WAAJIRI SERIKALINI KUBANWA ASEMA MKUCHIKA


WAZIRI wa Nchi, Ofi si ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Mkuchika amewaagiza waajiri wote wa serikali kuhakikisha wanatoa vielelezo vinavyotakiwa vya watumishi wao ndani ya siku 14 pale wanapoagizwa kufanya hivyo na Tume ya Utumishi wa Umma, kinyume cha hapo watawajibishwa.
Mkuchika alitoa agizo hilo jana alipotembelea Tume hiyo jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kujionea shughuli zinazofanywa. Aliwataka waajiri hao kuzingatia sheria kwa kuwa imeelezwa kuwa wamekuwa ndio chanzo cha kuchelewesha kesi za waajiriwa kwa kutokutoa ushirikiano kwa haraka.
“Waajiri zingatieni sheria, pale tume inapotaka kupata vielelezo inataka ijiridhishe. Kesi zinachukua muda mrefu kama hakuna vielelezo lazima zichelewe,” alisema Mkuchika. Kwa upande mwingine, aliwataka wafanyakazi wa tume hiyo kutekeleza majukumu yao ya kazi, huku wakijiepusha na rushwa kwa kuwa eneo wanalofanyia kazi lina ushawishi mkubwa.
Pia aliahidi kushughulikia changamoto mbalimbali zinazokabili tume hiyo zikiwemo za rasilimali fedha, watu na usafiri. Naye Kaimu Naibu Katibu wa Tume hiyo, Richard Odongo alisema tume hiyo inapokea na kushughulikia rufaa na malalamiko ya watumishi wa umma ambao hawajaridhika na mamlaka zao za nidhamu.

No comments: