ELIMU YATOLEWA KWA VIONGOZI WA DINI DHIDI YA KUPINGA NDOA ZA UTOTONI


Mwenyekiti wa Mtandao wa kutokomeza Ndoa za Utotoni Bi. Valeria Msoka akisisitiza jambo katika mkutano uliowakutanisha viongozi wa dini zote lengo likiwa ni kujadili nafasi yao katika kupinga ndoa za utotoni.
Baadhi ya wageni waalikwa wakifuatilia kwa umakini mkutano mapema leo jijini Dar es salaam.

Sheikh Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Al Hadi Mussa Salim akitoa ufafanuzi wa jambo fulani mapema leo katika mkutano uliowakutanisha viongozi wa dini mbalimbali na kimila katika kujadili nafasi yao katika kupinga ndoa za utotoni.
Sheikh Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Al Hadi Mussa Salim akichangia mada mbele ya wageni walioudhuria mkutano huo mapema leo jijini Dar es salaam.

 Mkurugenzi mtendaji wa RICPT ambaye pia ni muwakilishi wa dini ya kikristo Rev. Canon Thomas Godda akitoa ufafanuzi juu ya siku hiyo, na nini nafasi yao kama viongozi wa dini katika kupinga ndoa za utotoni na ushiriki wao katika kuleta mabadiliko ya sheria ya ndoa inayotumika hivi sasa.
Mwanasheria kutoka Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu Bw. Godfrey Mpandikizi akitoa presentetion mbele ya wageni waliudhuria mkutano wa kujadili kushinikiza viongozi wa dini na wakimila kupambana ili kuweza kubadilishwa kwa sheria ya ndoa iliyopo hivi sasa.

  • Viongozi wa dini zote hapa nchini wametakiwa kuwa mstari wa mbele kuishinikiza serikali kukubali kubadilisha sheria ndoa ya mwaka 1971.

  • Hayo yamesemwa mapema leo jijini Dar es salaam katika semina iliyoandaliwa na Mtandao wa Kutokomeza Ndoa za Utotoni(TECMN) iliyowakutanisha viongozi wa dini zote mbili pamoja na viongozi wa kimila kutoka mikoa mbalimbali.

  • Akiongea katika semina hiyo Bi. Valeria Msoka alisema kuwa viongozi wa dini ni watu walio karibu sana na jamii, hivyo wanazijua vizuri changamoto wanazokutana nazo wananchi ikiwemo ndoa za utotoni na wanatakiwa wasikae kimya kwani wao ndio msaada pekee kwa jamii yao.

  • Lakini pia viongozi wa dini ni watu wanaopewa nafasi nzuri na kuheshimiwa kwa kiasi kikubwa na serikali hivyo watumie muda huo kuiamba serikali kuwa sheria hii ya mwaka 1971 inayotoa ruhusa kwa mtoto wa kike kuolewa akiwa na miaka 14 haifai na inatakiwa kubadilishwa.

  • Mwenyekiti huyo aliendelea kusema kuwa lengo la kukutana na viongozi wa dini ni kujaribu kushauriana na kuona nini watakifanya kushinikiza kubadilishwa kwa sheria hiyo inayomnyima haki za zake za msingi mtoto wa kike.

  • Akiongea kwa niaba ya dini ya kiislamu Sheikh Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Al Hadi Mussa Salim alisema kuwa dini zetu zimekuja kwa lengo kuu la kuwasaidia wanadamu na hasa wanawake ambao walikuwa wakinyanyaswa na kunyimwa haki zao katika jamii hususani kwa upande wa ndoa.

  • Aidha Sheikh Mkuu wa Mkoa alisema kuwa cha muhimu tuungane kwa pamoja Waislamu, Wakristo, viongozi wa Kimila pamoja na serikali katika mitazamo na mwazo yetu ili tujue kuwa mtoto wa kike ni nani na haki zake ni zipi anazostahili kupata, kwa njia hiyo tunaweza kufanikiwa kulitokomeza tatizo hili la ndoa za utotoni.

  • Sheikh huyo aliendelea kusema kuwa tusipokuwa na sauti moja hatutaweza kama viongozi wa dini tukisema ndoa za utotoni zikome lakini serikali ikipinga atuwezi kuondoa tatizo hili, cha msingi ni kukubaliana makundi yote kuwa hatuzitaki ndoa za utotoni katika jamii yetu serikali ikubali viongozi wa kimila wakubali, wananchi wakubali na makundi yote yawe tayari kupambana vita hivi.

  • Kwa upande wake kiongozi aliwakilisha dini ya kikristo Rev. Canon Thomas Godda alisema kuwa zama zimebadilika kwani mwanzo sharia hii ilivyotungwa na ilipitishwa kwa urahisi kwa kuwa watu hawakuwa na uelewa, ila kwa sasa watu wameelimika na inapaswa kupingwa kwa nguvu zote swala hili.

  • Bw. Thomas aliendelea kusema kuwa ndoa inayokubalika hata katika vitabu vya dini ni ya watu wazima wote ambao umri wao ni kuanzia miaka 18 na kuendelea, hivyo basi wao kama viongozi wa dini watajaribu kufanya ushawishi kwa kushirikiana na wadau wengine kuhakikisha swala hili linatokomezwa kabisa na sheria inabadilishwa.

No comments: