MSANII wa filamu nchini, Elizabeth Michael maarufu kama Lulu ameanza kujitetea katika Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam akieleza alichokuwa akifanyiwa na marehemu Steven Kanumba.
Akitoa utetezi wake katika kesi hiyo ya kuua bila kukusudia, Lulu amesema Kanumba alikuwa akilewa na kumpiga na kwamba Kanumba aliwahi alimpiga kwa panga mapajani na akapelekwa Hospitali ya Mwananyamala.
“Sijasababisha kifo cha Kanumba kwa namna yoyote ile. Umbo langu lilikuwa dogo hivyo mimi ndiyo nilikuwa nashambuliwa. Kama marehemu asingeanguka labda angenidhuru. Kanumba alikuwa kama mlezi wangu, tulianza mahusiano miezi minne kabla ya kifo chake,” amesema Lulu.
“Nilikuwa nataka kutoka ila marehemu (Kanumba) alinikataza, alikuwa hataki nitoke, nilipomwambia natoka na marafiki zangu alinikimbiza na taulo na mimi nilikuwa naogopa kupigwa, mara nyingi alikuwa ananipiga kila akilewa na sio kwa akili zake. Alipoona simu yangu inaita akahisi ni simu ya mwanaume akasema kwa nini naongea na simu ya mwanaume mbele yake? Marehemu akaingia uvunguni akatoa panga akasema leo nakuua huku akinipiga na panga kwenye mapaja”, ameelezea Lulu.
Lulu ameendelea kusimulia…. “Marehemu alianguka mwenyewe na kujigonga kwa nguvu na kuinuka akitapatapa, nilimwambia Seth kuwa Kanumba amedondoka na akajaribu kumuamsha hakuamka, akasema anaenda kumuita daktari, alivyosema anaenda kumuita daktari na mimi nikaondoka nikiogopa anaweza akaamka akaanza kunipiga. Niliondoka nikawasha gari kuelekea Coco Beach kutuliza akili”.
Muigizaji huyo ameendelea kusimulia kwamba … “Nilivyofika Coco Beach meseji zilianza kusambaa kuniuliza kuwa nasikia Kanumba amefariki, nikampigia Kidume ambaye ni rafiki yake Kanumba kumuuliza Kanumba yupo hospitali gani niende kumuona, akaniambia wewe usije hospitali, niambie uko wapi, tukakubaliana tuonane Bamaga. Tulivyokutana Bamaga alikuwa kama anataka kuongea na mimi ghafla wakaja askari kunikamata,” ameeleza Lulu.
Baada YA Muigizaji, Elizabeth Michael ‘Lulu’kuanza kujitetea katika Mahakama Kuu Kanda ya Dar, kwa tuhuma za kusababisha kifo cha Steven Kanumba bila kukusudia, msanii huyo amekana kuhusika na kifo hicho.
Lulu ameeleza siku ya tukio, Kanumba alikuwa amelewa na yeye Lulu alitaka kutoka na marafiki zake lakini alimkataza, baada ya Kanumba kuona simu ya Lulu imeita alizani anaongea na mwanamme mwingine huku ambapo alichukua panga na kumkimbiza nalo. Kanumba alianguka na Lulu kuchukua gari na kukimbilia Coco Beach ambapo baadaye alikamatwa na polisi maeneo ya Bamaga.
Jaji wa Mahakama Kuu, Samu Rumanyika amemtwanga maswali Lulu kama ifuatavyo;
Jaji Sam Rumanyika: Kipindi unaendesha gari ulikuwa na leseni halali?
Lulu: Ndiyo.
Jaji: Tufafanulie uhalali wake.
Lulu: Nilikuwa sina.
Lulu: Baada ya kukamatwa nilipelekwa kituo cha polisi Oysterbay nilikuwa nikihojiwa nikiwa sijui kama Kanumba amefariki.
Lulu ameeleza hayo leo Jumatatu akijitetea katika kesi ya kuua bila kukusudia inayomkabili.