Mlima Kilimanjaro kwa vitendo.
“Ni matumaini yetu kuwa watakwenda kuitangaza Tanzania pamoja na vivutio vyake katika nchi za nje na kufanya ongezeko la watalii kuja nchini kuongeza maradufu,” alifafanua Tengeneza. Alisema kupitia ziara hiyo, mabalozi watakwenda kutekeleza kwa vitendo Diplomasia ya Uchumi kwa kuvitangaza vivutio vya utalii vilivyopo Tanzania na ukarimu wa Watanzania kwa wageni.
“Kama Bodi ya Utalii tunatoa wito kwa mabalozi wengine wanaoiwakilisha Tanzania katika nchi nyingine duniani kutumia nafasi hiyo katika kuvitangaza vivutio hasa Mlima Kilimanjaro ambao ndio mlima mrefu barani Afrika,” alieleza ofisa huyo wa TTB.
Kwa upande wake, Balozi wa Algeria nchini Qatar, Abdelaziz Sebaa ambaye pia ni Mwenyekiti wa Mabalozi nchini humo, alisema hiyo ni nafasi ya pekee kwake kupanda Mlima Kilimanjaro na kujionea vivutio vingine vya utalii Tanzania.
Alisema kwa nafasi hiyo na vitu atakavyokwenda kuviona, atakwenda kuwahamasisha mabalozi wengine katika umoja wao ili kuvitangaza vivutio vilivyopo Tanzania, hivyo kusaidia kujenga uhusiano mzuri zaidi katika sekta ya utalii. Ziara hiyo ya mabalozi kupanda Mlima Kilimanjaro, imeratibiwa na TTB na katika kupanda mlima huo, wataongozwa na Kampuni ya ZARA Tours iliyopo mjini Moshi.

MSIGWA ASEMA NA POLISI

Related imageMbunge wa Iringa Mjini, Peter Msigwa ametupa jiwe gizani kwa wapinzani wao wa kisiasa kwamba wamewashinda kwa hoja zote za kisiasa na wameshindwa kuzijibu hivyo anawashangaa kushangilia ushindi.
 
Msigwa amesema kwamba wapinzani  wao lazima watawashinda kama watatumia vyombo vya usalama na siyo kwa hoja na kwamba wao Chadema wakitoa hoja wao wamekuwa wakishindwa kuzijibu.

Msigwa kupitia ukurasa wake wa Twiter ameandika kwamba "Hatuna mafunzo ya kipolisi wala kijeshi! Mkitumia vyombo vya usalama lazima mtatushinda , lakini tumewashinda HOJA zote za kisiasa! Mmeshindwa kuzijibu! Eti unashangilia Ushindi! Huu ni uporaji" Msigwa

Chama cha upinzani CHADEMA kimekuwa kikilalamikia chama tawala kutumia vyombo vya dola katika kuwakandamiza.

TAMKO LA ACT KWA SERIKALI YA AWAMU YA TANO

CHAMA cha ACT-Wazalendo kimeainisha mambo tisa ambayo Serikali ya awamu ya tano  imefanya vibaya katika miaka miwili ya uongozi wa Rais John Magufuli.
Mwenyekiti wa chama hicho, Yeremia Maganja, akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam amesema  mambo hayo yamegawanywa katika mafungu makuu matatu.

“Leo tutatoa tathmini yetu ya miaka miwili ya utawala huu, tathmini hii ni zao la utafiti husika uliofanyika nchi nzima. Tathmini yetu itaainisha mambo 9 ambayo tunaamini hayakufanywa vizuri kabisa na Serikali,” amesema Maganja.

“ACT Wazalendo inao wajibu wa kujihusisha na masuala ya watu, tunatimiza wajibu huo kwa tathmini hii ya kuangazia mambo haya risa ambayo ni mapungufu ndani ya miaka miwili hii ya utawala huu,”ameongeza.

Amesema mambo hayo yamefanya vibaya kiasi cha kuleta athari nchini, kisiasa, kiutawala na kiuchumi.

Ametaja maeneo hayo kuwa ni ya, Haki za Msingi  Usimamizi wa Uchumi na Uendeshaji wa Nchi.

Haki za Msingi 
Maganja amesema  kumekuwepo na uminywaji wa uhuru wa Vyama vya Siasa Kufanya mikutano ya hadhara, uhuru wa Vyombo vya habari, pamoja na Uhuru wa Kujieleza, Kuminywa kwa haki ya wazanzibari kuchagua viongozi wao na Kupuuzwa kwa matakwa ya Katiba Mpya.


Usimamizi wa Uchumi wa Nchi

Amesema kumekuwepo kwa hali ya Kusinyaa kwa Uchumi wa Nchi, Kudhohofishwa kwa Sekta Binafsi,  Mazingira Mabaya ya Biashara Nchini, pamoja Kupaa kwa Deni la Taif.

Mengine ni kutelekezwa kwa kilimo na utekelezaji wa miradi mikubwa bila kuzingatia maslahi ya umma.

Uendeshaji wa nchi

Mwenyekiti huyo amesema katika kipengele hiki serikali hii imefanya vibaya kwa uvunjaji wa misingi ya Sera ya Mambo ya Nje, unyanyasaji wa watumishi wa umma na utawala unaovunja taasisi za kikatiba na kisheria kutoakana na kwamba utawala huu umekuwa wa mtu mmoja.