TETEMEKO LAIKUMBA MPANDA


TETEMEKO lililovikumba vitongoji na viunga vya Mji wa Mpanda mkoani Katavi pamoja na maeneo ya nchi jirani, ni la 5.2 katika kipimo cha richa.
Akizungumza jana mjini Dodoma, Mjiolojia Mwandamizi wa Wakala wa Jiolojia Tanzania (GST), Gabriel Mbogoni alisema kwa kawaida tetemeko la kipimo hicho hugusa eneo kubwa kutokana na ukubwa wake.
Mbogoni alisema tetemko hilo lilitokea kwa takribani sekunde 20 hadi 30. “Eneo hilo lililokumbwa na tetemeko lipo kwenye Bonde la Ufa, kwani ni kawaida kwa maeneo hayo kukumbwa mara kwa mara na matetemeko na kubwa zaidi lililowahi kutokea lilikuwa la mwaka 1969 ambalo hilo ni la mwaka 1982 la 5.0 kipimo cha richa na mengine madogo madogo ya 3.7, 3.8 na 4.0 katika kipimo cha richa.
Alisema tetemeko hilo la Mpanda, lilitokea saa 3.30.12 asubuhi, na kutokana na kutokea kwenye Bonde la Ufa inawezekana pia liligusa eneo kubwa mkoani Katavi, Rukwa na hata maeneo ya mpakani ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) na Zambia.
Mbogoni alisema maeneo yaliyokumbwa na tetemeko hilo ni la Kaskazini-Mashariki umbali wa umbali wa kilometa 46 kutoka mji wa Mpanda. “Eneo hilo lipo umbali wa kilometa 16 Kaskazini- Mashariki mwa mji wa Kalambo na umbali wa kilometa 100 Mashariki wa Mbuga ya Mahale iliyopo karibu na Ziwa Tanganyika,” alieleza.
Mbogoni alitoa ushauri kwamba, pale inapotokea kwamba kuna tetemeko, watu wasitoke ndani ya nyumba kama wamo humo kutokana na kasi yake ya kusafiri umbali wa kilometa nane hadi 13 kwa sekunde moja.
Alisema hayo baada ya kuambiwa kuwapo kwa taharuki kubwa kwa wakazi wa Mji wa Mpanda na wengi kuzikimbia nyumba zao. Miongoni mwa wakazi waliokumbwa na taharuki hiyo ni pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Raphael Muhuga ambaye wakati huo alikuwa kanisani na waumini wenzake.
Akizungumza na gazeti hili kwa njia ya simu, Muhuga alikiri kuwa tetemeko hilo lilikuwa kubwa la kutosha kwamba katika maisha yake hajawahi kushuhudia mtikisiko mkubwa wa ardhi. “Nilikuwa kanisani katika ibada ya misa takatifu ya Jumapili wakati huo.
Hakika lilikuwa kubwa la kutosha niliangalia saa lilianza saa tatu na dakika kumi na kudumu kwa dakika moja hivi, ilisababisha taharuki kubwa kwa waumini kanisani humo hususani watoto walikimbilia nje, sisi watu wazima tulikuwa tukiangalia paa la kanisa kama litatuangukia.
Mungu Mkubwa ibada iliendelea kama kawaida hadi mwisho,” alieleza. Alisema hadi sasa hakuna maafa yoyote ambayo yamesharipotiwa. Mkazi wa Mpanda Mjini, Adamu Juma alieleza kuwa wakati huo alikuwa akihemea sokoni, na alishuhudia wafanyabiashara wakitelekeza maduka yao na kukimbilia walikodhani ni salama kwa maisha yao.
“Wakati huo nilikuwa ndani ndipo ghafla nikahisi kuta za nyumba zikitikisika kwa nguvu nilitaharuki na kukimbilia chini ya uvungu wa meza ya chakula ili hata ukuta ukianguka usiniumize... Nilitetemeka sana kwa hofu,” alisema Mariam Yusufu anayeishi mjini Mpanda.
Katika siku 365 zilizopita, Tanzania imekumbwa na matetemeko ya ardhi manane yenye ukubwa mbalimbali kuanzia 4.4 hadi 5.9. Baadhi ya matetemeko ukiachia lile lililotokea jana Mpanda, Katavi lenye ukubwa wa magnitude 5.2 kina cha kilomita 10, miezi mitano iliyopita lilitokea tetemeko la magnitude 4.4 huko Misasi, Mwanza.
Aidha, miezi 7 iliyopita tetemeko jingine lilitokea Utete kwa kipimo cha Magnitude wa 4.9 na kina cha kilometa 12 huku tetemeko baya kabisa lilikuwa la Nsunga, Kagera Tanzania ambalo lilikuwa na ukubwa wa Magnitude 5.9 na kina cha kilometa 40.4: Pia eneo la Msanga Dodoma lilipatwa na tetemeko la ukubwa wa Magnitude 5.1 na kina cha kilometa 10. Imeandikwa na Magnus Mahenge, Dodoma na Peti Siyame, Mpanda.

No comments: