MKURUGENZI KUCHUNGUZWA UKEREWE



Baraza la Madiwani la Halmashauri la Mji wa Ukerewe hawana imani na utendaji kazi wa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri Mji huo Frank Bahati.

Akizungumza na KWANGULEO Blog baada kuvurugika kwa Kikao cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri, Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo George Nyamaha alisema Mkurugenzi anapaswa kuchunguzwa.

"Siku tatu kabla ya kikao tulishuhudia stakabadhi feki walizopewa wafanyabiashara zikiwa na zina mhuri wa halmashauri, baada ya kuhoji kuhusu hizo stakabadhi Mkurugenzi akawa hataki tuhoji na kujadili suala hilo, jambo lililopelekea madiwani kuanza mvutano na mkurugenzi katika kikao na kutoka nje," alisema Nyamaha.

Nyamaha alisema kwa muda mrefu wamekuwa na shaka naye juu ya utendaji kazi wake, ambapo walimfikishia taarifa Mkuu wa Mkoa na Mkuu wa Wilaya na walikuwa wanasubiri majibu.

Aidha ameiomba Serikali kupitia  Mamlaka husika kufuatilia suala hilo kwa haraka kwani wafanyabiashara wamekuwa wakiilalamikia halmashauri wanavyonyanyaswa na watozaji ushuru pamoja na wanaopiga doria ya utokomezaji uvuvi haramu.

No comments: