tgnp mtandao yafungua rasmi mafunzo ya sikutatu kwa wanawake wanaofanya biashara mipakani


TGNP Mtandao kwa kushirikiana na Taasisi ya Mafunzo ya Jinsia GTI na AWDF wameandaa mafunzo ya siku tatu kwa wafanya biashara wanawake wa mipakani lengo likiwa ni kuwajengea uwezo wanawake hawa wa kuingiza maswala ya jinsia katika biashara zao.
Mafunzo hayo yamewaleta pamoja zaidi ya washiriki 35 wakiwemo Maafisa wa serikali kutoka mipaka tofauti tofauti, Asasi za kiraia ili kuwajengea uwezo wa kuzifahamu haki zao na kukabiliana na changamoto mbalimbali wanazokutana nazo wafanya biashara wanawake wa mipakani katika biashara zao.

Akiongea na waandishi wa habari mapema leo Mkurugenzi Mtendaji wa TGNP Mtadao Bi. Lilian Liundi alisema kuwa wameamua kuwapa wafanyabiashara wa mipakani elimu hiyo ili waweze kufahamu kanuni mbalimbali za Afrika Mashariki na namna ya kuboresha huduma zao ili kuweza kuyafikia masoko kwa urahisi kuanzia ngazi ya kikanda na kufikia kimataifa.

Aliongezea kwa kusema kuwa utafiti uliofanywa na Kituo cha Sera za Biashara Afrika unaonyesha kuwa biashara  imatoa ajira kwa zaidi ya asilimia 60 ya wanawake, na katika biashara zifanyikazo katika nchi za jangwa la Sahara, ambapo asilimia kati ya 70 na 80 ya wanawake wamejikita zaidi katika biashara isiyo rasmi na utafiti wa UN Woman unaonyesha zaidi ya asilimia 74 ya wafanyabiashara za mipakani katika nchi za maziwa makuu ni wanawake.

Mkurugenzi huyo aliendelea kwa kusema kuwa wanawake wanaofanya biashara mipakani wanakumbana na changamoto nyingi ikiwemo usawa katika mgawanyo wa kipato na maamuzi juu ya rasilimali katika kufikia zana za uzalishaji kama vile mitaji, ardhi na teknolojia sahihi na taarifa pamoja na elimu ya mafunzo, vilevile ukatili wa kijinsia ikiwemo rushwa ya ngono na nyingine nyingi.
Lakini pia pamoja na nchi zetu kuridhia mikataba mbalimbali ya kitaifa, kimataifa na ya kikanda ya kuendeleza usawa wa kijinsia na uwezeshaji wanawake kama mkataba wa Umoja wa kimataifa wa mwaka 1979, mpango mkakati wa Beijing wa mwaka 1995, Itifaki ya Maputo ya mwaka 1997 na mkataba wa jinsia na maendeleo wa ukanda wa SADC 1998.

Aidha bi. Lilian liundi alisema licha ya juhudi hizo zote lakini bado hakuna muungano kati ya biashara na sera za jinsia kwani mikataba muhimu ya biashara bado inaupofu mkubwa wa kijinsia, kwa kiasi cha kushindwa kuzingatia mahitaji muhimu ya wanawake, lakini pia utekelezaji hafifu wa mikataba na kutokuwepo kwa taarifa mbalimbali za fursa za biashara hii imewaongezea vikwazo wanawake wanaofanya biashara isiyo rasmi katika mipaka na kwa wajasiliamali wadogo kwa ujumla kuweza kukuza biashara zao.

Lakini pia serikali za nchi za afrika mashariki zilitakiwa kukaa chini na kuunda sera na mipango itakayowasaidia wafanyabiashara hawa wadogo wa mipakani kwa kuwaondolea kodi kandamizi ili na wao waje kuwa wafanyabiashara wakubwa kwa kuwawekea mikakati madubuti, kwani wafanya biashara hawa wakiwezeshwa wanaweza kuwa wakubwa na kuchangia vizuri pato la taifa.
Na mwisho alimalizia kwa kusema kuwa changamoto hizi zinahitaji sera kufanyiwa maboresho ili kuunga mkono juhudi za wanawake na kuwapa ujasiri wanawake wa kuimarisha  biashara zao, lakini pia maboresho hayo yanatakiwa kulenga kuongeza ushiriki wa wanawake katika biashara za mipakani kwa kuboresha na kurahisisha mchakato wa kufanya biashara mipakani.

Inatambulika kuwa wanawake hurudisha asilimia kubwa ya pato lao kwa familia na jamii zao, hivyo juhudi za makusudi zinahitajika katika kuwainua kiuchumi wanawake hawa na kwa nchi kama za afrika mashariki zinahitajika kuhakikisha kuwa wanawake wanapata haki na fursa sawa kama wanaume ili kupunguza pengo la kijinsia, wanawake wanatakiwa kutoa michango yao katika maendeleo ya jamii zao.

No comments: