Klabu ya Simba imemtangaza Masudi Juma ria wa Burundi kuwa kocha wake msaidizi akichukua nafasi ya Jackson Mayanja.
Kocha huyo mpya aliwasili mchana wa leo nchini kwa ajili ya kusaini mkataba wa kufundisha Simba akisaidiana na Joseph Omog.
Baada ya kuwasili Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) mjini Dar es Salaam, Juma alisema: “Nimekuja kuwa kocha Msaidizi wa Simba chini ya kocha aliopo kwa sasa. Nataka kusaidia Simba ifanikiwe kutwaa mataji zaidi, najua hiyo ndiyo kiu kubwa.”
Kocha huyo ambaye mwaka 1995 aliichezea Burundi katika michuano ya Vijana ya Dunia ya FIFA nchini Qatar alionekana kuwa mchangamfu katika mazungumzo yake.
Mshambuliaji huyo wa zamani wa Prince Louis ya Burundi, Inter Star za Burundi na Rayon Sport ya Rwanda amesema anafurahi kuja kufundisha Simba timu kubwa Afrika na anaamini atajifunza zaidi, hususan akifanya kazi chini ya kocha mzoefu zaidi, Omog.
Masudi Juma amesema atasaini mkataba na Simba kesho Ijumaa.
No comments:
Post a Comment