HALI YA LISSU YAIMARIKA AANZA KUFANYA MAZOEZI





HALI ya Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (Chadema) anayepatiwa matibabu katika hospitali jijini Nairobi nchini Kenya baada ya kushambuliwa kwa risasi imeelezwa kuimarika huku akiwa ameanza kufanya mazoezi.
Aidha, gharama za matibabu yake yote kuanzia aliposhambuliwa hadi Oktoba 12, mwaka huu, anapoendelea na matibabu nchini Nairobi zimefikia jumla ya Sh milioni 412.4. Hata hivyo, Chadema imesema wanaiachia familia suala la kuwa wasemaji wa Lissu, lakini ikasisitiza kuwa atapelekwa nje ya nchi kwa ajili ya awamu ya tatu ya matibabu yake.
Kadhalika imesema kuanzia sasa inaanza kutoa sauti na picha za Lissu katika mitandao mbalimbali ya kijamii ili kuwaonesha Watanzania kuhusu hali halisi ya mgonjwa waliyekuwa wakimuombea.
Mwenyekiti wa Taifa wa Chadema, Freeman Mbowe alisema hayo jana Dar es Salaam wakati akizungumzia hali halisi ya Lissu na kuongeza kuwa wakati wa matibabu yake, ameweza kufanyiwa upasuaji wa aina tofautitofauti mara 17 huku akiwa amepewa damu nyingi kuliko wagonjwa waliowahi kutibiwa katika hospitali hiyo.
Kuhusu hali ya Lissu, Mbowe alisema kwa muda wote tangu alipofikishwa hospitalini hapo, alikuwa katika chumba cha uangalizi maalumu (ICU) akihudumiwa na madaktari 12, lakini wiki iliyopita ametoka na mashine zote alizokuwa akitumia zimeondolewa mwilini mwake.
“Kwa sasa mwili wake unaweza kusukuma damu peke yake, viungo vyote viko timamu ikiwemo figo, hatumii mashine ya oksijeni, mirija ya chakula pia haitumii tena,” alieleza Mbowe na kuongeza kuwa juzi kwa mara ya kwanza alikaa mwenyewe kwani viungo vyote vimeungwa.
Alisema Lissu pia anaweza kutembea katika kiti cha kubeba wagonjwa na wiki iliyopita aliweza kuliona jua kwa mara ya kwanza tangu aliposhambuliwa mjini Dodoma. Mbowe alisema Hospitali ya Nairobi ni ya pili iliyokuwa ikiendelea kutoa matibabu kwa Lissu, baada ya ile ya Dodoma siku ya shambulio na kwamba baada ya wiki moja kuanzia sasa, atamaliza matibabu ya awamu ya pili na kusudio ni awamu ya tatu ambayo atapelekwa nje ya Tanzania wa ajili ya uponyaji zaidi.
“Awamu ya tatu ambayo ni ya muda mrefu zaidi ya uponyaji atapelekwa nje ya nchi ambako kwa sasa hatuwezi kusema ni nchi gani kwa sababu za kiusalama,” alieleza Mbowe akisisitiza kuwa chama hicho bado kinaiomba serikali kuruhusu wachunguzi wa nje ili kufuatilia waliohusika katika shambulio hilo.
Kuhusu dereva wa Lissu, alisema chama hakijamficha na hajawahi kukimbia na kwamba Jeshi la Polisi linaweza kumpata popote pale alipo. Kuhusu kuiachia familia suala la Lissu, alieleza kuwa chama hicho kimefanya kazi na familia kwa muda wote waliokuwa wakimuuguza Lissu, lakini kwa awamu ya tatu ya matibabu yake wanaiachia ifanye maamuzi ya ndani.
“Jukumu la kuwa wasemaji wa suala la Lissu tunalikabidhi kwa familia, kwa sababu mgonjwa ameimarika anaweza kufanya uamuzi hivyo tumeona tusiingie mpaka uvunguni, bali tukasimu kwa familia ambayo ina haki,” alisema na kufafanua kuwa chama hakijivui wajibu, bali watawajibika nyuma ya familia.
Kuhusu gharama za matibabu, alisema fedha hizo zimetokana na michango mbali mbali kutoka kwa Watanzania wote wenye itikadi njema, wabunge, wanachama wa chama hicho, Watanzania waishio nje ya nchi pamoja na wafanyabiashara. Hata hivyo, aliwaomba Watanzania kuendelea kumchangia Lissu ili apate matibabu katika awamu yake ya tatu atakapokuwa nje ya nchi

No comments: