Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HESLB) imetoa orodha ya kwanza ya majina ya wanafunzi 10,196 kati ya wanafunzi 30,000 wanaotarajiwa kunufaika na mikopo ya elimu ya juu kwa mwaka mpya wa masomo 2017/2018.
Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi hiyo Abdul-Razaq Badru amewaambia waandishi wa habari katika mkutano uliofanyika ofisi kwake Mwenge jijiji Dar es salaam kuwa kufuatia hatua hiyo zaidi ya shilingi bilioni 34.6 tayari zimetengwa kwa ajili ya wanafunzi hao waliopitishwa.
Badru alibainisha kuwa kwa mwaka wa masomo wa 2017/2018 Serikali imetenga zaidi ya shilingi bilioni 108.8 kwa ajili ya wanafunzi hao wapya 30,000 wanaotarajiwa kujiunga na vyuo vikuu.
Kwa wanafunzi waliopata udahili katika chuo zaidi ya kimoja ambao wana sifa za kupata mkopo, Badru ameeleza kuwa wanafunzi hao watapatiwa mikopo baada ya “kuthibitishwa na vyuo watakavyojiunga kwa ajili ya masomo kwa mwaka huu wa masomo 2017/2018” Mkurugenzi huyo amewaeleza waandishi wa habari kuwa lengo la Ofisi yake ni kuhakikisha majina ya wanafunzi wote waliofanikiwa kupata mkopo yanatolewa kabla ya vyuo kufunguliwa mwishoni mwa Oktoba.
“Orodha ya kwanza tayari inapatikana katika tovuti ya bodi ya mikopo www.helsb.go.tz na itatumwa kwa vyuo husika. Orodha nyingine zitafuata kadri taratibu za udahili na uchambuzi zitakavyokuwa zinaendelea kukamilika” Badru alibainisha.
Badru amefafanua kuwa kwa wanafunzi waliofaulu mitihani yao na wanaoendelea na masomo watatumiwa fedha zao vyuoni kuanzia leo. “Kiasi cha shilingi bilioni 318.6 kitatolewa kwa wanafunzi 93,295 wanaoendelea na masomo kwa mwaka wa masomo 2017/2018.
Tayari serikali imeshatuma fedha hizo, ambapo bodi inahakikisha fedha zinafika vyuoni kabla ya kufunguliwa kwa vyuo ili kuwaondolea wanafunzi usumbufu,” aliongeza Badru. Wakati huo huo, Kaimu Mkurugenzi wa Upangaji na Utoaji Mikopo wa Bodi hiyo Dk Veronica Nyahende amesema kuwa majina ya wanafunzi wote waliokosea majina yao yatafanyiwa uchambuzi na zoezi hilo likikamilika majina yao yatatolewa.
“Kwa mwaka huu tuliingia kwenye mfumo mpya ambao ni wa mtandao ambapo mwombaji akikosea anaomba upya na kuweka viambatanisho vyote ili kuthibitisha uhalali wake hivyo mwaka huu hatukuwa na utaratibu wa kuwaita waje hapa makao makuu,” alieleza Dk Nyahende.
Awamu ya kwanza ya wanafunzi hao 10,196 waliopata mkopo imepatikana baada ya bodi ya mikopo kupokea na kuchambua awamu ya kwanza ya majina ya wanafunzi 32,495 waliopata udahili katika chuo kimoja. Ikumbukwe kuwa sifa kuu za kupata mkopo ni mwombaji awe amepata udahili katika taasisi ya elimu ya juu inayotambuliwa na serikali.
No comments:
Post a Comment