TANZANIA imesema haiwezi kutegemea ushuru wa forodha pekee kulinda bidhaa za ndani, hivyo ubora ni jambo la msingi ili ziweze kumudu ushindani wa kibiashara ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).
Kwa mujibu wa taarifa ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, kwa kuwa Tanzania ni mwanachama wa EAC na SADC, takribani nchi 22 zina haki ya kuingiza bidhaa nchini bila ukomo na bila kutozwa ushuru wa forodha.
Waziri mwenye dhamana na wizara hiyo, Charles Mwijage amesema, ili Tanzania ifanikwe kwenye masoko ya kimataifa na kufikia lengo la kuwa nchi yenye uchumi wa kati wa viwanda, inapaswa kuingiza matumizi ya viwango katika nyanja zote za uzalishaji, biashara na utoaji huduma.
Alisema, ingawa matumizi ya viwango nchini si ya kiwango cha juu kulinganisha na kasi ya kimataifa, Shirika la Viwango Tanzania (TBS) limetayarisha viwango vya kitaifa kwa lengo la kuchochea ukuaji uchumi na maendeleo ya jamii.
TBS ni miongoni mwa mashirika 162 ya viwango duniani ambayo ni wanachama wa Shirika la Viwango la Kimataifa (ISO). Hata hivyo, Mkurugenzi Mkuu wa TBS, Profesa Egid Mubofu amesema, utayarishaji wa viwango vya kitaifa unazingatia Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025, ambayo pamoja na mambo mengine inataka hadi kufikia mwaka 2025 Tanzania iwe nchi ya uchumi wa kati wa viwanda na kiwango kikubwa cha maendeleo ya watu.
Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji anayeshughulikia viwanda na biashara, Profesa Adolf Mkenda amesema, mbali na TBS viwango pia vinatazamwa na Tume ya Ushindani (FCC) na mamlaka nyingine za udhibiti na usimamizi ikiwemo Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) wanapaswa kuhakikisha Tanzania inatekeleza kikamilifu azma ya kujenga uchumi wa viwanda.
FCC ni chombo huru cha serikali kilichoanzishwa kwa Sheria ya Bunge Namba 8 ya Mwaka 2003 ili kuhamasisha usawa kwenye ushindani wa kibishara sanjari na kumlinda mlaji na mtumiaji wa bidhaa.
Aidha TFDA ni wakala wa Serikali chini ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia , Wazee na Watoto wenye wajibu wa kusimamia ubora na usalama wa chakula, dawa, vipodozi na vifaa tiba ili kulinda afya za wananchi.
Ilianzishwa kupitia kifungu 4(1) cha Sheria ya Chakula, Dawa na Vipodozi, na ilianza kazi rasmi Julai Mosi, 2003. Alisema, shughuli za mamlaka hizo ni muhimu zaidi wakati huu kwa sababu Serikali, kupitia Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano, imeamua kujenga uchumi wa viwanda.
Alisema, ili kuuza bidhaa kwenye soko la dunia, suala la usalama na ubora ni lazima lizingatiwe kwa kiwango cha juu. Profesa Mkenda alisema, kama bidhaa za viwandani nchini hazitakidhi viwango vya ubora na usalama, wananchi wataendelea kupenda bidhaa zinazoagizwa kutoka nje ya nchi hivyo kudhoofisha uzalishaji wa ndani.
Profesa Mkenda alisema pia kwamba, kuna haja ya kuzuia uingizwaji wa bidhaa zisizo na viwango na bidhaa bandia kutoka nje ya nchi kwa kuwa zitaleta ushindani usio wa haki kwa wazalishaji wa ndani.
“Bidhaa hizi zisizo na viwango na zile bandia zinapoingia nchini zinadhoofisha sana uzalishaji wa ndani kwa kuleta ushindani usio wa haki na kudhulumu walaji. Lazima tukubali kwamba bidhaa bora, salama na zisizo bandia kutoka nje zitaendelea kuingia nchini.
Baadhi ya bidhaa hizo zitatoka nchi za Jumuiya ya Afrika ya Mashariki na nchi za SADC, na hivyo zitaingia nchini bila kutozwa ushuru wa forodha na bila kuwekewa ukomo”alisema.
Alisema, uzalishaji wa ndani lazima ukukidhi viwango vya kimataifa, hivyo mamlaka za udhibiti na usimamizi zina wajibu wa kufanikisha hilo ili bidha za Tanzania zihimili ushindani ndani na kwenye masoko ya nje.
“Lazima tukubali kuwa ushindani wa haki ni jambo jema. Ushindani wa haki humnufaisha mlaji kwa kumpa bidhaa bora na salama kwa bei ahueni. Ushindani pia hulazimisha wazalishaji wengine kuacha kubweteka na badala yake kuongeza ubunifu na ubora wa bidhaa zao.
Kwa maana hiyo ushindani ni jambo bora sana” alisema Profesa Mkenda. Mkurugenzi wa Udhibiti Ubora wa TBS, Mhandisi Tumaini Mtitu amesema, bidhaa zisizo na viwango vya ubora husababisha ushindani usio sawa katika soko, zinadhuru afya za walaji au watumiaji wa bidhaa na huchafua mazingira kwa namna tofauti.
“Nembo ya ubora ya TBS ndiyo inayopaswa kutumika kuonesha kuwa bidhaa hii au ile imethibitishwa ubora kwa sababu inatolewa na shirika lenye dhamana ya kudhibiti ubora wa huduma na bidhaa zinazozalishwa na viwanda vya ndani na ndilo linaloviandaa viwango hivyo kwa ngazi ya taifa” alisema Mtitu. Alisema, hata bidhaa zinazoingizwa katika soko la ndani kutoka nje ya Tanzania hukaguliwa ubora ili kujiridhisha kuwa zinakidhi viwango vya kimataifa.