ACT WAZALENDO WAPINGA UCHAGUZI ULIOFANYWA NA RAIS KWENYE BARAZA LA MAWAZIRI



Jana, Oktoba 7, 2017, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, amefanya teuzi mbalimbali ikiwemo uteuzi wa Katibu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
ACT Wazalendo tunasikitika kusema Kwamba kama ilivyo desturi, Rais ameamua kuyaweka pembeni matakwa ya Sheria yanayoongoza mchakato wa uteuzi wa Katibu wa Bunge na kuamua kujichagulia apendavyo.

Kutokana na unyeti wa nafasi ya Katibu wa Bunge, na kwa minajili ya kuweka ‘check and balance’ pamoja na kulinda uhuru wa Bunge, kwenye mchakato wa uteuzi wa nafasi husika, sheria imeweka utaratibu wa kufuatwa kwenye uteuzi wa Katibu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Hivyo basi, mbali na Rais kuwa na mamlaka ya kumteua Katibu wa Bunge kwa mujibu wa Ibara ya 87 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, anapaswa kuzingatia utaratibu uliowekwa na Sheria ya Utawala wa Bunge – The National Assembly (Admintration Act), 2015. Kwa mujibu wa Kifungu cha 7(3) cha Sheria hiyo, Rais atateua jina moja kutoka miongoni mwa majina matatu yaliyopendekezwa na Tume ya Huduma za Bunge. 

Jambo hili sio la hiyari. Ni sharti la lazima la sheria ambalo Rais analazimika kulifuata. Ndio maana kifungu husika kinasema “The Commision shall recommend three names” (Tume ni LAZIMA ipendekeze majina matatu). 
Wajumbe wa Tume ya Huduma za Bunge kwa mujibu wa Kifungu cha 12(2) cha Sheria ya Utawala wa Bunge ni wafuatao:
1. Ndg. Job Ndugai, Spika wa Bunge

2. Ndg. Tulia Akson, Naibu Spika wa Bunge
3. Ndugu Jenister Mhagama – Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu – Bunge
4. Ndg. Freeman Mbowe, Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni
5. Ndg. Magdalena Sakaya – Kamishna wa Bunge (CUF)
6. Ndg. Peter Msigwa – Kamishna wa Bunge (Chadema)
7. Ndg. Salim Hassan Abdullah Turky – (Kamishna wa Bunge – CCM)
8. Ndg. George Masaju
9. Ndg. Mary Chatanda (Kamishna wa Bunge – CCM)
10. Ndg. Kangi Lugola-(Kamishna wa Bunge-CCM)
11. Ndg. Mussa Hassan Zungu-(Kamishna wa Bunge-CCM)
Kwa taarifa tulizonazo, hakuna kikao chochote cha Tume ya Bunge kilichoketi na kupendekeza majina kwa Rais kwa ajili ya uteuzi wa Katibu wa Bunge. Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na wajumbe wote wa Tume ya Huduma za Bunge waliohojiwa na vyombo vya habari wamethibitisha pia kutofanyika kwa kikao hicho.
Hitimisho:
1. ACT Wazalendo tunaona kuwa uteuzi huu si tu ni mwendelezo wa Rais kufanya maamuzi bila kuzingatia sheria za nchi bali ni ushahidi mwingine wa wazi wa kudharau mhimili wa Bunge.
2. Ni matumaini yetu kuwa Bunge la Jamhuri ya Muungano na watu wote wanaopenda uhuru na uimara wa Bunge watasimama imara kuupinga uteuzi huu ambao ni kinyume na sheria.
3. Kama Rais hatatengua uteuzi huu na kufuata utaratibu uliowekwa na Sheria za nchi, ACT Wazalendo kitalifikisha suala hili Mahakamani ili kupata ufafanuzi wa mahakama.
4. Ni wakati muafaka kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali ambaye ndiye mwenye dhamana ya kuishauri serikali kwenye masuala ya kisheria kuwajibika. ACT Wazalendo tunaamini suala hili na vitendo vingine vya huko nyuma vimetokea kwa sababu ya moja ya sababu mbili. Inawezekana Mwanasheria Mkuu wa Serikali, kwa woga au uzembe, hamshauri Rais ipasavyo au Rais hafuati ushauri wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali. Katika yote mawili, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Kama anataka kulinda heshima yake binafsi na ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, hana budi KUJIUZULU.
Ado Shaibu

Katibu, Itikadi, Mawasiliano na Uenezi 
ACT Wazalendo 
Oktoba 8, 2017
Dar es salaam

No comments: