Uchumi wa Nchi Unaanguka, Katiba ya Nchi Inakanyagwa, Utumieni Uchaguzi Huu Kuionyesha Serikali Mnayakataa Mambo Haya.Sehemu ya Hotuba ya Kiongozi wa Chama katika Mkutano wa Ufunguzi wa Kampeni za Udiwani - Kijichi]
Ndugu Watanzania,Ndugu Wanatemeke
Ndugu Wanakijichi
Pamoja na masuala haya ya uchaguzi mdogo hapa Kijichi ninaomba nizungumzie masuala machache ya kitaifa. Nafanya hivi kwa sababu baada ya siku thelathini kutoka leo hatutakuwa tena na nafasi ya kuzungumza majukwaani kama viongozi wa vyama vya siasa kwa sababu ya zuio lisilo la kikatiba ambalo limewekwa na Rais dhidi ya mikutano ya hadhara. Hivyo, sisi tumeamua kutumia majukwaa haya ya kampeni za uchaguzi mdogo kuzungumzia mambo ya kitaifa pia.
Tutaitumia mikutano hii ya kampeni kuelezea hali mbaya ya uchumi wa nchi yetu, pamoja na kuminywa kwa haki za wananchi na kusiginwa kwa Katiba ya Taifa letu.
Haki: Nitaanza na hili la haki za wananchi, nyie mtakuwa mashahidi juu ya jambo hili la kuvunjwa kwa haki za wananchi, kwa sababu ya muda nitatoa mifano minne kama ifuatavyo:
1. Utawala huu wa awamu ya 5 ndio utawala unaovunja haki za watu kwa kiwango kikubwa sana ambacho hakijawahi kuonekana nchini, ndani ya muda wake mfupi wa miaka miwili ya utawala huu, magazeti zaidi ya matatu yameshafungiwa sasa, magazeti yote hayo yalionekana kuwa mwiba kwa Serikali kwa kuhoji na kuandika mambo mbalimbali juu ya hali ya Nchi yetu. Si hilo tu, bado kuna zuio lisilo la kikatiba la Rais juu ya mikutano ya hadhara, huku mamia ya watu wakiwa wameshtakiwa, na wengine kuhukumiwa vifungo na faini, kwa kutumia sheria mbaya ya mitandao ya mitandao ya kijamii, kwa sababu tu ya kutoa maoni yao ambayo yako kinyume na Serikali. Yote haya ni rekodi mpya ya uvunjivu wa haki za wananchi nchini mnayopaswa kuikataa.
2. Ni ndani ya kipindi hiki cha Serikali ya awamu ya 5, ndipo utu umekosekana kabisa nchini, wananchi wanavunjiwa nyumba zao walizozijenga kwa jasho lao bila hata kulipwa fidia, huku hata mahakama zetu pamoja na Katiba ya nchi kutokuheshimiwa kwa Serikali kuvunja hata nyumba ambazo mahakama imeweka zuio, nyie Wanakijichi ni mashuhuda wa hili, ndugu zenu wa Kimara wamedhalilishwa kwa kuvunjiwa nyumba zao bila fidia na kurudishwa kwenye umasikini. Hali hiyo si Dar tu hapa, wananchi wanavunjiwa nyumba zao bila fidia mikoa mbalimbali nchini, hivi karibuni ni Tabora. Mnao wajibu wa kuwafuta machozi hawa, kwa kuhakikisha mnakikataa chama tawala.
3. Ni kipindi hiki pia ndio tumeshuhudia watu wanaouwawa hovyo hovyo hovyo tu, nanyi ni mashahidi hapa Dar, kila siku inaokototwa miili tu ya watu kule ufukweni Coco Beach, wakiwa wameuawa. Serikali haijawahi kusema chochote juu ya miili hiyo inayookotwa, tuna serikali isiyojali uhai wa watu wake. Si hilo tu, mbunge mwenzangu Tundu Lissu amepigwa risasi zaidi ya 30 zaidi ya mwezi mmoja sasa, mmesikia mtu yoyote amekamatwa kwa tukio hilo? Na msidhani wanaoathirika ni watu wa Upinzani tu, la hasha, aliyekuwa Mwenyekiti wa CCM wa Wilaya ya Kasulu amepotea tangu mwezi julai, mama mpaka leo hajapatikana. Kuinyima kura CCM ni kuonyesha uhai wa hawa watu una maana kwenu, ni kuonyesha mnajali.
4. Serikali hii imekataa kuwapa haki yenu ya kuwa na mchakato mpya wa Katiba Mpya, mchakato utakaoanzia kwenye maoni ya Tume ya Jaji Warioba, maoni yenu wananchi. Rais anasema kwa kiburi kuwa hakuwaahidi Katiba, na wapambe wake wanazunguka huku na huku kupinga uwepo wa mchakato wa Katiba mpya. Kukikataa chama tawala kwenye uchaguzi huu ni kukiambia kuwa mamlaka ya uongozi ni yenu nyie wananchi, na kwamba mnataka mchakato wenu wa Katiba uendelee.
Hiyo ni mifano michache tu ya ubinywaji wa haki kinyume kabisa na Katiba ya nchi yetu, Katiba ambayo Rais aliapa kuilinda. Wananchi wa Kijichi hampaswi kumchagua mtu atokanaye na chama tawala, chama kinachovunja Katiba na kuminya haki za wananchi namna hiyo kama tulivyoonyesha.
Uchumi: Hali ya uchumi wa Nchi ni mbaya sana, ni mbaya mno kinyume kabisa na takwimu zinazotolewa na kuonyesha kuwa kasi ya ukuaji wa uchumi kuwa kubwa kwa kiwango cha 7%. Mie ni mchumi, pamoja na wachumi wengi wenzangu tunajua kuwa shughuli za uchumi zimedorora, na nyie wananchi ni mashahidi juu ya hali mbaya ya uchumi wa nchi, hili ni jambo la dhahiri kabisa.
Oktoba 10, 2017 Serikali yenyewe kupitia Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) ilitoa taarifa yake juu ya hali ya uchumi wa nchi yetu, taarifa iliyoonyesha kuwa hali ya uchumi wa nchi si nzuri kabisa, kukiwa na dalili zote za uchumi wa nchi yetu kusinyaa na kudidimia, mfumuko wa bei ukionyesha kupanda na thamani ya shilingi kudidimia.
Taarifa hiyo inaonyesha namna hali ya uchumi wetu inavyozidi kuwa mbaya zaidi kwa wananchi wa hali ya chini, mfumuko wa bei umepanda mno tangu kuanza kwa utekelezaji wa bajeti ya 2017/18, ongezeko ambalo limechangiwa zaidi na kupanda kwa bei ya bidhaa za chakula (bidhaa ambazo wananchi wengi zaidi mnazitumia).
Baadhi ya bidhaa za vyakula zilizochangia ongezeko hilo ni dagaa asilimia 7.6, matunda makavu kama nazi kwa (3.1), viazi vitamu kwa (3.0), mchele (1.5) na ndizi (1.5). Bidhaa nyingine zilizochangia ni mkaa kwa asilimia 4.0, dizeli (2.4) na petroli (0.6). Ukizitazama bidhaa zote hizi ni zile ambazo zinatumiwa zaidi na wananchi wa kawaida kabisa, nyie watu wa Kijichi. CCM wameamua kuwadumbukiza kwenye umasikini.
Pamoja na kupanda kwa bei za vyakula, taarifa ile ilionyesha kuwa thamani ya sarafu ya Tanzania imeshuka, uwezo wa Tsh. 100 kununua bidhaa umeshuka hadi Tsh. 92.18. Maana yake ni kuwa kama mwaka 2016 shilingi 100,000 ilikupa bidhaa za shilingi 100,000. Mwaka huu 2017 shilingi 100,000 inakupa bidhaa za shilingi 92,000. Kwa hiyo ili upate bidhaa za shilingi laki moja inakubidi uongeze shilingi elfu 8 zaidi. Hali hii inawaumiza mno nyie wananchi.
Wakati Rais wa sasa akiingia madarakani bei ya sukari ilikuwa ninshilingi 1800 mpaka 2000, kwa sasa bei ya sukari ni shilingi 2800 hadi 3000. Gharama za maisha yenu zimepanda mno, Serikali hii imeshindwa kabisa kusimamia uchumi wa nchi.
Lakini msidhani ni uchumi wenu tu nyie watu wa chini ndio mbaya, hapana, ni nchi nzima, jana tulitoa taarifa ya uchambuzi wa takwimu za uchumi wa Serikali inayoonyesha kuwa hali ni mbaya nchi nzima, uzalishaji wa viwanda ukishuka kwa 50%, ujazo wa fedha ukishuka kwa 51%, mikopo kwa sekta binafsi ikishuka kwa 23%, mapato ya bidhaa za forodha yakiwa ni shilingi bilioni 300 tu kutoka bilioni 500 iliyotarajiwa.
Sekta ya Kilimo imeshuka mpaka kiwango cha kabla ya Uhuru, kwani kasi ya ukuaji wa sekta ya Kilimo mwaka 2016 ilikuwa 1.6% tu. Wakulima wa Korosho hawajapewa pembejeo, hivyo uzalishaji wa zao linalotuingia mapato ya Kigeni zaidi nchini utashuka msimu huu wa mavuno, Tumbaku (zao la pili Kwa kuingiza Fedha za kigeni) tayari wakulima wanalia, mazao ya choroko na kunde bei imeshuka kwa zaidi ya 500%, Pamba uzalishaji umeshuka Kwa 63% kati ya mwaka 2015 na 2017 (miaka miwili ya utawala wa awamu ya 5), na mauzo Nje ya dhahabu kuanza kushuka na hivyo kupelekea shilingi kushuka thamani na hivyo mfumuko wa bei kupanda Kwa kasi.
Kiufupi, ukuaji wa pato la taifa umesinyaa katika robo ya pili ya mwaka huu, ikiwa ni - 0.6, ukuaji hasi ukionyesha kusinyaa kwa uchumi. Tunazo dalili zote za kuanguka kwa uchumi wa nchi.Wanakijichi, mna sababu tena ya kuendelea kukichagua chama kilichowafikisha kwenye hali hiyo? Mnataka uchumi wa nchi ushuke zaidi? Mnataka watu wetu waokotwe zaidi Coco Beach? Mnataka magazeti zaidi yafungiwe? Mnataka bei ya sukari na vyakula vingine ipande zaidi? Kama hamtaki hilo mnao wajibu wa kumpuuza mgombea wa CCM, na kumchagua mgombea wa ACT Wazalendo, ndugu Edgar Mkosamali ili asaidiane nanyi kutatua kero zenu kama alivyojieleza hapa. Mkifanya hivyo mtakuwa pia mmeiambia Serikali irelebishe masuala haya ya Kitaifa.
Ahsanteni kwa kunisikiliza
Kabwe Z. Ruyagwa Zitto
Kiongozi wa Chama - ACT Wazalendo
Oktoba 29, 2017
Kijichi
Dar es salaam