KAMBI Rasmi ya Upinzani Bungeni imesema imejipanga kumbana kwa hoja 15
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe,
atakapowasilisha bungeni mjini Dodoma leo hotuba ya makadirio ya wizara
yake kwa mwaka ujao wa fedha.
Mambo hayo ni pamoja na kutotungwa kwa kanuni za sheria mpya ya habari
iliyotungwa mwaka 2016, kupotea kitatanishi kwa waandishi wa habari,
kusajili magazeti kila mwaka, waandishi wa habari kulipia vitambulisho
vya kitaifa kila mwaka na ufujaji wa mapato ya mechi za soka
zinazochezwa nchini.
Zingine ni serikali kutotenga bajeti kusaidia maendeleo ya michezo,
madai ya wasanii kutengenezewa matabaka na wenye ving'amuzi kutoza
huduma hadi kwa vituo vya televisheni (TV) visivyopaswa kulipiwa.
Pia wasanii kuimba nyimbo zisizo na maadili na kuvaa mavazi yasiyoendana
na utamaduni wa Kitanzania, kuvamiwa kwa viwanja vya michezo nchini na
changamoto katika upatikanaji wa washindi wa shindano la Miss Tanzania.
Kwa mujibu wa ratiba ya vikao vya Bunge la Bajeti iliyotolewa na Idara
ya Habari na Elimu ya Bunge leo, Bunge litajadili kwa siku moja hotuba
ya makadirio ya wizara hiyo kwa mwaka ujao wa fedha.
Akizungumza na Nipashe mjini hapa jana, Naibu Waziri Kivuli wa Habari,
Vijana, Utamaduni na Michezo, Devotha Minja, alisema wamepanga kuutumia
mjadala huo kuibana serikali ili izitatue changamoto hizo.
Alisema hoja ya kwanza ni kile alichokiita kuvifunga midomo kwa vyombo
vya habari vinavyomilikiwa na watu binafsi kwa kuvifungia na kuvitoza
faini pale zinapochapisha au kutangaza habari kukosoa mwenendo wa
utendaji wa serikali.
Alisema hali hiyo inarudisha nyuma maendeleo ya tasnia ya habari na kuminya uhuru wa kujieleza na haki ya kupata habari.
Minja ambaye pia ni Mbunge wa Viti Maalum (Chadema), alisema hoja yao ya
pili ambayo Dk. Mwakyembe watamtaka awape majibu bungeni leo ni
kutotungwa kwa Kanuni za Sheria mpya ya Habari nchini.
Alisema licha ya Bunge kuipitisha muswada wa sheria hiyo na kutiwa saini
na Rais takriban miaka miwili sasa, kanuni hazijatungwa ili ianze
kutumika.
"Kwa sheria ile ambayo tuliipitisha, bado hazitengenezwa zile kanuni za
kuunda mabaraza ya kushughulikia kesi za mwandishi mmoja mmoja," alisema
Minja.
"Na hapa tunaona kuna ucheleweshaji wa makusudi ili sheria ya zamani
iendelee kutumika kwa sababu inampa mamlaka waziri kufungia magazeti.
Sheria ya sasa haina kitu kama hicho, inataka mwandishi aliyekosea ndiyo
awajibike na si kufungia gazeti zima."
Minja ambaye kitaaluma ni mwandishi wa habari, pia alisema upinzani
umejipanga kuutumia mjadala wa leo kumbana Dk. Mwakyembe ili wizara yake
iachane na utaratibu wa waandishi wa habari kulipia kila mwaka Sh.
30,000 kupata vitambulisho vya kitaifa (press cards) badala yake wawe
wanalipa kila baada ya miaka kuanzia mitatu hadi 10 kama ilivyo kwa
leseni ya udereva na hati ya kusafiria.
Minja alisema malipo ya aina hiyo yako pia katika usajili wa magazeti,
akieleza kuwa kuna utaratibu mpya umeanzishwa na wizara hiyo wa kusajili
gazeti kila mwaka ambao hawauungi mkono.
Alisema utaratibu huo aliodai upo katika nchi mbili tu katika Jumuiya ya
Afrika Mashariki wanaona si rafiki kwa uhai wa tasnia ya habari kwa
kuwa umelenga kuyazima usajili magazeti yanayoandika habari
zisizoifurahisha serikali.
Pia alisema watautumia mjadala wa leo kumbana Dk. Mwakyembe na serikali
kwa ujumla kuhusu kile alichodai wasanii nchini wamegawanyika.
"Kuna wasanii wanapata upendeleo mkubwa wa serikali, na hili sasa
limetengeneza matabaka kwa wasanii wetu. Yaani sasa tumefikia hatua
wasanii wanakuwa wa chama fulani ilhali wanapaswa kuwa pamoja na kufanya
kazi kwa kushirikiana," Devotha alisema.
Naibu waziri kivuli huyo pia alisema bado kuna changamoto ya ufujaji wa
mapato ya milangoni kwenye mechi za soka nchini, akidai kuna Sh. milioni
mbili zinadaiwa zinalipwa kwa wanaojiita wawezeshaji wa uwanja kwa kila
mechi inayochezwa Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Sambamba na hayo, alisema watahoji bungeni sababu za uongozi wa
Shirikisho la Soka (TFF) kuteua mtu mwenye tuhuma za rushwa kushika
nafasi ya mtu aliyeondolewa madarakani kwa tuhuma zenye mwelekeo huo.
Aliongeza kuwa upinzani umejipanga kuibana serikali leo ichukue hatua
stahiki dhidi ya watoa huduma za ving'amuzi ambao wamekuwa wakikata
huduma hadi kwenye Tv zisizoruhusiwa kulipiwa nchini.
Wakati Minja akieleza hayo, Mbunge wa Wawi, Ahmed Juma Ngwali (CUF),
alisema upinzani pia umejipanga kumbana Waziri Mwakyembe ili wizara yake
iwe inatenga bajeti ya kusaidia maendeleo ya sekta ya michezo nchini.
Ngwali alidai kuwa kwa takribani miaka mitatu sasa, TFF haijawahi
kupokea kiasi chochote cha fedha kutoka serikalini kusaidia maendeleo ya
mpira wa miguu nchini.
Naye Mbunge wa Kaliua, Magdalena Sakaya (CUF), aliiambia Nipashe mjini
hapa jana kuwa kama atapata nafasi ya kuchangia mjadala huo leo,
ataitaka serikali kudhibiti maudhui ya nyimbo za wasanii na uvaaji wao.
"Nyimbo za wasanii wetu zinapaswa kuzingatia maadili. Mavazi yao pia ni
lazima yazingatie utamaduni wetu ili kutunza heshima ya nchi," Sakaya
alisema huku akisisitiza Baraza la Sanaa (Basata) linapaswa kuwajibishwa
kwa kile alichodai limeshindwa kudhibiti wizi wa kazi za wasanii.
Mbunge huyo pia alisema atautumia mjadala wa leo kumshauri Dk. Mwakyembe
na wizara yake kudhibiti udanganyifu katika upatikanaji wa washindi wa
Miss Tanzania, akidai kuwa katika miaka ya karibuni shindano hilo
limetawaliwa na udanganyifu.
"Miaka ya nyuma, nilifuatilia miaka mitatu ya mwanzo, mshindi ulikuwa
unamwona kuanzia hatua ya mwisho kuwa huyu atashinda na kweli inakuwa
hivyo. Lakini miaka ya karibuni kumekuwa na udanganyifu mkubwa ambao
unaashiria ama rushwa au kujuana," alisema.
"Baadhi ya ma-Miss wenyewe wanaishi maisha ya ajabu ya kubadilisha
wanaume. Hivi kweli hii ndiyo maana ya shindano hili? Kulikoni kuendelea
kuiabisha nchi, ni heri lifutwe tu."
Sakaya pia alisema atautumia mjadala wa leo kuibana serikali ivirejeshe
viwanja vya michezo na maeneo ya wazi yaliyovamiwa na kuendelezwa kwa
kuwa uvamizi huo unakwamisha maendeleo yua watoto kimichezo.
"Ni aibu viwanja vya michezo vimevamiwa kujengwa majumba na serikali ipo inaangalia tu," alisema Sakaya na kuongeza:
"Ni lazima kama serikali inayojali maendeleo ya watoto na michezo
tuvirejeshe viwanja na maeneo ya wazi yaliyovamiwa. Kama kuna mtu
kajenga nyumba kwenye eneo la wazi tubomoe ili watoto wapate mahali pa
kucheza.
"Lazima kama taifa tuwekeze katika michezo kwa sababu michezo ni ajira,
ni afya na burudani. Rais mstaafu (Jakaya) Kikwete alikuwa analipa hadi
mishahara ya makocha lakini sasa serikali inaonekana imejiweka kando
kuendeleza michezo. Shuleni hakuna vifaa vya michezo.
"Tunategemea nini huko mbele kama hatuwekezi kwa watoto kwa sasa? Kina
(Cristiano) Ronaldo hawakutengenezwa ukubwani, tuwekeze kwa watoto."