HUDUMA ZA UCHUNGUZI WA SARATANI PAMOJA NA MATIBABU YA AWALI SASA BURE KWENYE HOSPTALI ZA SERIKALI

Huduma za Uchunguzi wa Saratani kutolewa bila malipo

Waganga wa vituo vyote vya Serikali hapa nchini wametakiwa kuhakikisha huduma za uchunguzi wa saratani ya mlango wa kizazi na saratani ya matiti zinatolewa bila malipo yeyote sambamba na matibabu ya awali.
Hatua hiyo imekuja baada ya Serikali kuamua kuboresha huduma hizo kwa kununua mashine 100 za tiba mgando,mashine 9 za upasuaji mdogo ambazo zitatumika kwa ajili ya matibabu ya awali ya saratani kwa wanawake pamoja na mitungi 173 ya gesi ya carbon dioxide zitakazowezesha mashine hizo kufanya kazi.

Waziri wa Afya,Maendeleo ya jamii,Jinsia,wazee na Watoto Ummy Mwalim amebainisha hayo jijini Dar es salaam ambapo amevitaka vituo vya umma nchini kuhakikisha vinatenga siku maalum katika kila mwezi ili kuweza kuwahamasisha wanawake waweze kujitokeza kupata huduma hizo.

"natoa rai kwa wananchi hasa wanawake wenzangu kuhudhuria vituoni ili kuweza kupata huduma za uchunguzi mapema"alisema Ummy.

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Afya Dkt Faustine Ndugulile amesema kuwa katika kupunguza gharama za matibabu kwa wagonjwa wanaoenda kutibiwa nje,Serikali ya awamu ya tano imeamua kuboresha huduma za afya hususani upande wa saratani ili kuweza kuhakikisha wagonjwa hao wanatibiwa hapa nchini.

Ifahamike kuwa takribani wagonjwa wapya elfu 50 kila mwaka wanagundulika kuwa na saratani ,na idadi hii inakadiriwa kuongezeka kwa asilimia 50 ifikapo mwaka 2020.

No comments: