LOWASSA ANENA ALICHOZUNGUMZA NA RAISI MAGUFULI IKULU

HATIMAYE LOWASSA AANIKA ALICHOZUNGUMZA NA RAIS MAGUFULI IKULU

 
Mjumbe wa Kamati Kuu Chadema, Edward Lowassa ametoa ufafanuzi kuhusu mazungumzo yake na Rais John Magufuli yaliyofanyika Ikulu Dar es Salaam siku sita zilizopita. 



Kupitia taarifa yake kwa vyombo vya habari aliyoitoa leo Januari 15, 2015, Lowassa amesema alimueleza masuala mbalimbali yanayowakumba wananchi na wanasiasa tangu Serikali ya Awamu ya Tano iingie madarakani.


“Nilijadiliana naye kuhusu masuala mbalimbali ya msingi kuhusu nchi yetu ikiwemo kutoheshimiwa kwa Katiba na sheria, uminywaji wa demokrasia, ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu,” amesema na kuongeza,


“Unaohusisha kupotea kwa watu, kuvamiwa, kutishwa na kushambuliwa kwa viongozi wa kisiasa wa upinzani na hali ngumu ya uchumi kwa wananchi wetu. Ni imani yangu kwamba Rais atayazingatia na kufanyia kazi masuala haya kwa masilahi yetu”.


Kupitia barua hiyo, Lowassa amesema yupo madhubuti kuliko wakati mwingine wowote ule.

SEKTA YA MADINI IWE MCHANGO MKUBWA KWENYE PATO LA TAIFA ASEMA MHE:DOTTO BITEKO

SEKTA YA MADINI LAZIMA IWE NA MCHANGO MKUBWA KWENYE PATO LA TAIFA: MHE DOTTO BITEKO

Naibu Waziri wa Wizara ya Madini Mhe Dotto Mashaka Biteko akizungumza na wakuu wa idara na vitengo pamoja na wafanyakazi wote wa wizara ya madini mara baada ya kuwasili ofisini Mjini Dodoma, Leo Januari 15, 2018. Picha Zote Na Mathias Canal
Naibu Waziri wa Wizara ya Madini Mhe Dotto Mashaka Biteko akisisitiza jambo wakati akizungumza na wakuu wa idara na vitengo pamoja na wafanyakazi wote wa wizara ya madini mara baada ya kuwasili ofisini Mjini Dodoma, Leo Januari 15, 2018.
Naibu Waziri wa Wizara ya Madini Mhe Stanislaus Nyongo akizungumza jambo kabla ya kumkaribisha Naibu Waziri mwenzake katika Wizara hiyo Mhe Dotto Mashaka Biteko kuzungumza na wakuu wa idara na vitengo pamoja na wafanyakazi wote wa wizara ya madini mara baada ya kuwasili ofisini Mjini Dodoma, Leo Januari 15, 2018.
Naibu Waziri wa Wizara ya Madini Mhe Dotto Mashaka Biteko akizungumza na wakuu wa idara na vitengo pamoja na wafanyakazi wote wa wizara ya madini mara baada ya kuwasili ofisini Mjini Dodoma, Leo Januari 15, 2018.


Na Mathias Canal, Dodoma

Sekta ya Madini inachangia kati ya asilimia 3.5 mpaka 4 katika Pato la Taifa ukilinganisha na sekta zingine ambazo zimejitutumua kwa kiasi kikubwa katika mchango mahususi wa pato la Taifa nchini Tanzania.

Naibu Waziri wa Wizara ya Madini Mhe Dotto Mashaka Biteko amebainisha kuwa kiasi cha kati ya asilimia 3.5 mpaka 4 ni kidogo sana ukilinganisha na umuhimu wa sekta hiyo nchini hivyo Wizara ya Madini imekusudia kuongeza tija katika mchango wa pato la Taifa kupitia sekta hiyo muhimu ya Madini.

Mhe Biteko amebainisha hayo Leo Januari 15, 2018 wakati akizungumza na wakuu wa idara na vitengo pamoja na watumishi wa Wizara ya Madini ofisi Kuu Mjini Dodoma huku akiwataka watumishi wote kufanya kazi kwa bidii, nidhamu na uzalendo mkubwa kwa manufaa ya Taifa.

Alisema kuwa sekta ya Madini ni muhimu nchini kutokana na rasilimali Madini ilizonazo hivyo watumishi wote wanapaswa kufikiria namna ya kufanya kazi kwa tija ili kuwa na ongezeko la mchango mkubwa katika pato la Taifa.

"Natamani nione kwenye taarifa ya robo mwaka ya BOT ikisoma kwamba sekta ya madini inachangia angalau asilimia 10 ya Pato la Taifa kuliko ilivyo hivi sasa na hilo naamini linawezekana kwa ushirikiano wa pamoja" Alisisitiza Mhe Biteko

Mhe Biteko alisema kuwa hakuna mtu yeyote ambaye atatutumua mabega kwamba ni mkubwa katika Wizara badala yake ukubwa wa cheo na umri utaonekana katika matokeo muhimu na makubwa katika utendaji kazi.

"Mimi kuwa Naibu Waziri hapa So What... kama sitofanya kazi yenye matokeo makubwa kutokana na imani niliyopewa na Rais nitakuwa si lolote, hivyo kwa ushirikiano wenu pekee tutaweza kutimiza utendaji uliotukuka na wenye manufaa makubwa" Alikaririwa Mhe Biteko wakati akizungumza na watumishi wa Wizara ya Madini

Mhe Biteko alisema kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt John Pombe Magufuli anafanya kazi nzuri kwa manufaa makubwa ya watanzania wote hivyo watumishi mbalimbali wa serikali, sekta binafsi na wananchi kwa ujumla wanapaswa kuunga mkono jitihada hizo pasina kurudisha nyuma makusudi na matakwa ya utekelezaji wa ilani ya ushindi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mwaka 2015-2020.

Asubuhi siku ya Jumatatu Januari 8, 2018 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt John Pombe Magufuli alimuapisha Mhe Dotto Mashaka Biteko kuwa Naibu Waziri wa madini, Ikulu Jijini Dar es salaam.

KOREA KASKAZINI YATUPA KOMBORA KUBWA


Taifa la Korea Kaskazini limefanyia majaribio kombora lake la masafa marefu lililoruka juu zaidi na kombora hilo tayari limeonekana kuhatarisha usalama duniani kulingana na waziri wa maswala ya ulinzi nchini Marekani James Mattis.

Jaribio hilo la kombora mapema siku ya Jumatano lilianguka katika maji ya Japan.
Liliruka kwa urefu wa kilomita 4,500 na kusafiri umbali wa kilomita 960 kulingana na jeshi la Korea Kusini.

Ni jaribio la hivi karibuni ambalo limezua hali ya wasiwasi, Mara ya mwisho kwa taifa hilo kulifanyia jaribio kombora lake ni mwezi Septemba, Wakati huo, kombora lake la mwisho lilikuwa la sita la nguvu za kinyuklia mwezi huo.

Korea Kaskazini imeendeleza mpango wake wa kinyuklia pamoja na ule wa utengenezaji wa makombora licha ya shutuma kutoka kwa jamii ya kimataifa.

KIMENUKA TENA NYUMBANI KWA PLATINUM


Zarinah Hassan ‘Zari The BossyLady’

Mipasho! Mwanamitindo mjasiriamali, Zarinah Hassan ‘Zari The BossyLady’ ambaye aliingia katika mtafaruku wa maisha yake ya kimapenzi, kwa mara nyingine juzikati alionyesha kuwepo kwa kutoelewana kwao baada ya kuliamsha dude kwa kutoa maneno ya kumnanga mzazi mwenzake.

Awali, vyanzo vyetu vilivyo karibu na mrembo huyo mwenye watoto watano, alisema kwa sasa hana uhusiano mzuri na baba wa watoto wake wawili, kwa kile kinachosemwa kuwa ni kitendo cha mwenzake huyo kuendekeza mapenzi na wanawake wengine.

“Ni kama mchezo unaelekea mwishoni hivi sasa, maana maneno na ugomvi kati yao hauishi, jamaa anafanya kazi kubwa kuficha kuhusu huu uhusiano wake kuwa juu ya mawe, lakini ukweli ni kwamba hakuna dalili za wawili hawa kukaa tena imara kama zamani,” kilisema chanzo hicho.

Katika tukio la hivi karibuni, mwanamama huyo aliandika katika mtandao wake maneno yenye kumlenga mzazi mwenzake, akisema anaendekeza wanawake na watoto wengi na kwamba badala ya kuona anauza kazi zake nyingi za muziki, yeye amekuwa hodari wa eneo ambalo hahusiki.

Katika kumnanga huko, Zari alisema endapo mtu anatafuta ubalozi wa kondom, ambacho ni kifaa cha kinga dhidi ya magonjwa ya kuambukizwa kupitia ufanyaji mapenzi, basi hana haja ya kuhangaika kumpata, kwa kuwa tayari mtu.

TASWIRA YA MAGAZETI YA LWO TAREHE 29/11/2017

MKUU WA MKOA MOROGORO APATA AJALI

Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Dk Steven Kebwe 

Morogoro. Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Dk Steven Kebwe amepata ajali katikati ya Hifadhi ya Taifa ya Mikumi iliyopo wilayani Kilosa mkoani hapa.

Ajali hiyo ilitokea saa saba usiku wa kuamkia leo Jumatano ambapo inadaiwa gari la mkuu huyo wa mkoa lilimgonga mnyama aina ya Nyati na gari hilo kuharibika vibaya.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Urlich Matei amethibitisha kutokea kwa ajali hiyo na kueleza kuwa taarifa kamili ataitoa mara baada ya kukamilika.

Inadaiwa kuwa ndani ya gari hilo mbali na kuwepo mkuu wa mkoa pia aliambatana na mlinzi wake ambao wote kwa pamoja walitoka salama.

Mwandishi wa Mwananchi alifanya juhudi za kumtafuta mkuu wa mkoa kwa njia ya simu ili kuzungumza naye juu ya ajali hiyo lakini simu yake iliita bila kupokelewa

HATUTA WAVUMILIA WENYE TAMAA NA FEDHA ZA UKIMWI




WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amesema serikali haitawavumilia wote, wanaotumia vibaya fedha za serikali, ambazo zinapaswa kuleta maendeleo kwa wananchi zikiwemo za Mfuko wa Udhibiti Ukimwi.
Majaliwa alisema Dar es Salaam jana wakati akifungua kongamano la Kitaifa la Maadhimisho ya Siku ya Ukimwi Duniani 2017, kaulimbiu ikiwa ‘Changia Mfuko wa Udhamini wa Udhibiti Ukimwi, Okoa Maisha.”
Alisema wito wake ni kuhakikisha bodi ya mfuko huo, inasimamia vizuri fedha hizo zinazochangiwa na wadau mbalimbali ili kuwahakikishia usalama wake. “Fedha hizi zikitumika vinginevyo hatutavumiliana. Malengo ni kuhakikisha fedha hizo zinazotolewa na wadau zinatumika kama ambavyo imekusudiwa,” alisema Majaliwa.
Alisema anayo furaha kuwa Mfuko huo wa Udhibiti Ukimwi umeanza kufanya kazi, ambapo Oktoba 21, mwaka huu kwa mara ya kwanza Mfuko huo uligawa fedha kwa ajili ya shughuli za kudhibiti ukimwi nchini Sh. milioni 660, zilitolewa kwa Wizara ya Afya kwa ajili ya kununua dawa za Cotrimoxazole ambazo hutumika kutibu na kuzuia magonjwa nyemelezi kwa watu waishio na virusi vya Ukimwi.
“Aidha kiasi cha Shilingi milioni 200 zilitolewa kwa Mkoa wa Manyara kwa ajili ya kuchangia ujenzi wa Kituo cha Afya Mererani, ambacho licha ya kutoa huduma nyingine za afya, kitatumika kutoa huduma za dawa za kufubaza VVU kwa watu waishio na virusi vya Ukimwi,” alisema.
Alisema serikali itaendelea kutenga fedha za mfuko huo na kuhakikisha inahamasisha wananchi na wadau, ikiwemo sekta binafsi kuchangia mfuko huo muhimu. Alisema Serikali ya Awamu ya Tano imedhamiria kujenga Tanzania ya viwanda na ili ifikie lengo hilo ni lazima wananchi wawe na afya bora.
“Nguvu kazi kwa ajili Tanzania ya viwanda itatokana na wananchi wenye nguvu na afya bora. Hivyo serikali tutahakikisha tunaendelea kutoa huduma bora za afya ili wananchi wetu waweze kuwa na afya bora,” alisema.
Alisema watu milioni 16 ya Watanzania wote ni vijana na wanapaswa kukingwa dhidi ya magonjwa mbalimbali ikiwemo Ukimwi ili taifa liwe na nguvu kazi ya kutosha hasa kipindi hiki linapoanza mageuzi makubwa ya kiuchumi na kimaendeleo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Tume ya Kudhibiti Ukimwi Tanzania (Tacaids), Dk Leonard Maboko alisema kongamano hilo ni sehemu ya shughuli za Maadhimisho ya Siku ya Ukimwi duniani, itakayofanyika Desemba mosi hapa nchini.
Alisema maonesho ya maandalizi hayo yalianza Jumamosi, yakijumuisha huduma mbalimbali za utoaji elimu na burudani kwa wananchi ikiwemo ushauri nasaha na upimaji wa hiari wa VVU.
Alisema pia kuwa tayari wamezindua mkakati wa kitaifa wa kondomu wa miaka mitatu wa 2016 hadi 2018, na siku ya kilele cha maadhimisho hayo kutakuwa na uzinduzi wa Ripoti ya Utafiti wa Kitaifa wa Matokeo ya Ukimwi wa Mwaka 2016/17.

MEYA WA CHADEMA IRINGA APANDISHWA KIZIMBANI




MEYA wa Manispaa ya Iringa, Alex Kimbe na wafuasi wenzake watano wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), wamepandishwa kizimbani mjini Iringa, kujibu mashitaka yanayohusishwa na vurugu za uchaguzi mdogo wa udiwani Kata ya Kitwiru, Iringa mjini.
Wakati Meya huyo aliachiwa jana kwa dhamana na Mahakama ya Wilaya Iringa, baada ya kusota rumande kwa siku tatu, Mahakama ya Hakimu Mkazi Iringa iliwanyima dhamana wafuasi hao watano kwa kuwa kati ya makosa matatu, wanayotuhumiwa kuyafanya kosa moja halidhaminiki.
Mwendesha Mashtaka wa Polisi, Aristeck Mwinyikheri alisema Kimbe aliyefikishwa mahakamani hapo kwa kesi Namba 189 ya mwaka 2017, anashitakiwa kutishia kumuua mtu kwa bastola katika tukio la Novemba 26, mwaka huu katika Kata ya Kitwiru mjini Iringa, wakati shughuli ya uchaguzi mdogo wa udiwani wa kata hiyo ikiendelea.
Mwinyikheri alisema Meya huyo alitenda kosa hilo kwa Alphonce Muyinga, ambaye ni Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM), kinyume na Kifungu Namba 89 (2) (a) cha Kanuni za Adhabu.
Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Wilaya ya Iringa, John Mpitanjia alisema shauri hilo litarudi tena mahakamani hapo Desemba 12, mwaka huu. Wakati huohuo, Mahakama ya Hakimu Mkazi Iringa imewanyima dhamana Martha Robert, Leonard Kulijira, Esau Bwire, Christopher Jevas na Samwel Nyanda, wafuasi wa Chadema ambao kwa pamoja wameshitakiwa mahakamani kupitia kesi namba 190 ya mwaka 2017 kwa makosa matatu.
Mbele ya hakimu mkazi wa Mahakama hiyo, Richard Kasele , Mwendesha Mashitaka wa Mahakama hiyo Chakila Felix alisema washitakiwa hao wafuasi wa Chadema, wanatuhumiwa kujeruhi, kuteka na kufanya unyang’anyi kwa kutumia nguvu.
Felix alisema watuhumiwa hao wanatuhumiwa kumjeruhi Dick Frank na kumnyang’anya simu yake ya mkononi. Mahakama hiyo imewarudisha rumande washitakiwa hao baada ya kunyimwa dhamana kwa kuwa kosa la unyang’anyi kwa kutumia nguvu, halina dhamana na shauri lao litarudi tena mahakamani hapo Desemba 12, mwaka huu.

MABALOZI KUPANDA MLIMA KILIMANJARO

KATIKA kuendeleza juhudi za kutangaza vivutio vya utalii nchini, mabalozi tisa kati yao wanane Watanzania na mmoja Balozi wa Algeria nchini Qatar, wanapanda mlima Kilimanjaro leo, ikiwa ni sehemu ya jitihada za Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) katika kuvitangaza vivutio vya nchi yetu, ukiwemo Mlima Kilimanjaro.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini Moshi, Ofisa Habari Mkuu wa TTB, Geoffrey Tengeneza alisema wameandaa ziara hiyo ya mabalozi kwa lengo la kuwajengea uwezo na wigo mpana wa kuvitangaza vivutio vya utalii katika nchi watakazokwenda kuhudumia kama mabalozi. “Maandalizi yamekamilika na tunatarajia mabalozi na wafanyakazi wa Bodi ya Utalii na mjumbe kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na waandishi wa kutoka Clouds Media Group watapanda mlima Kilimanjaro kesho (leo),” alisema Tengeneza.
Mabalozi hao wanaopanda Mlima Kilimanjaro leo ni Balozi Aziz Mlima, Balozi Samwel Shelukindo, Balozi Luteni Jenerali Wynjones Kisamba, Balozi Pastor Ngaiza, Balozi Bernard Achiula, Balozi Alan Mzengi na Balozi Antony Cheche. Pia yumo Balozi wa Algeria nchini Qatar, Abdelaziz Sebaa.
Tengeneza alisema katika kupanda mlima huo mrefu kuliko wote barani Afrika, kuna vivutio vingi watakutana navyo hivyo kuwafanya kuwa na vitu vingi vya kusimulia kama vielelezo watakapokuwa katika maeneo yao ya kazi na kuwa mabalozi wa kutangaza vivutio vya utalii ukiwemo Mlima Kilimanjaro kwa vitendo.
“Ni matumaini yetu kuwa watakwenda kuitangaza Tanzania pamoja na vivutio vyake katika nchi za nje na kufanya ongezeko la watalii kuja nchini kuongeza maradufu,” alifafanua Tengeneza. Alisema kupitia ziara hiyo, mabalozi watakwenda kutekeleza kwa vitendo Diplomasia ya Uchumi kwa kuvitangaza vivutio vya utalii vilivyopo Tanzania na ukarimu wa Watanzania kwa wageni.
“Kama Bodi ya Utalii tunatoa wito kwa mabalozi wengine wanaoiwakilisha Tanzania katika nchi nyingine duniani kutumia nafasi hiyo katika kuvitangaza vivutio hasa Mlima Kilimanjaro ambao ndio mlima mrefu barani Afrika,” alieleza ofisa huyo wa TTB.
Kwa upande wake, Balozi wa Algeria nchini Qatar, Abdelaziz Sebaa ambaye pia ni Mwenyekiti wa Mabalozi nchini humo, alisema hiyo ni nafasi ya pekee kwake kupanda Mlima Kilimanjaro na kujionea vivutio vingine vya utalii Tanzania.
Alisema kwa nafasi hiyo na vitu atakavyokwenda kuviona, atakwenda kuwahamasisha mabalozi wengine katika umoja wao ili kuvitangaza vivutio vilivyopo Tanzania, hivyo kusaidia kujenga uhusiano mzuri zaidi katika sekta ya utalii. Ziara hiyo ya mabalozi kupanda Mlima Kilimanjaro, imeratibiwa na TTB na katika kupanda mlima huo, wataongozwa na Kampuni ya ZARA Tours iliyopo mjini Moshi.

MSIGWA ASEMA NA POLISI

Related imageMbunge wa Iringa Mjini, Peter Msigwa ametupa jiwe gizani kwa wapinzani wao wa kisiasa kwamba wamewashinda kwa hoja zote za kisiasa na wameshindwa kuzijibu hivyo anawashangaa kushangilia ushindi.
 
Msigwa amesema kwamba wapinzani  wao lazima watawashinda kama watatumia vyombo vya usalama na siyo kwa hoja na kwamba wao Chadema wakitoa hoja wao wamekuwa wakishindwa kuzijibu.

Msigwa kupitia ukurasa wake wa Twiter ameandika kwamba "Hatuna mafunzo ya kipolisi wala kijeshi! Mkitumia vyombo vya usalama lazima mtatushinda , lakini tumewashinda HOJA zote za kisiasa! Mmeshindwa kuzijibu! Eti unashangilia Ushindi! Huu ni uporaji" Msigwa

Chama cha upinzani CHADEMA kimekuwa kikilalamikia chama tawala kutumia vyombo vya dola katika kuwakandamiza.

TAMKO LA ACT KWA SERIKALI YA AWAMU YA TANO

CHAMA cha ACT-Wazalendo kimeainisha mambo tisa ambayo Serikali ya awamu ya tano  imefanya vibaya katika miaka miwili ya uongozi wa Rais John Magufuli.
Mwenyekiti wa chama hicho, Yeremia Maganja, akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam amesema  mambo hayo yamegawanywa katika mafungu makuu matatu.

“Leo tutatoa tathmini yetu ya miaka miwili ya utawala huu, tathmini hii ni zao la utafiti husika uliofanyika nchi nzima. Tathmini yetu itaainisha mambo 9 ambayo tunaamini hayakufanywa vizuri kabisa na Serikali,” amesema Maganja.

“ACT Wazalendo inao wajibu wa kujihusisha na masuala ya watu, tunatimiza wajibu huo kwa tathmini hii ya kuangazia mambo haya risa ambayo ni mapungufu ndani ya miaka miwili hii ya utawala huu,”ameongeza.

Amesema mambo hayo yamefanya vibaya kiasi cha kuleta athari nchini, kisiasa, kiutawala na kiuchumi.

Ametaja maeneo hayo kuwa ni ya, Haki za Msingi  Usimamizi wa Uchumi na Uendeshaji wa Nchi.

Haki za Msingi 
Maganja amesema  kumekuwepo na uminywaji wa uhuru wa Vyama vya Siasa Kufanya mikutano ya hadhara, uhuru wa Vyombo vya habari, pamoja na Uhuru wa Kujieleza, Kuminywa kwa haki ya wazanzibari kuchagua viongozi wao na Kupuuzwa kwa matakwa ya Katiba Mpya.


Usimamizi wa Uchumi wa Nchi

Amesema kumekuwepo kwa hali ya Kusinyaa kwa Uchumi wa Nchi, Kudhohofishwa kwa Sekta Binafsi,  Mazingira Mabaya ya Biashara Nchini, pamoja Kupaa kwa Deni la Taif.

Mengine ni kutelekezwa kwa kilimo na utekelezaji wa miradi mikubwa bila kuzingatia maslahi ya umma.

Uendeshaji wa nchi

Mwenyekiti huyo amesema katika kipengele hiki serikali hii imefanya vibaya kwa uvunjaji wa misingi ya Sera ya Mambo ya Nje, unyanyasaji wa watumishi wa umma na utawala unaovunja taasisi za kikatiba na kisheria kutoakana na kwamba utawala huu umekuwa wa mtu mmoja.

NYARANDU AIKIMBIA CCM NA KUACHIA JIMBO LA SINGIDA MASHARIKI

Image result for NYALANDU

Nimeamua kujiuzulu nafasi yangu ya Ujumbe wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi CCM, pamoja na nafasi zote za Uongozi ndani ya Chama kuanzia leo, Oktoba 30, 2017, halikadhalika asubuhi ya leo nimemwandikia Spika wa Bunge, Mh. Job Ndugai, barua ya kujiuzulu nafasi yangu ya Ubunge wa Jimbo la Singida Kaskazini kupitia tiketi ya CCM, nafasi ambayo nimeitumikia kwa vipindi vinne mfululizo tangu nilipochaguliwa kwa mara ya kwanza mnamo mwaka 2000 hadi Sasa.

Aidha, Nimechukua uamuzi huo kutokana na kutorishwa kwangu na mwenendo wa hali ya Kisiasa nchini, ikiwa ni pamoja na ukiukwaji wa haki za kibinadamu, ongezeko la vitendo vya dhuluma wanavyofanyiwa baadhi ya watanzania wenzetu, na kutokuwepo kwa mipaka ya wazi kati ya Mihimili ya dola (Serikali, Bunge, na Mahakama) kunakofanya utendaji kazi wa Kibunge wa Kutunga Sheria na wa Kuisimamia Serikali kutokuwa na uhuru uliainishwa na kuwekwa bayana kikatiba.

vilevile, Naamini kwamba bila Tanzania kupata Katiba Mpya Sasa, hakuna namna yeyote ya kuifanya mihimili ya dola isiingiliane na kuwepo kwa ukomo wa wazi na kujitegemea kwa dhahiri kwa mihimili ya Serikali, Bunge na mahakama ambayo ndio chimbuko la Uongozi Bora wa nchi, na kuonesha kwa uwazi kuwa madaraka yote yatokana na wananchi wenyewe, na kwamba Serikali ni ya Watu kwajili ya Watu.

Mimi Naondoka na kukiacha Chama Cha Mapinduzi CCM, nikiwa nimekitumikia kuanzia ngazi ya Uenyekiti wa UVCCM Mkoa, Ujumbe wa Kamati za Siasa Wilaya na Mkoa, Ujumbe wa Kamati ya Wabunge Wote wa CCM na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM TAIFA,  kwani nimejiridhisha kuwa kwa mwenendo wa hali ya kisiasa, kiuongozi na kiuchumi uliyopo Tanzania Sasa, CCM imepoteza mwelekeo wake wa kuisimamia Serikali kama ilivyokuwa hapo awali. Aidha, Naamini kuwa, kama ilivyotokea kwa mihimili ya Bunge na Mahakama kutokuwa na uhuru kamili, bila kuingiliwa kiutendaji kwa namna Moja au nyigine, CCM nayo imekuwa Chini ya miguu ya dola badala ya chama kushika hatamu na kuikosoa Serikali inapobidi kama yalivyokuwa maono ya Baba wa Taifa mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

Hivyo basi, kwa dhamira yangu, na kwa uamuzi wangu mwenyewe, nikiwa na haki ya kikatiba, natangaza kikuhama Chama Cha Mapinduzi CCM leo hii, na nitaomba ikiwapendeza wanachama wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA, basi waniruhusu kuingia mlangoni mwao, niwe mwanachama, ili kuungana na CHADEMA na watanzania wote wanaopenda kuleta mabadiliko ya kisiasa na kiuchumi nchini kwa kupitia mfumo wa ki demokrasia na uhuru wa mawazo.

vilevile, nimemua kujiuzulu kiti Cha Ubunge, Jimbo la Singida Kaskazini kuruhusu kufanyika kwa uchaguzi mwingine ili wananchi wapate fursa ya kuchagua itikadiwanayoona inawafaa kwa majira na nyakati hizi zenye changamoto lukuki nchini Tanzania.
Ni imani yangu, kamwe hayatakuwa ya bure maneno haya, wala uamuzi huu niufanyao mbele ya Watanzania leo ili kwamba, sote kama TAIFA tuingie kwenye mjadala wa kuijenga upya misingi ya nchi yetu. Ni maombi yangu kwa MUNGU kuwa Haki itamalaki Tanzania.Upendo, amani na mshikamano  wa watu wa imani zote za dini, mitazamo yote ya kiitikadi za Kisiasa, na makabila yote nchini uimarike. Tushindane ki sera na kuruhusu tofauti za mawazo, lakini tubaki kama ndugu, na Taifa lililo imara na nchi yenye Adili.

                                             mungu awabariki wote

                                                                   LAZARO NYARANDU