DR KIGWANGALA AFUTA UTARATIBU WA UTOAJI VIBALI VYA UWINDAJI

..
Katika kile alichoeleza kuwa ni
kuimarisha sekta ya maliasili na utalii iweze kutoa mchango unaostahili kwa
jamii na taifa kwa ujumla, Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi
Kigwangalla
 amesitisha utaratibu wa kuhuisha upya vibali vyote vya makampuni ya uwindaji wa kitalii ambavyo
vilitolewa mwaka huu mwezi Januari i
li kupisha utaratibu mpya wa utoaji wa
vibali hivyo kwa njia ya mnada.
Dk. Kigwangalla ametangaza uamuzi
huo jana mjini Dodoma katika mkutano alioutisha wa wadau wa sekta ya maliasili
na utalii ambao ulilenga kukusanya maoni, kero na kujadili changamoto
mbalimbali zinazoikabili sekta hiyo muhimu nchini kwa ajili ya kuzitafutia
utatuzi wa haraka.
“Kwa mamlaka niliyopewa na sheria ya
wanyamapori namba 5 ya mwaka 2009, nimeamua bila kushawishiwa na mtu yeyote
yule wala kushauriwa na mtu yeyote yule zaidi ya kusikiliza tu ushauri wa
kitaalamu na ushuari wa ndugu yangu Mhe.  Naibu Waziri, lakini  sasa
hivi ninavyotamka haya sijamshirikisha mtu yeyote yule, nimeamua kwa mamlaka
yangu, nasitisha vibali vyote  vya uwindaji wa makampuni ambavyo
vilitolewa mwaka huu mwezi Januari kwa maana ya ‘kurenew’ (kuhuisha).
“Nasitisha ili kupisha mchakato wa
kutengeneza taratibu mpya za kuendesha ugawaji wa vitalu kwa njia ya mnada,
tunataka twende kwenye ‘auction’ (mnada) ya vitalu, na auction (mnada) iwe ya
wazi, iwe na faida kubwa  zaidi, na natoa siku sitini utaratibu huo uwe
umekamilika ili tuweze kuendesha ‘auction’ (mnada) kabla ya muda wa kuanza kwa
awamu ya miaka mitano ambayo ni january 2018 mpaka 2022.
“Kwahiyo ndani ya siku sitini,
wataalam mkae mniletee utaratibu wa namna bora zaidi ya uwazi inayotoa haki ya
kugawa vitalu lakini pia yenye faida kubwa zaidi kama tunavyoelekezwa na mpango
wa taifa wa miaka mitano kwamba ni lazima vitalu vyote vifanyiwe ‘auction’
(mnada)”. alisema Dk. Kigwangalla.
Alisema utaratibu huo hautahusisha
vitalu vilivyopo kwenye maeneo yenye migogoro ya ardhi kwa sasa mpaka pale
migogoro hiyo itakapomalizika.
“Ni mwiko kugawa vitalu kwenye
maeneo yenye mgogoro, kuna maeneo kama vitalu vilivyopo Loliondo, kuna mgogoro,
ni mwiko kugawa vitalu, kuna maeneo kama Lake Natron kuna mgogoro, mwiko kugawa
vitalu, mpaka tutatue migogoro kwanza, Kama kuna mtu alipewa kibali huko nyuma
ajue hicho kibali cha renewal  kimekufa leo na mimi ndio nimekiua” alisema
Dk. Kigwangalla.
Kuhusu uwindaji wa Wenyeji kwenye
maeneo ya wazi uliosimamishwa kwa muda wa miaka miwili sasa, Dk. Kigwangalla
alitoa muda wa siku sitini kwa watendaji wa wizara yake kukamilisha masharti
mapya ya uendeshaji wa biashara hiyo na kuyawasilisha kwake aweze kuyasaini ili
kufungulia biashara hiyo.
“Natoa siku sitini, wataalam wetu
mnaohusika na utoaji wa vibali vya uwindaji wa wenyeji mkamilishe masharti
mapya mniletee nisaini tutoe vibali, hatuwezi kuzuia wenyeji wanufaike na
rasilimali ambazo ziko huko vijijini alafu tukaruhusu makampuni ya watu kutoka
nje kuja kuwinda wakaondoka na nyama, ni lazima tutoe haki kwa wazawa kama wapo
wanaovunja masharti sisi tudhibiti na tusimamie sheria” alisema Dk.
Kigwangalla.
Wakati huo huo, Waziri Kigwangalla
amemuagiza Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Mej. Jen. Gaudence
Milanzi kuwasiliana na Msajili wa Hazina kwa ajili ya kuanza mchakato wa
kuzirudisha serikalini hoteli za kitalii kumi zilizobinafsishwa miaka 1990 kufuatia
kushindwa kutimiza masharti ya mkataba wa uendeshaji.
“Niagize Katibu Mkuu wa Maliasili na
Utalii uwasiliane na mamlaka ambayo ina dhamana ya kushikilia mali zilizokuwa
za Serikali ambazo ziliuzwa kwa maana ya msajili wa hazina, umueleze nimetoa agizo
kwamba hizi hoteli zote ambazo zimekiuka masharti na hivyo kuathiri utendaji wa
sekta ya utalii nchini na hivyo kuathiri uchumi mpana wa taifa letu,
zichukuliwe na zirudi kuwa mali ya serikali ili serikali ipate fursa ya
kuzitangaza upya na kutafuta waendeshaji wapya watakaoweza kuendesha hoteli
hizi  kwa tija na ufanisi kwa maana ya kukuza sekta ya utalii ambayo
