TAKUKURU WAMKANYA JOSHUA NASARI





TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) imemuonya Mbunge wa Jimbo la Arumeru Mashariki, Joshua Nassari wa Chadema, ikimtaka aiache taasisi hiyo ifanye kazi kwa mujibu wa sheria na kamwe asiihusishe wala kuiingiza kwenye matukio ya kisiasa.
Taasisi hiyo imetoa tamko hilo, baada ya kushtushwa na kitendo cha mbunge huyo na wenzake, kila wanapowasilisha taarifa zao Takukuru, huzungumza na vyombo vya habari kuhusu yaliyojiri walipowasilisha taarifa hizo huku wakishinikiza hatua zichukuliwe haraka.
Hayo yalibainishwa na Mkurugenzi Mkuu wa taasisi hiyo, Kamishna wa Polisi, Valentino Mlowola wakati alipozungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana kuhusu taarifa mbalimbali zinazotolewa na mbunge huyo kuhusu ushahidi aliouwasilisha kwenye taasisi hiyo.
Kamishna Mlowola alisema mbunge huyo kwa takribani mara tatu alifika katika ofisi za Takukuru na kuwasilisha kile alichokiita ushahidi, lakini mara baada ya kuwasilisha taarifa hizo kwa Takukuru huitisha vyombo vya habari na kuelezea yale yaliyojadiliwa na taasisi hiyo.
“Hiki ni chombo kinachojiendesha kwa mujibu wa sheria, hakishinikizwi wala kuingiliwa na mtu yeyote. Na kinapokea kwa mujibu wa sheria na taratibu taarifa za siri au wazi kutoka kwa mtu yeyote, Nassari anachokiita ushahidi sisi tunakiita taarifa mpaka pale uchunguzi wetu utakapokamilika,” alisisitiza Mlowola.
Alisema Oktoba 2, mwaka huu, mbunge huyo akiambatana na Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema na Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa, wote wa Chadema, walifika katika ofisi za Takukuru na kuwasilisha taarifa zao kuhusu matukio ya rushwa yaliyotokea mkoani Arusha.
Alisema Oktoba 14 pamoja na Oktoba 16, mwaka huu, Nassari pia aliwasilisha tena maelezo yake kuhusu suala hilo la rushwa kwa Takukuru na kila alipoondoka alifanya mkutano na waandishi wa habari na kuelezea yaliyojiri wakati akiwasilisha taarifa hizo.
Mkuu wa Takukuru alisema kwa mshtuko taasisi hiyo ilishangaa kuona mbunge huyo na wenzake, wakifanya vikao na waandishi wa habari na kuzungumzia kwa undani yaliyojiri hadi yale ambayo hayakupaswa kuzungumzwa kutokana na kuharibu uchunguzi.
Alisema kazi ya Takukuru ni kupokea taarifa za rushwa na ubadhirifu na kuzifanyia uchunguzi wa kina na ikishathibitika kuwepo kwa tatizo, hufungua jalada na kuliwasilisha katika ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka kwa ajili ya hatua za kisheria kuchukuliwa.
“Kwetu sisi Nassari alikuwa mtoa taarifa na tuna jukumu la kumlinda kwa mujibu wa sheria, lakini safari hii yeye mwenyewe anaji expose mbele ya vyombo vya habari. Ninachoona Nassari anataka kulifanya suala hili kuwa la kisiasa badala ya kisheria,” alisema.
“…Namuonya ameshatupa taarifa atuache tufanye kazi kwa mujibu wa sheria. Na akiendelea tutamchukulia hatua za kisheria bila kuathiri taarifa alizotuletea,” alisisitiza. Alitoa onyo hilo pia kwa watu wengine, wanaofikiri kuwa wanaweza kuishinikiza Takukuru na kuingiza katika masuala ya kisiasa kuwa wakome, kwani inafanya kazi wa mujibu taratibu na sheria zilizopo.
Mbunge huyo hivi karibuni baada ya kuwasilisha taarifa yake kwa Takukuru, alizungumza na waandishi wa habari nje ya ofisi za taasisi hiyo Upanga na kubainisha wazi kuwa amewasilisha ushahidi mwingine kwa Takukuru kuhusu tuhuma za ununuzi wa madiwani wa Chama hicho.
Alidai aliwasilisha ushahidi huo ukiwa kwenye ‘flash’, ambayo amekuwa akizunguka nayo kila mahali. Madiwani wanane wa Chadema walijiuzulu hivi karibuni, wakieleza kumuunga mkono Rais John Magufuli kwa utendaji kazi wake, jambo ambalo Nassari anadai siyo kweli, bali walinunuliwa.
“Huu ni ushahidi wa tatu na kadri upelelezi ukiwa unaendelea nitaleta mwingine, hii ni kama filamu ya Isidingo,” alisema Nassari na kuongeza kuwa alitarajia Rais Magufuli angewachukulia hatua wateule wake wanaohusishwa katika sakata hilo ili kupisha uchunguzi ufanyike kwa uhuru

No comments: