MTU mmoja amekufa na nyumba mbili zimeezuliwa mapaa yake na kuanguka kutokana na mvua kubwa iliyonyesha ikiwa ni msimu wa mvua za vuli ambao umeanza mkoani Kigoma.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kigoma, Martin Otieno alisema hayo mjini Kigoma na kumtaja aliyekumbwa na mkasa huo ni Jumanne Masudi (54) ambaye ni mkazi wa Kijiji cha Nyarubanda, Tarafa ya Kalinzi Kigoma Vijijini na kwamba alikumbwa na mauti saa 10:30 jioni juzi akiwa nyumbani kwake.
Kamanda Otieno alisema wakati mvua ikinyesha, Masudi alikuwa nyumbani kwake na kwamba mvua hiyo iliyoambatana na upepo, iliezua paa la nyumba aliyokuwemo na kusababisha ukuta kuanguka, ambao ulimuangukia kichwani na kusababisha kifo chake.
Maafa hayo yamekuja siku moja baada ya juzi Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Dk Agnes Kijazi kuzungumzia mwelekeo wa mvua za msimu, akisema kutakuwa na mvua za wastani hadi juu ya wastani katika maeneo mengi yanayopata msimu moja wa mvua kwa mwaka, na kwamba mvua kubwa inatarajiwa Januari mwakani.
"Msimu huu ni mahsusi katika maeneo ya magharibi mwa nchi, Kanda ya kati, nyanda za juu Kusini Magharibi, Kusini mwa nchi, maeneo ya Kusini mwa mkoa wa Morogoro pamoja na Ukanda wa Pwani ya Kusini. Mvua inatarajiwa kuanza wiki ya kwanza ya Novemba na kuisha wiki ya nne ya Aprili, 2018,” alieleza Dk Kijazi.
Katika tukio lingine, Kamanda Otieno alisema dereva wa pikipiki ya abiria maarufu bodaboda, William Nashon (22) ameuawa kwa kuchomwa kisu shingoni na mtu asiyefahamika aliyekuwa abiria wake, aliyemtoa eneo la Ujenzi manispaa ya Kigoma Ujiji na kumpeleka eneo la Burega.
Otieno alisema Nashon alikufa akiwa anakaribia Hospitali ya Mkoa ya Kigoma ya Maweni, akifanya jitihada za kuokoa maisha yake na kwamba alianguka baada ya kupoteza damu nyingi kutokana na jeraha alilolipata na hivyo kufariki dunia. Hata hivyo, licha ya mauaji hayo muuaji hakuchukua kitu chochote kutoka kwa mtu huyo na polisi wanaendelea na uchunguzi kuhusu kadhia hiyo.
No comments:
Post a Comment