MVUA KUBWA ZINATARAJIA KUJA TMA



MAMLAKA ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), imewataka wachimbaji wa madini katika migodi midogo midogo kuwa makini kwani ongezeko la maji katika udongo linaweza kusababisha mmomonyoko wa ardhi na maporomoko migodini katika kipindi hiki cha mvua za msimu.
Mkurugenzi Mkuu wa TMA, Dk Agnes Kijazi alisema hayo jana alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu utabiri wa mvua za msimu wa Novemba mwaka huu hadi Aprili mwakani.
Pia imezitaka mamlaka za miji pamoja na wananchi, kuchukua tahadhari kwa kuhakikisha mifumo na njia za kupitisha maji zinafanya kazi katika kiwango cha kutosha ili kuepusha maji kutuama na kusababisha mafuriko na uharibifu wa miundombinu pamoja na upotevu wa maisha na mali.
Akizungumzia mwelekeo wa mvua za msimu, Dk Kijazi alisema kutakuwa na mvua za wastani hadi juu ya wastani katika maeneo mengi yanayopata msimu moja wa mvua kwa mwaka, na kwamba mvua kubwa inatarajiwa Januari mwakani.
“Msimu huu ni mahususi katika maeneo ya magharibi mwa nchi, kanda ya kati, nyanda za juu Kusini Magharibi, kusini mwa nchi, maeneo ya kusini mwa mkoa wa Morogoro pamoja na Ukanda wa Pwani ya Kusini.
Mvua inatarajiwa kuanza wiki ya kwanza ya Novemba na kuisha wiki ya nne ya Aprili, 2018,” alieleza Dk Kijazi. Alisema Kanda ya Kati kwenye mikoa ya Singida na Dodoma, mvua zinatarajiwa kuanza kati ya wiki ya kwanza na ya pili ya Desemba mwaka huu, zinatarajiwa kuwa za wastani hadi juu ya wastani katika maeneo mengi.
Kwa Nyanda za Juu Kusini Magharibi na maeneo ya Kusini mwa nchi, mvua zinatarajiwa kuanza wiki ya nne ya Novemba na wiki ya kwanza ya Desemba. Alisema Pwani ya Kusini kwenye mikoa ya Lindi na Mtwara mvua zinatarajiwa kuanza kati ya wiki ya nne ya Novemba na wiki ya kwanza ya Desemba.
Dk Kijazi aliwataka watumiaji wa taarifa za hali ya hewa ambao ni wakulima, wafugaji, mamlaka za wanyama pori, mamlaka za maji na afya waendelee kutafuta, kupata na kufuata ushauri wa wataalamu katika sekta husika.

No comments: