SHIRIKA la Umeme Tanzania (TANESCO), limesema, tayari asilimia 95 ya uboreshaji miradi ya umeme katika jiji la Dar es Salaam, imekamilika.
Meneja Mwandamizi wa TANESCO Kanda ya Dar es Salaam na Pwani, Mhandisi, Mahende Mgaya, (pichani juu), amewaambia waandishi wa habari ofisini kwake jijini Dar es Salaam leo Septemba 27, 2017 na kwamba ifikapo Desemba mwaka huu wa 2017, wananchi na wakazi wa Dar es Salaam wataona ile hali ya kukatika kwa umeme, mara kwa mara imebadilika.
“Tulikuwa na jumla ya miradi mipya 18 ya kuboresha vituo vya umeme jijini Dar es Salaam ili viweze kutoa umeme wa kutosha na wa uhakika, hadi sasa, vituo vinane vimekamilika kabisa na vinafanya kazi, vimebaki vituo 10 ambavyo navyo viko katika hatua za mwisho za kukamilika, na ifikapo Desemba, 2017 vituo vyote 18 vitakuwa vinafanya akzi.” Alitoa hakikisho Mhandisi Mgaya.
Alisema, kufuatia kuongezeka kwa shughuli za kiuchumi na idadi ya watu jijini Dar es Salaam, mahitaji ya nishati ya umeme nayo yameongezeka na hivyo Serikali kupitia Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), iliamua kuchukua hatua za haraka kuboresha vituo vyake vya umeme ikiwa ni pamoja na kujenga vipya ili kukidhi mahitaji halisi ya umeme.
“Wafadhili kama vile Benki ya Maendeleo ya Afrika, (AfDB, World Bank, Finland, na Japan), walijitokeza na kufadhili miradi hiyo.”Alifafanua.
Kazi hiyo ya kuboresha vituo hivyo ambavyo ni pamoja na Mbagala, Kurasini, Kigamboni, Ilala Mchikichini, Kisutu, Mikocheni, Gongolamboto, na maeneo mengine imekuwa ikifanyika tangu miaka miwili iliyopita lakini kutokana na matatizo ya hapa na pale, ikiwa ni pamoja na mapingamizi ya wananchi kuzuia utekelezaji wa miradi hiyo, na wakandarasi, kumepelekea ucheleweshaji.
Maeneeo ambayo yamekuwa yakiathirika zaidi na hali hiyo ya kukatika kwa umeme mara kwa mara ni pamoja na Wilaya ya Temeke, Kigamboni, Ubungo na baadhi ya maeneo ya wilaya ya Kinodnoni.
“Nichukue fursa hii kuwaomba radhi wananchi, hususan wateja wetu, kutokana na hali hii ya kukatika kwa umeme, lakini napenda pia waelewe kuwa hali hiyo inatokana na kazi ambayo tumekuwa tukiifanya, na mara nyingi umeme tunakata siku za weekend, kwa vile shunguli nyingi za kiofisi zinakuwa zimepungua na hivyo inakuwa fursa nzuri kwetu kufanya kazi.” Alifafanua Mhandisi Mgaya.
Alisema, wananchi wanataka umeme, tena ulio bora na wa uhakika, ndio maana TANSCO imeamua kuchukua hatua madhubuti za kuboresha na kujenga vituo vipya vya kupoza na kusambaza umeme ikiwa ni pamoja na kujenga lini mpya za kusafirisha umeme.
“Hatu hizi zote lazima ziwe na changamoto za hapa na pale, lakini kwa kiasi kikubwa TANESCO inaelekea kulitatua tatizo hilo la umeme jijini Dares Salaam na Mkuranga.”. Alisisitiza.
Wakandarasi na mafundi wa TANESCO wakiwa kazini
Moja ya vituo ambavyo vimefungwa mitambo mipya ili kuboresha upatikanaji wa umeme jijini Dar es Salaam.
Kituo cha kupoza na kusambaza umeme cha Kisutu.