KAMISHNA mmoja kati ya makamishna saba wa Tume ya Uchaguzi na Mipaka ya Kenya (IEBC), Roselyn Akombe (pichani) amejiuzulu wadhifa wake, ikiwa ni siku saba zimebaki kufikia uchaguzi mpya wa rais utakaofanyika Oktoba 26, mwaka huu.
Ofisa huyo alitoa taarifa ya kujiuzulu kwake akiwa jijini hapa na kusema hawezi kuendelea kufanya kazi katika tume hiyo aliyodai kuwa imegawanyika. Alisema kujiuzulu kwake pia kumechangiwa na hali ya mazingira ya sasa ya kisiasa nchini humo huku akisisitiza kuwa uchaguzi huo ukifanyika Oktoba 26 hautakuwa huru wala wa haki. “Siwezi kuendelea kufanya kazi katika mazingira kama hayo, kuna kila dalili zinazoonesha wazi kuwa uchaguzi hauwezi kuwa huru wala wa haki,” alisema Akombe.
Akombe aliondoka Kenya Oktoba 17 kwenda Dubai kushuhudia uchapishaji wa karatasi za kupigia kura, lakini akaamua kwenda Marekani ambako pia ana uraia wa nchi hiyo. Kujiuzulu kwa Akombe ni pigo kwa tume hiyo ambayo ilikuwa inamtegemea kuzungumza kwa niaba yake na kuitetea mara kwa mara. “Tume ijitokeze wazi, iwe na ujasiri na kusema kuwa uchaguzi huu hauwezi kuwa huru na haki katika mazingira haya,” aliongeza Akombe.
Alisema akiwa Kenya alikuwa anapata vitisho kuhusu maisha yake na huenda asirejee humo kwa muda. Baada ya Akombe kutoa tamko hilo, Mwenyekiti wa IEBC, Wafula Chebukati alizungumza na vyombo vya habari na kusema Akombe alikuwa mmoja wa ofisa bora wa tume hiyo aliyetegemewa na kwamba kujiuzulu kwake kumechangiwa na siasa chafu za wanasiasa nchini Kenya. “Wakenya wenzangu, nchi yetu imebarikiwa kuwa na watu wenye akili duniani na wanaotumia vizuri vipaji vyao kwa manufaa ya nchi zao kama alivyokuwa Akombe, lakini siasa chafu zinazofanywa na wanasiasa wetu zimesababisha ashindwe kufanikisha azma yake kwa taifa hili,” alisema Chebukati.
No comments:
Post a Comment