inachangia asilimia 17 ya pato la taifa.
“Nimetoa agizo hoteli hizi 10 ambazo
zimeshindwa kukidhi masharti ya mikataba ya mauziano, mchakato wa kuzirudisha
Serikalini uanze mara moja na ukamilike ndani ya siku sitini.
Alisema kumekuwepo na changamoto
kubwa ya uhaba wa vyumba katika sekta ya utalii hali iliyosababishwa na
ubinafsishaji wa hoteli 17 za Serikali uliofanywa miaka 1990 kwa nia njema ya
kuimarisha usimamizi na uendeshaji wa hoteli hizo kupitia sekta binafsi lengo
ambalo halikufikiwa kwa baadhi ya hoteli hizo.
“Baada ya kufanya uchunguzi katika
hoteli zote 17 tulizouza ni saba tu zinafanya vizuri, hoteli zinazofanya vizuri
na zimekidhi masharti yote ambayo yalikuwepo kwenye ile mikataba ni Kilimanjaro
Hotel, Kunduchi Beach Hotel, Mt. Meru Hotel, New Africa Hotel, New Safari
Hotel, Mafia Highland Hotel na Hotel 77.
“Hoteli 10 zimeshindwa kukidhi
masharti ya mikataba ya mauziano na mwaka ulioisha Serikali ilifanya uchunguzi
kwenye hoteli nyingine nne kati ya hizo 10 ambazo ni Robo Wildlife Lodge,
Seronera Wildlife Lodge, Ngorongoro Wildlife Lodge na Lake Manyara Hotel, na
zote zilionesha zipo chini ya kiwango na hazikidhi mahitaji.
“Kwa kuwa watu hawa wamekiuka
masharti ya ubinafsishaji kama walivyopewa wakati wananunua hizo hoteli ni
wakati muafaka sasa kwa Serikali kuvunja hii mikataba kuzichukua hizi hoteli na
kuzibinafsisha kwa watu wengine watakaoweza kuziendesha kwa faida lakini pia
kuziendesha kwa tija zaidi” alisema Dk. Kigwangalla.
Awali akijibu baadhi ya hoja za
wadau wa mkutano huo kuhusu wizara yake kuwa na vishawishi vingi vya rushwa na
fitna ambazo husababisha viongozi wengi kutodumu kwenye nafasi zao, Dk.
Kigwangalla alisema kamwe hatoruhusu hali hiyo ijitokeze kwa kuwa hata
aliyemteua anamjua vizuri kuwa ni muarobaini wa changamoto hizo.
“Mimi nipo hapa kwenye hiki kiti, na
nitakuwepo kama sababu ni hiyo ya maslahi, Mimi sihongeki, sinunuliki, na
sishawishiki, najua hata aliyeniweka hapa ananijua vizuri, kwahiyo alivyoniweka
hapa alishajua hii ni dawa, muarobaini.
“Watu wote humu ndani tuna njaa,
lakini njaa yangu nabaki nayo mwenyewe, bora nife kwa heshima zangu kuliko
kuaibika na kudharaulika kwa kuchukua rushwa ama kwa kutokutenda haki ama kwa
kumuonea mtu.
“Hilo nina uhakika nalo, kwa maana
ya rushwa, maslahi ya kibiashara hapana, hutonikuta mimi huko, na kama kuna
mdau mmoja anadhani kuna siku anafkiria anaweza kuja kuongea na mimi kwa
maslahi binafsi akaweka mbele mazingira ya rushwa, sana sana ataona nimemuaga
na kikao chetu kimeishia hapo, kwahiyo ukija kwangu njoo na ishu ambayo ipo
straight maslahi ya umma yapo ndani yake utaraibu wa kisheria upo”. Alisema Dk.
Kigwangalla.
Miongoni mwa maagizo mengine
aliyoyatoa kwenye kikao hicho kwa watendaji wa wizara yake ni kuandaa taratibu
za kuanzishwa kwa mwezi maalumu wa kuadhimisha utamaduni wa Mtanzania (Tanzania
Heritage Month), Makumbusho ya Marais wa Tanzania (Presidential Museum) na
Utalii wa Mabasi kwa Miji ya Dar es Salaam na Arusha (Dar Bus Tour/ Arusha Bus
Tour) ili kurahisisha utoaji wa huduma kwa watalii katika miji hiyo.
Katika mkutano huo wadau wa maliasii
na utalii walipata fursa ya kutoa maoni, mapendekezo ushauri na kero mbalimbali
wanazokumbana nazo katika sekta hiyo ambazo ziliahidiwa kufanyiwa kazi kwa
haraka na Waziri Kigwangalla.  Miongoni mwa ushauri na mapendekezo
waliyotoa ni pamoja na kuanzishwa kwa mamlaka moja inayosimamia rasilimali za
misitu nchini na kufunguliwa kwa biashara ya kusafirisha viumbe hai nje ya
nchi.
Mkutano huo wa siku moja
ulihudhuriwa na viongozi wakuu wa Wizara ya Maliasili ambao ni Naibu Waziri,
Mhe. Japhet Hasunga, Katibu Mkuu, Mej. Jen. Gaudence Milanzi, Naibu Katibu
Mkuu, Dk. Aloyce Nzuki, Wakurugenzi wa Idara na Wakuu wa taasisi zilizopo chini
ya Wizara hiyo.

Wengine ni wadau zaidi ya 200 kutoka
sekta mbalimbali ya maliasili na utalii ambao ni wawakilishi kutoka vikundi,
taasisi, vyama na vyombo mbalimbali vinavyoshughulika na utoaji wa huduma
katika sekta ya utalii, wanyamapori, misitu na nyuki pamoja na waandishi wa
habari. 


No comments: