MHE:LUKUVI ATOLEA UFAFANUZI WA BOMOA BOMOA


Image result for PHOTO OF WILLIAM LUKUVI
SERIKALI imewaondoa hofu wananchi juu ya tishio la bomoabomoa ya nchi nzima kwa waliojenga bila kuwa na vibali vya ujenzi, ikisisitiza si wote watakaohusika, bali `matapeli’ na wavamizi wa maeneo ya watu wengine.
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi ameongeza kuwa, wananchi waliojengwa kwenye maeneo yasiyopimwa na wasio na vibali vya ujenzi, hawatabolewa nyumba zao, kama umma ulivyopotoshwa.
Lukuvi alisema hayo Ikulu jijini Dar es Salaam jana wakati wa hafla ya kuwatunuku vyeti wajumbe walioteuliwa na Rais John Magufuli kuchunguza biashara ya madini. Kwa mujibu wa Lukuvi, alilazimika kufafanua hivyo baada ya jana baadhi ya vyombo vya habari, hususani magazeti, kumnukuu vibaya kwa kuandika kuwa wananchi waliojenga kwenye maeneo yasiyopimwa na bila kuwa na vibali watabolewa nyumba zao.
“Asilimia 85 ya wananchi wanaishi kwenye makazi holela katika maeneo ambayo hayakupimwa. Serikali hatutabomoa nyumba zao ila tunachokifanya ni kurasimisha makazi yao ili waishi mahali salama, wapate huduma za kijamii na waweze kulipa kodi kwa serikali,” alieleza Waziri Lukuvi.
Lukuvi alisema nyumba zitakazobolewa ni zile zilizojengwa kwenye viwanja walivyoporwa wananchi wanyonge na masikini. Alisema Serikali haitafumbia macho watu wenye nguvu ya pesa, wanaoshirikiana na baadhi ya watumishi wasio waaminifu wizarani na kwenye halmashauri, kunyang’anya viwanja vya wananchi masikini na kubadilisha umiliki wa viwanja hivyo.

No comments: