TUNDAMAN:NILIKUWA KIMYA KWA SABABU...............



Msanii wa muziki wa kizazi kipya Tunda Man, amesema sababu iliyomfanya awe kimya baada ya kuoa ni kutafuta heshima ya ndoa, ambayo alihisi asingeipata kwa mapema angedhalilika.

Akizungumza na eNewz ya East Africa Television, Tunda Man amesema kwamba kitendo cha kutokuwa na mtoto baada ya kuoa kilikuwa kinamnyima raha, hivyo aliamua aache vingine vyote ili kutafuta heshima ya ndoa, lakini sasa anarudi kwenye game rasmi kwani ameshapata alichokuwa akikitafuta.

“Kitu kikubwa ni kwamba sasa niko huru, mwanzo ilikuwa heshima ya ndoa lazima mtoto, kitu kama hiko kilikuwa kinanitia stress kinoma yani, kwa hiyo nimeoa kama miaka miwili iliyopita, na nilikuwa nimekaa kimya ka muda mrefu kutafuta heshima ya ndoa, mnielewe wananchi, nafikiri heshima imekuja tayari, nina mtoto anaitwa Itsal, kwa hiyo kitu kikubwa sasa hvi nadeal na ngoma zangu”, amesema Tunda Man.

Msanii huyo amesema wiki ijayo anatarajia kuachia kazi mpya tatu kwa pamoja, ikiwemo ambayo ametunga baada ya kushuhudia machungu aliyopitia mke wake wakati wa ujauzito.

HOJA 15 ZA MWAKYEMBE



KAMBI Rasmi ya Upinzani Bungeni imesema imejipanga kumbana kwa hoja 15 Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe, atakapowasilisha bungeni mjini Dodoma leo hotuba ya makadirio ya wizara yake kwa mwaka ujao wa fedha.

Mambo hayo ni pamoja na kutotungwa kwa kanuni za sheria mpya ya habari iliyotungwa mwaka 2016, kupotea kitatanishi kwa waandishi wa habari, kusajili magazeti kila mwaka, waandishi wa habari kulipia vitambulisho vya kitaifa kila mwaka na ufujaji wa mapato ya mechi za soka zinazochezwa nchini.

Zingine ni serikali kutotenga bajeti kusaidia maendeleo ya michezo, madai ya wasanii kutengenezewa matabaka na wenye ving'amuzi kutoza huduma hadi kwa vituo vya televisheni (TV) visivyopaswa kulipiwa.

Pia wasanii kuimba nyimbo zisizo na maadili na kuvaa mavazi yasiyoendana na utamaduni wa Kitanzania, kuvamiwa kwa viwanja vya michezo nchini na changamoto katika upatikanaji wa washindi wa shindano la Miss Tanzania.

Kwa mujibu wa ratiba ya vikao vya Bunge la Bajeti iliyotolewa na Idara ya Habari na Elimu ya Bunge leo, Bunge litajadili kwa siku moja hotuba ya makadirio ya wizara hiyo kwa mwaka ujao wa fedha.

Akizungumza na Nipashe mjini hapa jana, Naibu Waziri Kivuli wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Devotha Minja, alisema wamepanga kuutumia mjadala huo kuibana serikali ili izitatue changamoto hizo.

Alisema hoja ya kwanza ni kile alichokiita kuvifunga midomo kwa vyombo vya habari vinavyomilikiwa na watu binafsi kwa kuvifungia na kuvitoza faini pale zinapochapisha au kutangaza habari kukosoa mwenendo wa utendaji wa serikali.

Alisema hali hiyo inarudisha nyuma maendeleo ya tasnia ya habari na kuminya uhuru wa kujieleza na haki ya kupata habari.

Minja ambaye pia ni Mbunge wa Viti Maalum (Chadema), alisema hoja yao ya pili ambayo Dk. Mwakyembe watamtaka awape majibu bungeni leo ni kutotungwa kwa Kanuni za Sheria mpya ya Habari nchini.

Alisema licha ya Bunge kuipitisha muswada wa sheria hiyo na kutiwa saini na Rais takriban miaka miwili sasa, kanuni hazijatungwa ili ianze kutumika.

"Kwa sheria ile ambayo tuliipitisha, bado hazitengenezwa zile kanuni za kuunda mabaraza ya kushughulikia kesi za mwandishi mmoja mmoja," alisema Minja.

"Na hapa tunaona kuna ucheleweshaji wa makusudi ili sheria ya zamani iendelee kutumika kwa sababu inampa mamlaka waziri kufungia magazeti. Sheria ya sasa haina kitu kama hicho, inataka mwandishi aliyekosea ndiyo awajibike na si kufungia gazeti zima."

Minja ambaye kitaaluma ni mwandishi wa habari, pia alisema upinzani umejipanga kuutumia mjadala wa leo kumbana Dk. Mwakyembe ili wizara yake iachane na utaratibu wa waandishi wa habari kulipia kila mwaka Sh. 30,000 kupata vitambulisho vya kitaifa (press cards) badala yake wawe wanalipa kila baada ya miaka kuanzia mitatu hadi 10 kama ilivyo kwa leseni ya udereva na hati ya kusafiria.

Minja alisema malipo ya aina hiyo yako pia katika usajili wa magazeti, akieleza kuwa kuna utaratibu mpya umeanzishwa na wizara hiyo wa kusajili gazeti kila mwaka ambao hawauungi mkono.

Alisema utaratibu huo aliodai upo katika nchi mbili tu katika Jumuiya ya Afrika Mashariki wanaona si rafiki kwa uhai wa tasnia ya habari kwa kuwa umelenga kuyazima usajili magazeti yanayoandika habari zisizoifurahisha serikali.

Pia alisema watautumia mjadala wa leo kumbana Dk. Mwakyembe na serikali kwa ujumla kuhusu kile alichodai wasanii nchini wamegawanyika.

"Kuna wasanii wanapata upendeleo mkubwa wa serikali, na hili sasa limetengeneza matabaka kwa wasanii wetu. Yaani sasa tumefikia hatua wasanii wanakuwa wa chama fulani ilhali wanapaswa kuwa pamoja na kufanya kazi kwa kushirikiana," Devotha alisema.

Naibu waziri kivuli huyo pia alisema bado kuna changamoto ya ufujaji wa mapato ya milangoni kwenye mechi za soka nchini, akidai kuna Sh. milioni mbili zinadaiwa zinalipwa kwa wanaojiita wawezeshaji wa uwanja kwa kila mechi inayochezwa Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Sambamba na hayo, alisema watahoji bungeni sababu za uongozi wa Shirikisho la Soka (TFF) kuteua mtu mwenye tuhuma za rushwa kushika nafasi ya mtu aliyeondolewa madarakani kwa tuhuma zenye mwelekeo huo.

Aliongeza kuwa upinzani umejipanga kuibana serikali leo ichukue hatua stahiki dhidi ya watoa huduma za ving'amuzi ambao wamekuwa wakikata huduma hadi kwenye Tv zisizoruhusiwa kulipiwa nchini.

Wakati Minja akieleza hayo, Mbunge wa Wawi, Ahmed Juma Ngwali (CUF), alisema upinzani pia umejipanga kumbana Waziri Mwakyembe ili wizara yake iwe inatenga bajeti ya kusaidia maendeleo ya sekta ya michezo nchini.

Ngwali alidai kuwa kwa takribani miaka mitatu sasa, TFF haijawahi kupokea kiasi chochote cha fedha kutoka serikalini kusaidia maendeleo ya mpira wa miguu nchini.

Naye Mbunge wa Kaliua, Magdalena Sakaya (CUF), aliiambia Nipashe mjini hapa jana kuwa kama atapata nafasi ya kuchangia mjadala huo leo, ataitaka serikali kudhibiti maudhui ya nyimbo za wasanii na uvaaji wao.

"Nyimbo za wasanii wetu zinapaswa kuzingatia maadili. Mavazi yao pia ni lazima yazingatie utamaduni wetu ili kutunza heshima ya nchi," Sakaya alisema huku akisisitiza Baraza la Sanaa (Basata) linapaswa kuwajibishwa kwa kile alichodai limeshindwa kudhibiti wizi wa kazi za wasanii.

Mbunge huyo pia alisema atautumia mjadala wa leo kumshauri Dk. Mwakyembe na wizara yake kudhibiti udanganyifu katika upatikanaji wa washindi wa Miss Tanzania, akidai kuwa katika miaka ya karibuni shindano hilo limetawaliwa na udanganyifu.

"Miaka ya nyuma, nilifuatilia miaka mitatu ya mwanzo, mshindi ulikuwa unamwona kuanzia hatua ya mwisho kuwa huyu atashinda na kweli inakuwa hivyo. Lakini miaka ya karibuni kumekuwa na udanganyifu mkubwa ambao unaashiria ama rushwa au kujuana," alisema.

"Baadhi ya ma-Miss wenyewe wanaishi maisha ya ajabu ya kubadilisha wanaume. Hivi kweli hii ndiyo maana ya shindano hili? Kulikoni kuendelea kuiabisha nchi, ni heri lifutwe tu."

Sakaya pia alisema atautumia mjadala wa leo kuibana serikali ivirejeshe viwanja vya michezo na maeneo ya wazi yaliyovamiwa na kuendelezwa kwa kuwa uvamizi huo unakwamisha maendeleo yua watoto kimichezo.

"Ni aibu viwanja vya michezo vimevamiwa kujengwa majumba na serikali ipo inaangalia tu," alisema Sakaya na kuongeza:

"Ni lazima kama serikali inayojali maendeleo ya watoto na michezo tuvirejeshe viwanja na maeneo ya wazi yaliyovamiwa. Kama kuna mtu kajenga nyumba kwenye eneo la wazi tubomoe ili watoto wapate mahali pa kucheza.

"Lazima kama taifa tuwekeze katika michezo kwa sababu michezo ni ajira, ni afya na burudani. Rais mstaafu (Jakaya) Kikwete alikuwa analipa hadi mishahara ya makocha lakini sasa serikali inaonekana imejiweka kando kuendeleza michezo. Shuleni hakuna vifaa vya michezo.

"Tunategemea nini huko mbele kama hatuwekezi kwa watoto kwa sasa? Kina (Cristiano) Ronaldo hawakutengenezwa ukubwani, tuwekeze kwa watoto."

HAWA HAPA WATEJA WATAKAOHUDUMIWA NA NSSF



SHIRIKA la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF), limetaja aina ya wanachama litakaohudumia baada ya Sheria ya Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kusainiwa na Rais John Magufuli hivi karibuni.

Meneja Kiongozi wa NSSF Mkoa wa Temeke, James Oigo, aliyasema hayo jana wakati akizungumza na waajiri kuhusu sheria hiyo mpya na wajibu wao katika kulinda haki za wanachama.

Watu watakaokuwa wanachama wa NSSF, alisema, ni waajiriwa wote wa sekta binafsi, wageni ambao wameajiriwa Tanzania Bara, waajiriwa katika taasisi za kimataifa zinazofanya kazi Tanzania Bara na watu wote waliojiajiri wenyewe na wale wa sekta isiyo rasmi.

Kwa mujibu wa Sheria ya Mfuko wa Hifadhi ya Jamii ya mwaka jana, mifuko ya sekta hiyo imeunganishwa na kubaki miwili - NSSF na Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF).

Mifuko iliyounganishwa kwa sheria mpya ni PPF, GEPF, LAPF na PSPF.

Oigo alisema NSSF inawatembelea wanachama wake nchi nzima kuwaelimisha juu ya sheria hiyo, ili kuondoa hofu iliyopo miongoni mwao baada ya mifuko kuunganishwa na kubaki miwili.

Katika ziara hizo, alisema, NSSF itahimiza waajiri kuwasilisha michango ya wafanyakazi kwa wakati ili kuliwezesha shirika kulipa mafao ya wanachama kwa ufanisi, kuzijua changamoto zinazowakumba waajiri.

"Waajiriwa wote ambao wataajiriwa baada ya sheria hii kuanza ndio watakuwa katika mfuko ama wa PSSSF endapo wanaajiriwa katika sekta ya umma na NSSF endapo wanaajiriwa katika sekta binafsi," alifafanua.

Aidha, alisema waliokwishaajiriwa wakati sheria hiyo inaanza ambao walikuwa katika mifuko iliyounganishwa watakuwa wanachama wa mfuko wa PSSSF bila kujali wapo setka binafsi au ya umma.

Aidha, watumishi ambao walikuwa wanachama wa NSSF watabakia kuwa wanachama wa NSSF bila kujali sekta wanayotoka, alisema Oigo.

Alizidi kufafanua kuwa kanuni ya ulipaji mafao na idadi ya mafao yatakuwa ya aina moja kwa mifuko yote miwili.

Akifungua mkutano huo, Kaimu Mkurugenzi wa Uendeshaji wa NSSF, Bathow Mmuni, alisema sheria mpya ya hifadhi ya jamii imeshasainiwa na Rais na sasa zimebakia taratibu za kiuendeshaji.

Naye Meneja wa NSSF Kinondoni, Marco Magheke, alisema shirika limejipanga kuendelea kutoa huduma bora zaidi kwa wanachama wake.

DUA ZA MZEE AKILIMALI JUU YA SIMBA



Katibu wa Baraza la Wazee wa klabu ya Yanga, Ibrahimu Akilimali amesema kuwa kuelekea mchezo wao dhidi ya watani zao Simba SC kunahaja ya kutupilia mbali tofauti zao na kumuomba Mungu katika kuhakikisha wanachomoza na ushindi siku hiyo ya Aprili 29.

Wakati zimesalia siku mbili pekee kabla ya kukutana kwa watani hao wajadi Simba SC dhidi ya Yanga SC kwenye dimba la Taifa siku ya Jumapili hii, Mzee Akilimali ametumia muda wake kuiyombea timu yake kuhakikisha inachomoza na ushindi siku hiyo.

Tunalengo la kuwashinda wapinzani wetu, siyo rahisi lakini lazima ujiandae kwa hayo wazee tunatoa baraka zote kwa vijana kwakuwa hatuna kinyongo.

Isipokuwa mimi naomba tu Yaarabbi Yaarabbi nakuomba turudishie hali yetu ileile ya umoja na mshikamano wetu kwa kila hali, tushikamane kwaajili ya kuwasapato vijana wetu na tumuombe Mwenyezi Mungu kila mmoja kwa dua yake na imani yake ili tupate ushindi siku hiyo ya Jumapili.

Nawaomba wana Yanga wenzangu tuwe wamoja tuwache tofauti zetu twende katika mchezo maana ni mgumu sana.

Kocha mpya ameingia na viongozi wetu wamefanya mambo haraka haraka sasa hivi yupo kazini, Msimbazi ubingwa bado isipokuwa tu mtu hawezi kukata tamaa ila hali bado. Amenitambuka mechi chache tu na yeye atarajie kufanya vibaya kwenye mechi hizo alizo nazo.

Wazee hatuna ahadi yoyote kwa vijana kwakuwa hayo yanatamkwa na viongozi.

Simba ambayo inaongoza kwenye msimamo wa ligi kwakuwa na jumla ya pointi 59 nyuma ya hasimu wake Yanga wenye alama 48 zinatarajia kukutana siku ya Jumapili ya Aprili 29 kwenye dimba la Taifa Jijini Dar es salaam.

MKURUGENZI KUCHUNGUZWA UKEREWE



Baraza la Madiwani la Halmashauri la Mji wa Ukerewe hawana imani na utendaji kazi wa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri Mji huo Frank Bahati.

Akizungumza na KWANGULEO Blog baada kuvurugika kwa Kikao cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri, Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo George Nyamaha alisema Mkurugenzi anapaswa kuchunguzwa.

"Siku tatu kabla ya kikao tulishuhudia stakabadhi feki walizopewa wafanyabiashara zikiwa na zina mhuri wa halmashauri, baada ya kuhoji kuhusu hizo stakabadhi Mkurugenzi akawa hataki tuhoji na kujadili suala hilo, jambo lililopelekea madiwani kuanza mvutano na mkurugenzi katika kikao na kutoka nje," alisema Nyamaha.

Nyamaha alisema kwa muda mrefu wamekuwa na shaka naye juu ya utendaji kazi wake, ambapo walimfikishia taarifa Mkuu wa Mkoa na Mkuu wa Wilaya na walikuwa wanasubiri majibu.

Aidha ameiomba Serikali kupitia  Mamlaka husika kufuatilia suala hilo kwa haraka kwani wafanyabiashara wamekuwa wakiilalamikia halmashauri wanavyonyanyaswa na watozaji ushuru pamoja na wanaopiga doria ya utokomezaji uvuvi haramu.