MAHAKAMA Kuu Kanda ya Dar es Salaam imepanga Oktoba 19 hadi 23 mwaka huu kuanza kusikiliza kesi ya mauaji bila kukusudia ya aliyekuwa nguli wa fi lamu nchini, Steven Kanumba inayomkabili mwigizaji wa fi lamu maarufu nchini, Elizabeth Michael “Lulu” (pichani).
Lulu aliye nje kwa dhamana atapanda kizimbani mahakamani hapo baada ya kusomewa maelezo ya awali karibu miaka miwili na nusu iliyopita. Msanii huyo anakabiliwa na kesi hiyo akidaiwa kumuua Kanumba bila kukusudia kinyume cha Kifungu cha 195 cha Kanuni za Adhabu.
Inadaiwa Lulu alimuua Kanumba bila ya kukusudia Aprili 7, 2012 nyumbani kwa marehemu huyo Sinza Vatican, Dar es Salaam. Kwa mujibu wa ratiba ya vikao vya kesi za mauaji ya bila kukusudia iliyotolewa na Mahakama Kuu Dar es Salaam jana, kesi hiyo itasikilizwa siku hizo na Jaji Sam Rumanyika. Kesi hiyo inaanza kusikilizwa baada ya kupangiwa Jaji kufuatia upelelezi kukamilika.
Mara ya kwanza Lulu alipandishwa kizimbani Aprili 11, 2012 mbele ya Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Jijini Dar es Salaam wakati huo, Augustina Mbando ambapo alisomewa mashitaka ya mauaji.
Hata hivyo, Februari 18, 2014 akisomewa maelezo ya awali Lulu alikiri mahakamani kuwa na uhusiano wa kimapenzi na Kanumba na pia kusema kulikuwepo ugomvi baina yao siku ya tukio la kifo cha mwigizaji huyo.
Lulu aliachiwa kwa dhamana Januari 29, 2013 baada ya kesi hiyo kubadilishwa hati ya mashitaka kutoka kwenye kesi ya mauaji kwenda mauaji ya bila kukusudia ambapo badiliko hilo lilimpa nafasi ya kupata dhamana.
Katika kesi ya msingi namba 125 ya mwaka 2012, inadaiwa Aprili 7, 2012 Sinza Vatican Lulu alimuua Kanumba bila kukusudia. Lulu alipelekwa rumande gereza la Segerea hadi mashitaka yalipobadilishwa akapata dhamana.

No comments: