ALIYEKUWA Katibu Mkuu wa chama cha siasa cha ACT Wazalendo, Samson Mwigamba na wenzake tisa, wamejivua uanachama wa chama hicho na kutangaza kujiunga na Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Mwigamba alieleza hayo jana alipozungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, na kuongeza kuwa wamefikia uamuzi huo baada ya kuona uongozi wa sasa wa ACT Wazalendo unachepuka kwa kasi mno nje ya chama tofauti na matarajio yaliyokuwepo. Alisema wameondoka ACT Wazalendo na kujiunga na CCM kwa kuwa ndicho chama kinachoakisi kwa karibu itikadi, falsafa na sera za chama walichotoka.
“Tumejiridhisha kuwa mpangilio wa sasa wa CCM na serikali yake upo katika misingi hii, na Serikali ya Awamu ya Tano ya Dk John Magufuli inaitekeleza misingi hii kwa utashi mkubwa mno,” alieleza Mwigamba na kuongeza: “Tumeamua kujiunga na CCM ili tuendelee kuwa sehemu ya mapambano ya kurudisha nchi katika misingi yake kama ambavyo tulidhamiria ndani ya chama chetu cha zamani.”
Alisema pia wamekwenda CCM kwa kuwa Serikali ya Magufuli ipo katika vitakubwa dhidi ya rushwa na ufisadi, na hivi sasa Tanzania ni kinara wa mapambano dhidi ya rushwa. “Lakini sasa upinzani ambao ndiyo uliasisi vita dhidi ya ufisadi umegeuka kuwa ndiyo watetezi wa mfumo wa kinyonyaji ulioitesa nchi kwa miaka mingi. Sisi tumeamua kujitenga na aina hii ya upinzani,” alifafanua Mwigamba.
Alisema wameamua kujitenga na upinzani unaokerwa na mafanikio ya serikali, kwa kuwa tangu wanachama wenzao Profesa Kitila Mkumbo na Anna Mghwira walipoteuliwa na Rais John Magufuli, kufanya kazi katika utumishi wa umma serikalini, wamekuwa wakikerwa na kutishwa katika utekelezaji wa majukumu yao, hususan wanapoelezea mafanikio ya serikali.
Profesa Mkumbo ambaye alikuwa Mshauri Mkuu wa ACT-Wazalendo, aliteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji na Umwagiliaji Aprili 4, mwaka huu, kuchukua nafasi ya Mhandisi Mbogo Futakamba ambaye amestaafu. Kwa upande wake, Anna Mghwira ambaye alikuwa Mwenyekiti wa Taifa wa chama hicho na mgombea urais wa ACT-Wazalendo katika uchaguzi mkuu wa 2015, aliteuliwa Kuwa Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Juni mwaka huu, kuchukua nafasi ya Said Mecky Sadiki aliyejiuzulu.
Mwigamba alikuwa miongoni mwa watu wa mwanzo kuanzisha ACT Wazalendo, na alijiunga nayo mwaka 2014. Alishika nyadhifa mbalimbali ikiwemo ya Katibu Mkuu wa chama, Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama pamoja na Mwenyekiti wa Kamati ya Kampeni na Uchaguzi.
Ofisa Habari wa chama hicho, Abdalah Khamis alisema Mwigamba aliandikiwa barua ya kuitwa leo ili aseme ni sehemu gani ambayo misingi ya chama hicho ilikiukwa. “Aliandikiwa barua aje atoe ufafanuzi nini kimekiukwa na kipi kiboreshwe. Kama kiongozi alitakiwa azungumze. Hatujui analalamikia nini kwa kuwa alikuwa na nafasi ya kueleza hilo kwenye Kamati ya Uongozi,” alisema Khamis, na kusikitishwa na Mwigamba kwa kuwatambulisha wanachama wengine waliohamia CCM kuwa walikuwa viongozi, akidai hawakuwa hivyo.
No comments:
Post a Comment