Majaliwa alisema Dar es Salaam jana wakati akifungua kongamano la Kitaifa la Maadhimisho ya Siku ya Ukimwi Duniani 2017, kaulimbiu ikiwa ‘Changia Mfuko wa Udhamini wa Udhibiti Ukimwi, Okoa Maisha.”
Alisema wito wake ni kuhakikisha bodi ya mfuko huo, inasimamia vizuri fedha hizo zinazochangiwa na wadau mbalimbali ili kuwahakikishia usalama wake. “Fedha hizi zikitumika vinginevyo hatutavumiliana. Malengo ni kuhakikisha fedha hizo zinazotolewa na wadau zinatumika kama ambavyo imekusudiwa,” alisema Majaliwa.
Alisema anayo furaha kuwa Mfuko huo wa Udhibiti Ukimwi umeanza kufanya kazi, ambapo Oktoba 21, mwaka huu kwa mara ya kwanza Mfuko huo uligawa fedha kwa ajili ya shughuli za kudhibiti ukimwi nchini Sh. milioni 660, zilitolewa kwa Wizara ya Afya kwa ajili ya kununua dawa za Cotrimoxazole ambazo hutumika kutibu na kuzuia magonjwa nyemelezi kwa watu waishio na virusi vya Ukimwi.
“Aidha kiasi cha Shilingi milioni 200 zilitolewa kwa Mkoa wa Manyara kwa ajili ya kuchangia ujenzi wa Kituo cha Afya Mererani, ambacho licha ya kutoa huduma nyingine za afya, kitatumika kutoa huduma za dawa za kufubaza VVU kwa watu waishio na virusi vya Ukimwi,” alisema.
Alisema serikali itaendelea kutenga fedha za mfuko huo na kuhakikisha inahamasisha wananchi na wadau, ikiwemo sekta binafsi kuchangia mfuko huo muhimu. Alisema Serikali ya Awamu ya Tano imedhamiria kujenga Tanzania ya viwanda na ili ifikie lengo hilo ni lazima wananchi wawe na afya bora.
“Nguvu kazi kwa ajili Tanzania ya viwanda itatokana na wananchi wenye nguvu na afya bora. Hivyo serikali tutahakikisha tunaendelea kutoa huduma bora za afya ili wananchi wetu waweze kuwa na afya bora,” alisema.
Alisema watu milioni 16 ya Watanzania wote ni vijana na wanapaswa kukingwa dhidi ya magonjwa mbalimbali ikiwemo Ukimwi ili taifa liwe na nguvu kazi ya kutosha hasa kipindi hiki linapoanza mageuzi makubwa ya kiuchumi na kimaendeleo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Tume ya Kudhibiti Ukimwi Tanzania (Tacaids), Dk Leonard Maboko alisema kongamano hilo ni sehemu ya shughuli za Maadhimisho ya Siku ya Ukimwi duniani, itakayofanyika Desemba mosi hapa nchini.
Alisema maonesho ya maandalizi hayo yalianza Jumamosi, yakijumuisha huduma mbalimbali za utoaji elimu na burudani kwa wananchi ikiwemo ushauri nasaha na upimaji wa hiari wa VVU.
Alisema pia kuwa tayari wamezindua mkakati wa kitaifa wa kondomu wa miaka mitatu wa 2016 hadi 2018, na siku ya kilele cha maadhimisho hayo kutakuwa na uzinduzi wa Ripoti ya Utafiti wa Kitaifa wa Matokeo ya Ukimwi wa Mwaka 2016/17.
No comments:
Post a Comment