Majaliwa, wakuu EAC wabana mawaziri
WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa ameungana na viongozi wengine wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kukemea rushwa na uroho wa madaraka, akiwataka mawaziri wa Tanzania watumie madaraka yao kwa manufaa ya Taifa na kamwe wasiyatumie kama fursa ya kujitajirisha wao binafsi.
Kauli hiyo imekuja siku chache baada ya Rais wa Rwanda, Paul Kagame naye kuwaagiza kuwa, kazi kubwa waliyonayo mbele yao ni kuijenga Rwanda na kwamba hatavumilia mawaziri wazembe, watakaojinufaisha kwa fedha za umma na kutumia vibaya madaraka waliyopewa.
Aliyasema hayo saa chache baada ya kuwaapisha jijini Kigali, Rwanda na na kusisitiza kuwa, wanachotaka Wanyarwanda ni maendeleo, hivyo wawe tayari kufanya kazi kwa juhudi na maarifa. Alikuwa ametoka kutangaza baraza jipya, baada ya kuchaguliwa kuiongoza Rwanda katika awamu ya tatu.
Amekuwa madarakani tangu mwaka 2000, na kabla ya hapo, kwa miaka sita alikuwa Makamu wa Rais na Waziri wa Ulinzi. Akisisitiza uchapakazi, alisema anataka viongozi hao wawe wabunifu, lakini pia wawe na ushirikiano na mshikamano, lengo likiwa kuwaharakishia Wanyarwanda maendeleo na ustawi wa nchi yao kwa ujumla.
Kauli kama hizo zimekuwa zikitolewa pia na Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta, Yoweri Museveni wa Uganda, Pierre Nkurunziza wa Burundi na Salva Kiir wa Sudan Kusini, wakilenga kuzifanya nchi za EAC kuwa mfano wa kuigwa katika mapambano dhidi ya rushwa, lakini pia kuwa na kasi katika kujiletea maendeleo.
KAULI YA MAJALIWA
Aliyasema hayo jana alipozungumza na baadhi ya Mawaziri, Manaibu na Makatibu Wakuu katika kikao kilichofanyika jijini Dar es Salaam, muda mfupi kabla ya kusafiri kwenda Canada kwa ziara ya kikazi.
Alisema Rais, Dk John Magufuli anayeongoza mapambano dhidi ya rushwa, amesisitiza kwamba amewateua ili wafanye kazi na kamwe wasitumie madaraka waliyopewa kwa maslahi yao binafsi.
“Madaraka haya ya Uwaziri si fursa ya kujipatia utajiri, tunatakiwa tufanye kazi kwa weledi, uadilifu, bidii na uaminifu mkubwa ili kuondoa kero za wananchi kwa wakati.” Alisema Mawaziri na Manaibu Waziri wazingatie Katiba ya nchi, Kanuni, Taratibu na Miongozo mbalimbali ya Serikali katika utekelezaji wa majikumu yao ya kila siku.
Waziri Mkuu amesema Mawaziri hao wanatakiwa wasimamie utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa miaka kuanzia mwaka 2016/2017 hadi 2020/2021. Pia utekelezaji wa ahadi zote zilizopo kwenye Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015 pamoja na ahadi alizozitoa Rais Dkt Magufuli wakati wa kampeni za uchaguzi.
Amewaagiza Mawaziri wahakikishe wanakwenda kufanya ufuatiliaji wa tathmini ya utekelezaji wa mipango mbalimbali ya maendeleo inayohusu sekta zao. Pia amewataka Mawaziri hao wakasimamie kikamilifu ukusanyaji wa mapato na kuanzisha vyanzo vipya vya ukusanyaji pamoja na kudhibiti mianya ya upotevu.
Hata hivyo Waziri Mkuu amewataka Mawaziri hao wakapunguze urasimu katika utekelezaji wa malengo ya Serikali kwa sababu wananchi wanahitaji kuhudumiwa kwa wakati. Mawaziri waliohudhuria kikao hicho ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais –TAMISEMI Suileiman Jaffo na Manaibu wake, Joseph Kandege na George Kakunda, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu na Naibu wake, Dk Faustine Ndungulile.
Wengine ni Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Isack Kamwelwe na Naibu wake, Jumaa Aweso, Waziri wa Viwanda na Biashara, Charles Mwijabe na Naibu wake, Stella Manyanya, Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Hamisi Kigwangalla na naibu wake, Josephat Hasunga, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako na naibu wake, William Ole Nasha, Naibu waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega na Makatibu Wakuu wa Wizara hizo.
Wakatihuohuo, Waziri Mkuu aliondoka nchini jana kwenda nchini Canada kwa shughuli za kikazi. Akiwa Canada, anatarajiwa kufanya mazungumzo na viongozi waandamizi wa sekta mbalimbali za kipaumbele. Canada ni moja ya nchi zenye ushirikano wa muda mrefu na Tanzania katika nyanja za kisiasa, kijamii na kiuchumi.
No comments:
Post a Comment