UTAFITI:VIFO VYA WANAUME NI VINGI ZAIDI YA VYA WANAWAKE


.


“MATOKEO ya utafiti huu yanatuonesha mahali tulipo na changamoto mbalimbali kuhusu ubora, utunzaji na utumiaji wa takwimu za vifo katika hospitali zetu. “Vile vile taarifa hii inaainisha vyanzo na sababu mbalimbali za vifo kwa wananchi tunaowahudumia katika hospitali zetu.
Ninaamini kuwa ripoti hii itaibua mjadala chanya na mawazo mapya ili kuboresha takwimu zetu za afya.” Yalikuwa maneno ya utangulizi ya Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Paul Ntinika alipomwakilisha Mkuu wa Mkoa, Amos Makala kwenye ufunguzi wa warsha kuhusu sababu za vifo katika hospitali za Tanzania. Huu ni utafiti uliofanywa na Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu nchini (NIMR).
Kwa mujibu wa Mtafiti Mkuu Kiongozi kutoka NIMR, Dk Leonard Moera, utafiti huu ulifanyika Julai 2015 hadi Juni 2016. Malengo yake yalikuwa ni kuainisha matukio ya vifo katika hospitali za nchini ili kutambua ongezeko la maradhi yanayoathiri jamii.
Ulichunguza pia uwepo, upatikanaji na ubora wa takwimu za vifo hospitalini. Dk Moera anasema utafiti huu ulihusisha hospitali 11, ikiwemo Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, hospitali za rufaa za mikoa na kanda, hospitali maalumu na za wilaya.
Hospitali ambazo takwimu hazikupatikana ni pamoja na Hospitali ya Wilaya ya Chunya iliyopo mkoani Mbeya. Mfuko wa Dunia wa kupambana na Ukimwi, Kifua kikuu na Malaria kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto ndiyo waliowezesha kufanyika kwa utafiti huu muhimu.
Mkuu wa wilaya anasema, kama ilivyoainishwa katika mpango mkakati wa sekta ya afya namba IV, serikali inachukua hatua mahususi kuboresha mfumo wa utoaji wa taarifa za afya ili kukidhi mahitaji ya ufuatiliaji wa huduma za afya.
Dhamira ya serikali ni kutumia mfumo wa kielektroniki katika ukusanyaji, uchanganuzi na matumizi ya takwimu. “Kwa utaratibu huu, ni matumaini yetu tutaongeza ubora wa takwimu tunazozalisha katika mfumo wetu wa tarifa.
Pamoja na hilo, serikali itatilia mkazo mafunzo ya watumishi na kuwakumbusha umuhimu wa kufuata miongozo ya kitaifa na kimataifa katika kuainisha vyanzo vya maradhi na vifo,” anasema Ntinika.
Mkuu huyo wa wilaya anaipongeza ripoti ya utafiti wa NIMRI akisema ni ya aina yake nchini kwa kuwa inaainisha upatikanaji na viwango au sababu za vifo vilivyotokea katika hospitali za Tanzania kwa kipindi cha miaka kumi kuanzia mwaka 2006 hadi 2015.
“Matokeo ya utafiti huu yanaonesha kuwa maradhi yanayoongoza katika kusababisha vifo nchini ni malaria, magonjwa ya mfumo wa kupumua, Ukimwi, upungufu wa damu na magonjwa ya moyo na mfumo wa damu,” anasema.
Hata hivyo, vifo vinavyotokana na malaria, Ukimwi pamoja na Kifua Kikuu vimepungua sana. Kwa mfano, vifo kutokana na malaria vimepungua kwa asilimia 47. Vifo vitokanavyo na Ukimwi vimepungua kwa asilimia 28 na kifua kikuu kwa asilimia 26 kutoka mwaka 2006 hadi 2015.
Pamoja na kupungua huko, takwimu za utafiti huu zinaonesha kuwa bado malaria ni ugonjwa unaoongoza kwa vifo vingi nchini huku Ukimwi ukishika nafasi ya tatu nyuma ya magonjwa ya mfumo wa kupumua.
Takwimu zinaonesha kuwa katika kipindi hicho (2006-2015), kati ya vifo 247,976 vilivyotokea, malaria iliongoza kwa asilimia 12.8, magonjwa ya mfumo wa kupumua asilimia 10.1, Ukimwi asiliamia 8.0, upungufu wa damu asilimia 7.8 na magonjwa ya moyo na mfumuko wa damu asilimia 6.3.
Pia kumekuwepo ongezeko kubwa la vifo kwa asilimia 128 vinavyosababishwa na magonjwa yanayoathiri kundi la watoto wachanga hasa wenye umri wa chini ya mwezi mmoja.
Kwa upande mwingine, vifo vinavyotokana na magonjwa yasiyoambukiza na ajali vimeongezeka. Katika miaka ya hivi karibuni, vifo vitokanavyo na ajali vimeongezeka kwa asilimia 16, saratani asilimia 24, kiharusi asilimia 27 na kisukari asilimia 11. Inaelezwa kuna dalili kuwa magonjwa haya yataendelea kuongezeka katika siku za usoni. “Hii ni ishara kuwa mafanikio yetu kupunguza magonjwa yasiyoambukiza yanaathiriwa na ongezeko la magonjwa yasiyoambukiza,” anasema Ntinika.
Ntinika anasema, “Kupungua kwa vifo kutokana na magonjwa makubwa ni dhahiri kuwa mikakati yetu katika magonjwa haya inafanikiwa. Hapa nawapongeza watumishi wote wa afya katika ngazi mbalimbali kwa mafanikiao haya makubwa.” Hata hivyo, anasema, baada ya kupitia na kuichambua ripoti hii amegundua kuwa watu wanakufa kwa magonjwa yanayozuilika.
“Ikiwa ni kweli kwamba malaria, Ukimwi, magonjwa ya mfumo wa kupumua, magonjwa yasiyoambukiza na ajali huua maelfu ya watu wetu, hii inatoa taswira kuwa tunayo kazi kubwa ya kufanya kuzuia vifo hivyo.
Mikakati mseto inahitajika kupambana na magonjwa ya makundi yote hayo,” anasema Ntinika. Utafiti unaonesha vifo vingi vimetokea katika hospitali za Dar es Salaam, Morogoro na Mwanza.
Idadi kubwa ya vifo ni katika kundi la wanaume. Mikoa inayoongoza kwa kuwa na vifo vingi kwenye kundi la wanaume kuliko wanawake ni Mara, Kilimanjaro, Kigoma, Pwani, Ruvuma na Rukwa.
Mtafiti mkuu kiongozi kutoka NIMR, Dk Moera anasema uzembe wa kutowahi matibabu ni chanzo cha wanaume nchini kukabiliwa na wimbi la vifo zaidi ya wanawake. Sababu ya vifo vingi vya wanaume ni utayari mdogo wa kwenda kuchunguza afya zao tofauti na ilivyo kwa wanawake.
“Wanaume ni wazito kwenda katika vituo vya tiba. Hata pale mtu anapojisikia tofauti ya mwili yaani maumivu ya kichwa au chochote mara nyingi ni watu wa kuhisi labda ni uchovu, na wakati mwingine utakwenda duka la dawa kutafuta dawa za kutuliza maumivu tu. “Hivyo mpaka unakwenda kwenye kituo cha tiba, tayari ugonjwa ulikwisha kuwa sugu mwilini hivyo kupona inakuwa vigumu,” anasema Dk Moera.
Anawasihi wanaume kubadili mitazamo na kupenda kuchunguza afya mara kwa mara hasa kutokana na kuwa mfumo wa maisha yao ni wa kukumbana na misukosuko mingi katika mazingira tofauti yakiwemo yaliyo hatari.
Utafiti pia unasema mikoa ya Mbeya, Iringa na Ruvuma bado inaongoza kwa vifo vitokanavyo na Ukimwi, hali inayoonesha kuwa bado kuna kazi kubwa ya kupunguza maambukizi ya Virusi vya Ukimwi (VVU).
Mkuu wa wilaya anasema taarifa ya utafiti huu ni muhimu sana kwa ajili ya kufanya uamuzi na kuandaa mipango kwa kutegemea ushahidi wa kitaalamu. Bila takwimu za uhakika si rahisi kujua ukubwa wa matatizo na changamoto za utoaji huduma za afya. “Bila takwimu sahihi, tutajikuta tunashughulika na matatizo yenye umuhimu mdogo na hivyo kutotumia rasilimali zetu ipasavyo.
Ni muhimu timu za menejimenti za mikoa za afya na hospitali zote kufanyia kazi mapendekezo ya ripoti hii ili kuboresha takwimu katika hospitali zetu,” anasisitiza Ntinika. Kaimu Mkurugenzi wa wa NIMR Mbeya, Dk Nyanda Elius na Mganga Mkuu Mkoa wa Rukwa, Dk Boniface Kasululu wanahimiza wadau wa afya kutumia taarifa za utafiti huo katika utekelezaji wao wa kila siku. Uwapo wa takwimu ni dira ya ufumbuzi wa jambo lolote. Ili takwimu zipatikane, ni muhimu utafiti ufanyike na uje na mapendekezo ya kufanyia kazi

No comments: