WAKWEPA KODI KIAMA KINAKUJA




RAIS John Magufuli amesema Tanzania ilikuwa inapoteza mapato mengi kutokana na udhaifu wa Sheria za Kodi na usimamizi wake, hivyo ili kuziba mianya hiyo, amemteua mtaalamu aliyebobea katika sheria za kodi kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa Florens Luoga kuwa gavana mpya wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT).
Profesa Luoga ambaye pia ni Naibu Makamu Mkuu wa Chuo wa UDSM anayeshughulikia Taaluma, atamrithi Profesa Benno Ndullu anayetarajiwa kustaafu rasmi utumishi wa umma ndani ya miezi mitatu kuanzia sasa.
Aliyasema hayo Ikulu, Dar es Salaam jana wakati akiwapongeza Wajumbe wa Kamati mbili zilizohusika katika kujadiliana na Kampuni ya uchimbaji dhahabu ya Barrick kuhusu mkataba mpya wa uchimbaji unaozingatia maslahi sawa ya faida.
Alisema nchi imekuwa ikipoteza fedha nyingi kutokana na wawekezaji kukwepa kodi kwa kuweka fedha zao katika nchi zisizotoza kodi kutokana na sheria ya mwaka 1992 kuhusu uwekaji fedha nchini kutosimamiwa vyema na BoT kutokazia sheria za kodi. Katika kuonesha msisitizo kuwa sasa anataka sheria za kodi zifuatwe, alitangaza kumteua Profesa Luoga ili akasimamie sheria za kodi kwa ukamilifu.
Alisema watu wengi huenda wakashangaa kwa nini amemteua mwanasheria kuwa gavana kinyume na ilivyozoeleka na wengi kuwa mchumi ndiye huwa gavana, lakini amefanya hivyo kwa sababu tatizo la BoT limekuwa kutosimamia sheria za kodi.
Rais alisema Profesa Luoga atasaidiwa na manaibu magavana wenye taaluma ya uchumi na fani nyingine, hivyo anaamini atamudu nafasi hiyo itakayoachwa wazi na Profesa Ndulu ambaye amemsifu kuwa amefanya kazi nzuri na atastaafu Januari.
Ndullu ambaye amekuwa Gavana wa BoT tangu mwaka 2008 anatarajiwa kumaliza muda wake wa kuiongoza taasisi hiyo Januari mwakani. Rais Magufuli akizungumza baada ya kutoa vyeti hivyo alisema atamteua gavana kutoka baadhi ya wajumbe wa kamati ya mashauriano kuhusu madini kutokana na kuridhishwa na kazi yao.
Huo ni uteuzi wa pili kwa Profesa Luoga, kwani Julai 11 mwaka huu Rais Magufuli alimteua kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Mamlaka ya Mapato ya Tanzania (TRA).
Profesa Luoga ambaye pia ni Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) anayeshughulikia Taaluma, alichukua nafasi ya Bernard Mchomvu ambaye bodi yake ilivunjwa na uteuzi wake kutenguliwa na Rais Magufuli.
Kuteuliwa kwa Profesa Luoga kutamfanya kuwa Gavana wa saba wa BoT tangu ilipoanza kazi Juni 14, mwaka 1966, ikiwa ni mwaka mmoja baada ya kuundwa kwa Sheria ya Benki ya Tanzania mwaka 1965.
Gavana wa kwanza alikuwa Edwin Mtei aliyeiongoza BoT hadi mwaka 1974 na nafasi yake kuchukuliwa na Charles Nyirabu aliyeongoza hadi mwaka 1989. Kuanzia mwaka 1989-1993, BoT iliongozwa na Gilman Rutihinda aliyemwachia Dk Idris Rashidi aliyedumu hadi mwaka 1998. Kuanzia mwaka huo, iliongozwa na Dk Daudi Ballali.
Na kuanzia Januari 8, mwaka 2008 BoT ilikuwa chini ya Profesa Ndulu. MAJUKUMU BOT Ikiwa ni benki ya kitaifa inayosimamia masuala ya kibenki na kifedha nchini Tanzania, miongoni mwa majukumu yake ni utoaji wa fedha za Tanzania, Shilingi ya Tanzania.
Imepewa pia majukumu mbalimbali yanayohusiana na usimamizi wa fedha nchini, yakiwemo; kuhakikisha uwepo wa akiba ya fedha za kigeni kwa lengo la kusaidia kuimarisha uchumi, na akiba hiyo kutumika wakati wa mkwamo wa kiuchumi nchini.
Aidha, ina jukumu la kchochea ukuaji wa soko la fedha nchini, kulinda na kuendeleza taasisi za kifedha zinazosimamiwa vema, lakini pia jukumu jingine ni kuhakikisha uwiano imara kati ya fedha ya Tanzania na pesa za kigeni.
ASISITIZA KODI, AKERWA
Aidha, Rais Magufuli alisema Serikali yake inawapenda wafanyabiashara na akawataka wafanyabiashara wazawa kuchangamkia fursa mbalimbali za kiuchumi zilizopo nchini hivi sasa, lakini akawataka walipe kodi ili nchi ipate fedha za kuendesha miradi yake mbalimbali.
Alisema nchi hivi sasa inakusanya mapato mengi inayoyatumia kutekeleza miradi yake kinyume na upotoshaji mkubwa unaofanywa na baadhi ya watu, wasomi na wanasiasa ambao wanaobeza kazi zinazofanywa na Serikali wakidai takwimu za uchumi ambazo Serikali inadai makusanyo yake yanapanda, ni za kupikwa na haziakisi uhalisia.
“Utakuta mtu anasema makusanyo yameshuka, hivi kama makusanyo yangeshuka tungeweza kujenga reli ya kisasa kwa gharama ya Shilingi trilioni 7 kutoka Dar es Salaam hadi Dodoma yenye urefu wa Kilomita 726?
Serikali ambayo haina mapato inaweza kununua ndege sita mpya kwa mpigo?” “Kama hatukusanyi mapato tungetangaza zabuni ya mradi wa kuzalisha umeme wa Stiegler’s Gorge ambao utazalisha Megawati 2,100? au kuongeza bajeti ya afya kutoka Shilingi bilioni 31 hadi Shilingi bilioni 269?
Kama huna pesa utatangazaje zabuni ya ununuzi wa meli mpya Ziwa Victoria au kusambaza umeme kwenye vijiji 4,000?,” alihoji Rais Magufuli. Alielezea kusikitishwa na taarifa iliyochapishwa na Gazeti la Tanzania Daima la juzi kuwa asilimia 67 ya Watanzania wanatumia dawa za kupunguza makali ya virusi vya Ukimwi (ARV’s).
Alisema upotoshaji wa aina hiyo una madhara makubwa kwa taifa kwa kuwa wawekezaji hawawezi kuja kuwekeza kwenye taifa la watu wagonjwa. Alisema lengo la watu wanaopotosha taarifa za serikali ni kutaka kuwatoa wananchi kutoka kwenye mjadala wa maendeleo ya nchi ili waanze kujadili matatizo ya watu hao.
Hivyo ameagiza Sheria ya Takwimu ya Mwaka 2015 ianze kutumika dhidi ya watu wanaopotosha takwimu za serikali. ATUNUKU VYETI Kwa kuthamini uzalendo, mchango na kazi ngumu iliyofanywa na kamati alizoziunda za kuchunguza biashara ya madini nchini, Rais Magufuli aliwatunuku vyeti vya shukrani na pongezi wajumbe 28 wa kamati hizo.
Alisema wajumbe hao walijitolea maisha yao kwa kufanya kazi hatari ya kumnyang’anya mtu mabilioni. Alisema wakati wanaanza kufuatilia suala la madini, walijua ni aina gani ya watu wanaoshughulika nao.
“Mimi mwenyewe nilipata mtikisiko, lakini nikasema niko kwa ajili ya Watanzania na ninachokifanya ni kwa faida yao. Walipogundua tuna taarifa zao zote za mawasiliano waliyokuwa wakiyafanya, akaunti zao za nje na kila kibaya walichofanya, waliamua kuja haraka kwenye mazungumzo, tulikuwa na ushahidi wote, walikuja kwanza nane, baadaye wakaongezeka wakafika 14 na baadaye 30, hii inaonesha dozi tulizokuwa tukiwapa ziliwatosha,” alieleza Rais Magufuli.
Alisema vyeti alivyowatunuku ni kumbukumbu ya maisha yao kwa kuwa wamewawakilisha Watanzania vizuri na wameonesha uzalendo wa kweli kwa taifa. Alitaka dhana ya uzalendo kwa nchi iendelee kuimarishwa kwa kuwa wajumbe wa kamati hizo wameonesha wao ni Watanzania wa kweli.
VIONGOZI WA DINI, WANASIASA
Akizungumza kwa niaba ya viongozi wa dini, Mufti Mkuu wa Tanzania Shehe Abubakar Zuberi, alimtaka Rais Magufuli asiogope lawama, aendelee kuwatumikia Watanzania. Alisema hata Mungu analaumiwa, mitume walilaumiwa, watu wema wanalaumiwa, hivyo Rais asikate tamaa, athamini anachokifanya kwa ajili ya taifa kwa kuwa yeye ni lulu kwa Watanzania.
Mwenyekiti wa Taifa wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba aliyeongea kwa niaba ya viongozi wa vyama vya siasa alitoa rai kuwa Watanzania watakaoingia kwenye bodi ya pamoja itakayoundwa wajali uzalendo na maslahi ya taifa na wasikubali kudanganywa.
Lipumba ambaye kitaaluma ni mchumi, alisema kwenye mambo yanayohusu maslahi ya taifa, Watanzania lazima wawe wamoja na kuweka kando tofauti za vyama. Alisema wanamshukuru Rais kwa hatua anazochukua za kunusuru rasilimali za taifa kwa kuwa wapinzani walikuwa wakilipigia kelele jambo hilo kwa muda mrefu.
MAJADILIANO YA TANZANITE, ALMASI
Ili kuhakikisha taifa linanufaika na rasilimali za madini, Rais Magufuli alimwagiza Waziri wa Sheria na Katiba, Profesa Palamagamba Kabudi na kamati yake ya majadiliano kuanza mara moja mazungumzo na Kampuni ya Tanzanite One inayochimba madini ya Tanzanite pamoja na kampuni inayochimba almasi.
Naye Waziri Kabudi alimhakikishia Rais Magufuli kuwa atalifanyia kazi agizo hilo mara moja na amenukuu msemo wa watu wa kabila la Waha usemao; “Mchuzi wa mbwa mwitu hunywewa ungali wa moto,” akimaanisha kuwa hatachelewa kulifanyia kazi agizo hilo la Rais.
Waziri wa Madini, Angellah Kairuki alisema Wizara hiyo itadhibiti utoroshwaji wa madini, lakini pia itasimamia utekelezaji wa makubaliano yote yaliyofikiwa ili kuleta tija kwenye sekta ya madini.
Kairuki alisema sekta ya madini inachangia asilimia 4.2 tu kwenye Pato la Taifa kiasi ambacho alisema ni kidogo. Alisema Wizara hiyo itahakikisha madini yanaongezewa thamani kabla ya kuuzwa nje ya nchi, lakini pia wataendelea kushirikiana na wajumbe wa kamati za Rais.
AKAUNTI ZA NJE
Rais Magufuli pia alisema Sheria ya Fedha ya mwaka 1992 inayozuia uwekaji wa fedha nje imekuwa haitumiki, hivyo kusababisha kampuni kufungua akaunti kwenye nchi ambako hawalipi kodi.
Rais alisema pamoja na kuwepo kwa sheria hiyo, BoT ilishindwa kuzuia mambo hayo yasitendeke. Wafanyabiashara wa ndani Ili kuhakikisha Watanzania wanachangamkia fursa za biashara ikiwemo ya madini, Rais Magufuli alikiagiza Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kuwasaidia wanyabiashara waweze kuwekeza kwa uhakika.
Alisema yeye na serikali yake wanawaunga mkono wafanyabiashara na akawataka wautumie muda huu wa uongozi wake vizuri kwa kuwekeza kwenye miradi ikiwemo madini na mafuta.

MARAIS WASTAAFU WA MAREKANI WACHANGIA FEDHA KUSAIDIA WAATHIRIKA WA JANGA LA KIMBUNGA



Marais watano wa zamani nchini Marekani wamekusanyika katika tamasha la kuchangisha fedha za kuwasaidia waathirika wa janga la kimbunga ambacho kiliyakumba maeneo kadha ya Marekani.
Rais Barack Obama, George W Bush, Bill Clinton, George HW Bush na Jimmy Carter wote walikutana Texas hapo jana kwa lengo la kuwasaidia wale walikumbwa na janga la vimbunga Irma na Maria.
Marais hao wamefanikiwa kuchangisha kiasi cha dola za kimarekani milioni 31 hadi sasa mchango ambao utasaidia jamii za Florida, Puerto Rico na visiwa vya Marekani vya Virgin vilivyopigwa na kibunga.

KABILA ASHAURIWA NA UN


Umoja wa Mataifa umetoa wito wa kuachiwa mara moja kwa watu 30, wa chama kikuu cha upinzani katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kutoka rumande ili waendelee na shughuli zao za kisiasa na za kila siku.
Wanachama wa vyama vya Union for Democracy na wenzao wa Social Progress, walikamatwa siku ya Jumapili katika mji wa Lubumbashi, ulioko Kusini mashariki mwa nchi hiyo, baada ya polisi kusambaratisha mkutano wao.
Aidha, utawala wa Rais wa nchi hiyo, Joseph Kabila umepiga marufuku mkutano wa aina yoyote wa kisiasa pamoja na maandamano ya upinzani, tangu muda wake wa kukaa madarakani ulipoisha kisheri mwaka mmoja uliopita.
Tume ya uchaguzi nchini humo imesema kuwa haitakuwa rahisi kuandaa uchaguzi mkuu wa Urais, kabla ya mwezi Aprili mwaka ujao kwani hali ya kisiasa bado ni tete nchini humo hasa baada ya kuzuiwa kwa mikutano ya hadhara.

SIBADILI MSIMAMO WANGU KENYATA ATETA











Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta amefanya mazungumzo na mwenyekiti wa tume ya uchaguzi na mipaka nchini humo, Wafula Chebukati kabla ya uchaguzi wa marudio uliozua utata  nchini humo.
Kenyatta ambaye amekuwa akishinikizwa na wadau mbalimbali kukutana na afisa huyo pamoja na mgombea urais wa muungano wa NASA, Raila Odinga, ili kutatua mzozo wa kisiasa unaoendelea kuikabili nchi hiyoAidha, baada ya mkutano huo, Kenyatta ametuma taarifa kwa vyombo vya habari iliyosema kuwa yeye hana masharti yoyote kwa tume hiyo, isipokwa tu kwamba uchaguzi ufanyike siku ya Alhamisi kama ilivyoagizwa na mahakama ya juu
“Msimamo wangu ni ule ule, Wakenya wapewe nafasi ya kushiriki kwenye zoezi la kidemokrasia la kupiga kura kama tu ilivyoagizwa na mahakama ya juu. hatuna masharti yoyote kwa IEBC,” amesema Kenyatta

MWAKYEMBE AKUTANA NA VIONGOZI WA MASUA TANZANIA

Waziri Mwakyembe Akutana Na Viongozi Wa Chama Cha Mashua Tanzania (TSAA)

Pix 01
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt. Harrison Mwakyembe akifafanua jambo kwa baadhi ya viongozi wa Chama cha Mashua Tanzania (TSAA) wakati alipokutana na viongozi hao kujadili changamoto mbalimbali wanazokutana nazo.
Pix 02
Mwanyekiti wa Chama cha Mashua Tanzania (TSAA) Bw. Philemon Nasari (kushoto) akimueleza  Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt. Harrison Mwakyembe changamoto mbalimbali wanazokutana nazo.
Pix 03
Mwanyekiti wa Chama cha Mashua Tanzania (TSAA) Bw. Philemon Nasari (kulia) akimkabidhi Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt. Harrison Mwakyembe DVD yenye matukio mbalimbali ya chama hicho wakati alipokutana na viongozi hao kujadili changamoto mbalimbali wanazokutana nazo.
Pix 04
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt. Harrison Mwakyembe (mwwenye miwani) akiwa katika picha ya pamoja na viongozi wa Chama cha Mashua Tanzania (TSAA) na maafisa wa Idara ya Michezo wakati alipokutana na viongozi hao kujadili changamoto mbalimbali wanazokutana nazo.

JESHI LA POLISI MBEYA LATOA TAARIFA HII DHIDI YA UHALIFU


Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya limeendelea kufanya misako, operesheni na doria zenye tija katika maeneo mbalimbali ili kudhibiti uhalifu na wahalifu na limekuwa likishirikiana na wananchi na wadau wengine katika jitihada hizo za kukabiliana na uhalifu na wahalifu na kupata mafanikio makubwa ikiwa ni pamoja na kupungua kwa matukio makubwa ya uhalifu.
Mafanikio yaliyopatikana katika Misako/Doria ni kama ifuatavyo:-
KUPATIKANA NA NOTI BANDIA.

Mnamo tarehe 22.10.2017 majira ya saa 15:00 Alasiri, Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya lilifanya msako huko eneo la Sisimba lililopo Kata na Tarafa ya Sisimba, Jiji na Mkoa wa  Mbeya na kufanikiwa kumkamata mtu mmoja aliyefahamika kwa jina la FAUSTINA MAGANGA [20] Mkazi wa Mtaa wa Teku akiwa na noti bandia 10 za Tshs 10,000/= sawa na Tshs 200,000/= kama zingekuwa halali.
Noti hizo zilikuwa na namba BU 3352850 noti 5 na BU 3352846 noti 5. Mtuhumiwa atafikishwa Mahakamani mara baada ya upelelezi kukamilika.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linaongeza jitihada za kuzuia na kupunguza matukio ya ajali za barabarani kwa kuhakikisha madereva na watumiaji wengine wa barabara wanafuata sheria na alama za usalama Barabarani. Aidha kumekuwa na ajali 01 ya vifo na majeruhi kama ifuatavyo:-
Mnamo tarehe 22.10.2017 majira ya saa 15:45 jioni huko maeneo ya DM Hotel, Kata ya Bulyaga, Tarafa ya Tukuyu mjini, Wilaya ya Rungwe, Mkoa wa Mbeya katika Barabara kuu ya Tukuyu/Mbeya, Gari yenye namba za usajili T 756 BGS aina ya Toyota Chaser iliyokua ikiendeshwa na dereva aitwaye CHARLES MWAMBENA [26] Mkazi wa Tukuyu ikitokea Kitongoji cha Bagamoyo kuelekea Tukuyu mjini iliacha njia na kwenda kuwagonga watembea kwa miguu wawili 1. BENARD FORTNATUS KASELA [22] Mwanachuo wa FDC – Katumba na Mkazi wa Nansio – Ukerewe
na 2. AYOUB WILLIAM MWAIJENGO [20] Mwanachuo wa FDC – Katumba, Mkazi wa mbeya na kusababisha vifo vyao wakiwa wanapatiwa matibabu katika Hospitali ya Wilaya – Makandana.
Inadaiwa kuwa Gari hilo baada ya kuwagonga watembea kwa miguu lilipinduka na kisha kutumbukia mtaloni. Aidha katika ajali hiyo watu watatu walijeruhiwa akiwemo dereva wa Gari hilo na watu wengine wawili ambao walikuwa katika gari hilo ambao ni ALLAN JAMES ALLAN [30] Mkazi wa Bagamoyo na NKUNDWE JOEL KASOKELA [29] Mkazi wa Msasani.
Chanzo cha ajali kinachunguzwa. Majeruhi wamehamishiwa Hospitali ya Rufaa Mbeya kwa matibabu zaidi. Mtuhumiwa ambaye ni dereva wa gari hiyo amekamatwa na amelazwa Hospitali ya Wilaya ya Rungwe – Makandana akiwa chini ya ulinzi wa Polisi. Miili ya marehemu imehifadhiwa Hospitali ya Wilaya ya Rungwe – Makandana.

Aidha Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya limeendelea kukabiliana na matukio makubwa ya uhalifu pamoja na wahalifu. Jitihada zinaendelea kwa kushirikiana na wananchi kuhakikisha Mkoa wetu unakuwa mahala salama. Hata hivyo Kumekuwa na matukio 02 ya mauaji kama ifuatavyo:-

Mnamo tarehe 22.10.2017 majira ya saa 13:00 mchana huko Kijijj cha Mwala, Kata ya Ilembo, Tarafa ya Isangati, Wilaya ya Mbeya Vijijini, Mkoa wa Mbeya, Mtu mmoja aliyefahamika kwa jina la ASA MWILE @ MWASENGA [21] Mkazi wa Kijiji cha Masoko aliuawa kwa kupigwa na kundi la wananchi walioamua kujichukulia sheria mkoanani wakitumia silaha za jadi fimbo na mawe.
Inadaiwa kuwa chanzo cha tukio hilo ni tuhuma za wizi baada ya marehemu kukutwa akivunja duka mali ya ZICKY YORAM [34] Mkazi wa Mwala hivyo wananchi kupiga yowe na kuanza kumshambulia hadi kufa. Mwili wa marehemu umehifadhiwa Hospitali Teule ya Ifisi. Upelelezi unaendelea
Mnamo tarehe 22.10.2017 majira ya saa 07:00 asubuhi huko maeneo ya Sae, Kata ya Ilomba, Tarafa ya Iyunga, Jiji na Mkoa wa Mbeya.  Mtu asiyefahamika jina wala anuani yake mwenye jinsia ya kiume anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka 20-30 jinsia ya kiume aliuawa kutokana na kupigwa na wananchi wanaojichukulia sheria mkononi.
Chanzo cha tukio ni tuhuma za wizi. Mwili wa marehemu umehifadhiwa Hospitali ya Rufaa Mbeya. Watuhumiwa wanne wamekamatwa kuhusiana na tukio hilo na mahojiano zaidi yanaendelea. Upelelezi unaendelea.







WITO:

Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya Kamishina Msaidizi wa Polisi MUSSA A. TAIBU anatoa wito kwa Madereva kuwa makini wanapotumia vyombo ili kuepuka ajali zinazoweza kuepukika. Kaimu Kamanda TAIBU anawataka madereva kufuata, kuheshimu na kuzingatia sheria na alama za barabarani ili kuepuka ajali. Aidha anatoa wito kwa wananchi kuendelea kutoa ushirikiano kwa Jeshi la Polisi ikiwa ni pamoja na kutoa taarifa za uhali/wahalifu na watuhumiwa mbalimbali wa uhalifu ili wachukuliwe hatua stahiki za kisheria. Pia Kamanda TAIBU anawataka wananchi kutii sheria bila shuruti na kuacha kujichukulia sheria mkononi kwani ni kinyume cha sheria na kamwe Jeshi la Polisi halitakuwa na huruma na mtu yeyote wala kikundi cha watu watakaoshindwa kutii sheria.
           Imesainiwa na:
[MUSSA A. TAIBU – ACP]
KAIMU KAMANDA WA POLISI MKOA WA MBEYA

DR KIGWANGALA AFUTA UTARATIBU WA UTOAJI VIBALI VYA UWINDAJI

..
Katika kile alichoeleza kuwa ni
kuimarisha sekta ya maliasili na utalii iweze kutoa mchango unaostahili kwa
jamii na taifa kwa ujumla, Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi
Kigwangalla
 amesitisha utaratibu wa kuhuisha upya vibali vyote vya makampuni ya uwindaji wa kitalii ambavyo
vilitolewa mwaka huu mwezi Januari i
li kupisha utaratibu mpya wa utoaji wa
vibali hivyo kwa njia ya mnada.
Dk. Kigwangalla ametangaza uamuzi
huo jana mjini Dodoma katika mkutano alioutisha wa wadau wa sekta ya maliasili
na utalii ambao ulilenga kukusanya maoni, kero na kujadili changamoto
mbalimbali zinazoikabili sekta hiyo muhimu nchini kwa ajili ya kuzitafutia
utatuzi wa haraka.
“Kwa mamlaka niliyopewa na sheria ya
wanyamapori namba 5 ya mwaka 2009, nimeamua bila kushawishiwa na mtu yeyote
yule wala kushauriwa na mtu yeyote yule zaidi ya kusikiliza tu ushauri wa
kitaalamu na ushuari wa ndugu yangu Mhe.  Naibu Waziri, lakini  sasa
hivi ninavyotamka haya sijamshirikisha mtu yeyote yule, nimeamua kwa mamlaka
yangu, nasitisha vibali vyote  vya uwindaji wa makampuni ambavyo
vilitolewa mwaka huu mwezi Januari kwa maana ya ‘kurenew’ (kuhuisha).
“Nasitisha ili kupisha mchakato wa
kutengeneza taratibu mpya za kuendesha ugawaji wa vitalu kwa njia ya mnada,
tunataka twende kwenye ‘auction’ (mnada) ya vitalu, na auction (mnada) iwe ya
wazi, iwe na faida kubwa  zaidi, na natoa siku sitini utaratibu huo uwe
umekamilika ili tuweze kuendesha ‘auction’ (mnada) kabla ya muda wa kuanza kwa
awamu ya miaka mitano ambayo ni january 2018 mpaka 2022.
“Kwahiyo ndani ya siku sitini,
wataalam mkae mniletee utaratibu wa namna bora zaidi ya uwazi inayotoa haki ya
kugawa vitalu lakini pia yenye faida kubwa zaidi kama tunavyoelekezwa na mpango
wa taifa wa miaka mitano kwamba ni lazima vitalu vyote vifanyiwe ‘auction’
(mnada)”. alisema Dk. Kigwangalla.
Alisema utaratibu huo hautahusisha
vitalu vilivyopo kwenye maeneo yenye migogoro ya ardhi kwa sasa mpaka pale
migogoro hiyo itakapomalizika.
“Ni mwiko kugawa vitalu kwenye
maeneo yenye mgogoro, kuna maeneo kama vitalu vilivyopo Loliondo, kuna mgogoro,
ni mwiko kugawa vitalu, kuna maeneo kama Lake Natron kuna mgogoro, mwiko kugawa
vitalu, mpaka tutatue migogoro kwanza, Kama kuna mtu alipewa kibali huko nyuma
ajue hicho kibali cha renewal  kimekufa leo na mimi ndio nimekiua” alisema
Dk. Kigwangalla.
Kuhusu uwindaji wa Wenyeji kwenye
maeneo ya wazi uliosimamishwa kwa muda wa miaka miwili sasa, Dk. Kigwangalla
alitoa muda wa siku sitini kwa watendaji wa wizara yake kukamilisha masharti
mapya ya uendeshaji wa biashara hiyo na kuyawasilisha kwake aweze kuyasaini ili
kufungulia biashara hiyo.
“Natoa siku sitini, wataalam wetu
mnaohusika na utoaji wa vibali vya uwindaji wa wenyeji mkamilishe masharti
mapya mniletee nisaini tutoe vibali, hatuwezi kuzuia wenyeji wanufaike na
rasilimali ambazo ziko huko vijijini alafu tukaruhusu makampuni ya watu kutoka
nje kuja kuwinda wakaondoka na nyama, ni lazima tutoe haki kwa wazawa kama wapo
wanaovunja masharti sisi tudhibiti na tusimamie sheria” alisema Dk.
Kigwangalla.
Wakati huo huo, Waziri Kigwangalla
amemuagiza Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Mej. Jen. Gaudence
Milanzi kuwasiliana na Msajili wa Hazina kwa ajili ya kuanza mchakato wa
kuzirudisha serikalini hoteli za kitalii kumi zilizobinafsishwa miaka 1990 kufuatia
kushindwa kutimiza masharti ya mkataba wa uendeshaji.
“Niagize Katibu Mkuu wa Maliasili na
Utalii uwasiliane na mamlaka ambayo ina dhamana ya kushikilia mali zilizokuwa
za Serikali ambazo ziliuzwa kwa maana ya msajili wa hazina, umueleze nimetoa agizo
kwamba hizi hoteli zote ambazo zimekiuka masharti na hivyo kuathiri utendaji wa
sekta ya utalii nchini na hivyo kuathiri uchumi mpana wa taifa letu,
zichukuliwe na zirudi kuwa mali ya serikali ili serikali ipate fursa ya
kuzitangaza upya na kutafuta waendeshaji wapya watakaoweza kuendesha hoteli
hizi  kwa tija na ufanisi kwa maana ya kukuza sekta ya utalii ambayo
inachangia asilimia 17 ya pato la taifa.
“Nimetoa agizo hoteli hizi 10 ambazo
zimeshindwa kukidhi masharti ya mikataba ya mauziano, mchakato wa kuzirudisha
Serikalini uanze mara moja na ukamilike ndani ya siku sitini.
Alisema kumekuwepo na changamoto
kubwa ya uhaba wa vyumba katika sekta ya utalii hali iliyosababishwa na
ubinafsishaji wa hoteli 17 za Serikali uliofanywa miaka 1990 kwa nia njema ya
kuimarisha usimamizi na uendeshaji wa hoteli hizo kupitia sekta binafsi lengo
ambalo halikufikiwa kwa baadhi ya hoteli hizo.
“Baada ya kufanya uchunguzi katika
hoteli zote 17 tulizouza ni saba tu zinafanya vizuri, hoteli zinazofanya vizuri
na zimekidhi masharti yote ambayo yalikuwepo kwenye ile mikataba ni Kilimanjaro
Hotel, Kunduchi Beach Hotel, Mt. Meru Hotel, New Africa Hotel, New Safari
Hotel, Mafia Highland Hotel na Hotel 77.
“Hoteli 10 zimeshindwa kukidhi
masharti ya mikataba ya mauziano na mwaka ulioisha Serikali ilifanya uchunguzi
kwenye hoteli nyingine nne kati ya hizo 10 ambazo ni Robo Wildlife Lodge,
Seronera Wildlife Lodge, Ngorongoro Wildlife Lodge na Lake Manyara Hotel, na
zote zilionesha zipo chini ya kiwango na hazikidhi mahitaji.
“Kwa kuwa watu hawa wamekiuka
masharti ya ubinafsishaji kama walivyopewa wakati wananunua hizo hoteli ni
wakati muafaka sasa kwa Serikali kuvunja hii mikataba kuzichukua hizi hoteli na
kuzibinafsisha kwa watu wengine watakaoweza kuziendesha kwa faida lakini pia
kuziendesha kwa tija zaidi” alisema Dk. Kigwangalla.
Awali akijibu baadhi ya hoja za
wadau wa mkutano huo kuhusu wizara yake kuwa na vishawishi vingi vya rushwa na
fitna ambazo husababisha viongozi wengi kutodumu kwenye nafasi zao, Dk.
Kigwangalla alisema kamwe hatoruhusu hali hiyo ijitokeze kwa kuwa hata
aliyemteua anamjua vizuri kuwa ni muarobaini wa changamoto hizo.
“Mimi nipo hapa kwenye hiki kiti, na
nitakuwepo kama sababu ni hiyo ya maslahi, Mimi sihongeki, sinunuliki, na
sishawishiki, najua hata aliyeniweka hapa ananijua vizuri, kwahiyo alivyoniweka
hapa alishajua hii ni dawa, muarobaini.
“Watu wote humu ndani tuna njaa,
lakini njaa yangu nabaki nayo mwenyewe, bora nife kwa heshima zangu kuliko
kuaibika na kudharaulika kwa kuchukua rushwa ama kwa kutokutenda haki ama kwa
kumuonea mtu.
“Hilo nina uhakika nalo, kwa maana
ya rushwa, maslahi ya kibiashara hapana, hutonikuta mimi huko, na kama kuna
mdau mmoja anadhani kuna siku anafkiria anaweza kuja kuongea na mimi kwa
maslahi binafsi akaweka mbele mazingira ya rushwa, sana sana ataona nimemuaga
na kikao chetu kimeishia hapo, kwahiyo ukija kwangu njoo na ishu ambayo ipo
straight maslahi ya umma yapo ndani yake utaraibu wa kisheria upo”. Alisema Dk.
Kigwangalla.
Miongoni mwa maagizo mengine
aliyoyatoa kwenye kikao hicho kwa watendaji wa wizara yake ni kuandaa taratibu
za kuanzishwa kwa mwezi maalumu wa kuadhimisha utamaduni wa Mtanzania (Tanzania
Heritage Month), Makumbusho ya Marais wa Tanzania (Presidential Museum) na
Utalii wa Mabasi kwa Miji ya Dar es Salaam na Arusha (Dar Bus Tour/ Arusha Bus
Tour) ili kurahisisha utoaji wa huduma kwa watalii katika miji hiyo.
Katika mkutano huo wadau wa maliasii
na utalii walipata fursa ya kutoa maoni, mapendekezo ushauri na kero mbalimbali
wanazokumbana nazo katika sekta hiyo ambazo ziliahidiwa kufanyiwa kazi kwa
haraka na Waziri Kigwangalla.  Miongoni mwa ushauri na mapendekezo
waliyotoa ni pamoja na kuanzishwa kwa mamlaka moja inayosimamia rasilimali za
misitu nchini na kufunguliwa kwa biashara ya kusafirisha viumbe hai nje ya
nchi.
Mkutano huo wa siku moja
ulihudhuriwa na viongozi wakuu wa Wizara ya Maliasili ambao ni Naibu Waziri,
Mhe. Japhet Hasunga, Katibu Mkuu, Mej. Jen. Gaudence Milanzi, Naibu Katibu
Mkuu, Dk. Aloyce Nzuki, Wakurugenzi wa Idara na Wakuu wa taasisi zilizopo chini
ya Wizara hiyo.

Wengine ni wadau zaidi ya 200 kutoka
sekta mbalimbali ya maliasili na utalii ambao ni wawakilishi kutoka vikundi,
taasisi, vyama na vyombo mbalimbali vinavyoshughulika na utoaji wa huduma
katika sekta ya utalii, wanyamapori, misitu na nyuki pamoja na waandishi wa
habari.