SERA YA MPIRA YANUKIA


WAZIRI wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe amewataka wadau wa michezo watumie fursa waliyopewa kuhakikisha wanapitisha sera nzuri ya michezo ili ipelekwe bungeni mapema kwa ajili ya kutungwa sheria.
Hayo aliyasema jana wakati akifungua mkutano wa wadau wa michezo wa kupitisha Sera ya Michezo uliofanyika kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. “Mimi sitakaa hapa baada ya kufungua ila mnatakiwa mbishane na baadaye mtoke na kitu kizuri ambacho kitasaidia michezo yetu kuwa ya kulipwa,” alisema Dk Mwakyembe.
Dk Mwakyembe alisema michezo ni ajira yenye fedha nyingi duniani na kumtolea mfano mchezaji ghali duniani kwa sasa, Neymar wa PSG ya Ufaransa na kusema fedha anayolipwa kwa mwezi inaweza kuendesha wizara tano kwa mwaka.
Neymar alihamia PSG kutoka Barcelona ya Hispania kwa ada ya dola za Marekani milioni 263. Pia aligusa kwenye ngumi na kueleza kuwa anafurahi kuona mabondia wakicheza nje na kuchukua mataji makubwa na kumtolea mfano Ibrahim Class na kuahidi atahakikisha anatetea mkanda wake wa dunia wa GBC nchini.
“Sera itamke namna wanamichezo, serikali na vyama vitakavyonufaika na kulinda timu za taifa,” aliongeza Dk Mwakyembe. Kwa muda mrefu wadau wa michezo wamekuwa akidai Sera ya Michezo baada ya kutofanyiwa marekebisho kwa miaka mingi. Mara ya mwisho sera ya Michezo ilifanyiwa marekebisho mwaka 1995.
Kwa maana hiyo mambo mengi yaliyokuwa kwenye sera hiyo yamepitwa na wakati. Wadau waliokuwepo kupitia sera hiyo ni viongozi wa vyama mbalimbali vya michezo nchini na wakufunzi wa michezo kutoka vyuo vikuu.

Awali kabla ya kufungua mkutano huo, Dk Mwakyembe alifanya ukaguzi wa Uwanja wa Taifa ambao unafanyiwa marekebisho na Kampuni ya michezo ya kubahatisha ya SportPesa.

No comments: