MAKUBALIANO YA AWALI KATI YA TANZANIA NA KAMPUNI YA BARRICK GOLD YAONYESHA MWANZO MZURI


RAIS John Magufuli amesema kufikiwa makubaliano kati ya Tanzania na Kampuni ya Barrick Gold Corporation ni mwanzo mzuri, na kwamba Tanzania inaweka mwelekeo ambao haujawahi kuwekwa kokote barani Afrika katika udhibiti wa rasilimali zake.
“Sasa Barrick ni ndugu zetu, msikubali mazungumzo tuliyoyaanza kuingiliwa na watu wengine, tumeweka mwelekeo ambao haujawahi kufanyika popote Afrika, huu ni mwanzo wa kutengeneza Tanzania mpya,” alisema Rais Magufuli. Alitoa kauli hiyo jana Ikulu, Dar es Salaam, wakati wa kutiwa saini kwa makubaliano baada ya Kamati maalumu ya mazungumzo baina ya timu ya wataalamu wa Tanzania na Kampuni ya Barrick Gold Corporation kukamilika.
Katika hafla hiyo iliyofanyika baada ya mazungumzo hayo yaliyochukua takribani miezi mitatu kukamilika, Waziri wa Sheria na Katiba, Profesa Palamagamba Kabudi ambaye pia ndiye Mwenyekiti wa Kamati hiyo ya mazungumzo aliongozana na baadhi ya wajumbe wake, pamoja na Mwenyekiti Mtendaji wa Barrick, Profesa John Thornton.
Akizungumza baada ya kutiwa saini kwa makubaliano hayo ambayo Kampuni ya Barrick imekubali kulipa Dola za Marekani milioni 300 (zaidi ya Sh bilioni 700), kama malipo ya kuonesha nia njema ya kufidia fedha zilizotokana na upotevu wa mapato kupitia biashara ya kampuni hiyo, Rais Magufuli alisema huo ni mwanzo mzuri.
“Huu ni mwanzo nzuri wa kutengeneza Tanzania mpya na sasa Barrick ni ndugu zetu tumeanza mazungumzo vizuri na tumefikia hatua nzuri ambapo wamekubali kutoa dola milioni 300, wametambua msimamo wetu ndiyo faida ya mazungumzo,” alisema Rais Magufuli. Aidha, Rais Magufuli ameafiki kuundwa kwa kamati ndogo itakayohusisha pande zote mbili za mazungumzo ili kupitia nyaraka zote za malipo na kuangalia maeneo yenye utata ili kuangalia jinsi ya kutafuta suluhu.
“Chochote kinawezekana kinachohitajika ni uaminifu kati ya pande mbili, tutafikia muafaka kwa mazungumzo, ila wamefahamu kuwa hatutaki kuchezewa tena, tumekuwa shamba la bibi kwa muda mrefu, sasa basi,”alisema Rais Magufuli. Mbali na kusifia hatua ya mazungumzo iliyofikiwa na pande zote mbili, Rais Magufuli aliitaka kampuni hiyo ya Barrick kuwasilisha fedha hizo haraka kwa sababu zina kazi ya kufanya na kusisitiza kuwa nchi itaendelea kulinda rasilimali zake zote kwa faida ya Watanzania.
Alisema pamoja na kampuni hiyo kukubali kulipa kianzio cha fidia ya biashara ya madini, pia wamekubali kuanzia sasa Tanzania itakuwa ikipata nusu ya faida ya biashara ya kampuni hiyo ya madini ya dhahabu sambamba na kumiliki hisa kwa asilimia 16. Mbali na kulipa faida na nchi kumiliki hisa hizo, Rais Magufuli alisema kampuni hiyo pia itaendelea kulipa kodi nyingine kama kawaida zikiwemo za halmashauri pamoja na menejimenti ya kampuni hiyo itaundwa kwa kuwahusisha pia Watanzania.
Akizungumzia suala la kuundwa kwa menejimenti ya kampuni hiyo itakayowashirikisha Watanzania, Rais Magufuli alitoa mwito kwa vyombo vitakavyohusika na usaili wa watu wenye sifa, kuangalia kwa makini tabia na mwenendo wao, ili kuhakikisha wanapatikana watu waadilifu na siyo wezi.
“Tumesikia katika makubaliano yao menejimenti mpya ya Kampuni ya Barrick sasa itaundwa kwa kuzingatia watu wa Tanzania, sasa hii ni faida kwetu labda tuweke majizi, ila nitoe rai kwa vyombo vitakavyohusika kutafuta watu wenye sifa, kuhakikisha wanawachunguza kwa undani na kujua tabia zao ili wapatikane watu sahihi kwa faida ya nchi,” alisisitiza Rais Magufuli.
Akiipongeza kamati hiyo, Rais Magufuli alisema imefanya kazi yake kwa weledi mkubwa na uzalendo kwani walikuwa na uwezo wa kupindisha mambo au kula rushwa, lakini wamekuwa waaminifu kwa faida ya taifa.
“Naipongeza kamati, mngeweza kukaa kimya au kula rushwa lakini pamoja na ukubwa wa wajumbe wa Barrick ambao nasikia walifika 25 na nyie mko nane, lakini mmeonesha uwezo wenu mkubwa na nidhamu, na wametambua jambo hili siyo jepesi na mmefikia hatua nzuri, nitaandaa siku ya kuwapongeza hata kwa kuwapa cheti kwa kuwa mmejitolea maisha yenu,” alisema Rais Magufuli.

No comments: