Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri mkuu Sera,Bunge,Kazi,Vijana,Ajira na watu wenye ulemavu Mhe. Genesta Mhagama(katikati) akiwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Selemani Jaffo(tatu kulia), Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu(tatu kushoto) pamoja na viongozi wengine baada ya uzinduzi wa namba maalumu ya kuchangia mfuko wa udhamini wa kudhibiti Ukimwi
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu Mhe. Genesta Mhagama amemkabidhi Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Selamani Jaffo Tsh mil 200,000 kwa ajili ya ukarabati wa kituo cha Afya Mererani ikiwa ni ahadi ya Rais Dr.John Magufuli aliyoitoa wakati wa ziara yake Mkoani hapo mwezi uliopita.
Ujenzi wa Kituo hicho ambao utaboresha huduma za mama na mtoto pia ni maalumu kwa ajili ya kusaidiazaidi katika kutoa huduma kwa watu walioathirika na virusi vya ukimwi katika Wilaya ya Simanjiro.
Ikiwa ni miongoni mwa Wilaya zilizoathirika zaidi na virus vya Ukimwi haswa katika eneo la mererani imeonekana inahitaji msaada wa haraka ili kudhibiti au kupunguza kabisa tatizo hilo katika jamii ya eneo hilo.
Fedha hizo zimetoka katika mfuko wa udhamini wa udhibiti wa Ukimwi ambao ulizinduliwa mwishoni mwa mwaka jana na kuanza kazi rasmi ya kukusanya fedha kutoka katika vyanzo vya ndani kusaidia katika mapambano dhidi ya Ukimwi.
Akipokea Hundi hiyo Waziri wa Tamisemi Mhe. Selemani Jaffo kabla ya kumkabidhi Mkuu wa Mkoa wa Manyara Mhe Joel Bendera amesema umefika wakati ambapo jamii ya watanzania wanapaswa kuunga mkono jitihada hizi ili kupunguza maambukizi ya virusi vya Ukimwi.
Wakati huo huo Tume ya kudhibiti Ukimwi Tanzania (TACAIDS) imezindua rasmi namba maalum ya kuchangia Mfuko huo wa udhamini wa Kudhibiti Ukimwi.
Katika uzinduzi huo ambapo mgeni Rasmi alikua Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera,Bunge,Kazi,Vijana,Ajira na Walemavu Mhe. Genesta Mhagama alitaja namba ya uchangiaji wa mfuko huo kuwa 0684909090 na kwamba kila mwananchi anahimizwa kuchangia Fedha ili fedha itakayopatikana isaidie watu wanaoishi na Virusi vya Ukimwi.
Katika hatua Nyingine Waziri Mhagama alimkabidhi hundi ya Tsh. Milioni 660 kwa Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe.Ummy Mwalimu kwa ajili ya kununua dawa aina ya Contrimaxozole za watu wanaoishi na VVU.
Fedha zote hizi zimetoka katika Mfuko wa udhamini wa kudhibiti Ukimwi.
No comments:
Post a Comment