RAIS John Magufuli amesema Tanzania ilikuwa inapoteza mapato mengi kutokana na udhaifu wa Sheria za Kodi na usimamizi wake, hivyo ili kuziba mianya hiyo, amemteua mtaalamu aliyebobea katika sheria za kodi kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa Florens Luoga kuwa gavana mpya wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT).
Profesa Luoga ambaye pia ni Naibu Makamu Mkuu wa Chuo wa UDSM anayeshughulikia Taaluma, atamrithi Profesa Benno Ndullu anayetarajiwa kustaafu rasmi utumishi wa umma ndani ya miezi mitatu kuanzia sasa.
Aliyasema hayo Ikulu, Dar es Salaam jana wakati akiwapongeza Wajumbe wa Kamati mbili zilizohusika katika kujadiliana na Kampuni ya uchimbaji dhahabu ya Barrick kuhusu mkataba mpya wa uchimbaji unaozingatia maslahi sawa ya faida.
Alisema nchi imekuwa ikipoteza fedha nyingi kutokana na wawekezaji kukwepa kodi kwa kuweka fedha zao katika nchi zisizotoza kodi kutokana na sheria ya mwaka 1992 kuhusu uwekaji fedha nchini kutosimamiwa vyema na BoT kutokazia sheria za kodi. Katika kuonesha msisitizo kuwa sasa anataka sheria za kodi zifuatwe, alitangaza kumteua Profesa Luoga ili akasimamie sheria za kodi kwa ukamilifu.
Alisema watu wengi huenda wakashangaa kwa nini amemteua mwanasheria kuwa gavana kinyume na ilivyozoeleka na wengi kuwa mchumi ndiye huwa gavana, lakini amefanya hivyo kwa sababu tatizo la BoT limekuwa kutosimamia sheria za kodi.
Rais alisema Profesa Luoga atasaidiwa na manaibu magavana wenye taaluma ya uchumi na fani nyingine, hivyo anaamini atamudu nafasi hiyo itakayoachwa wazi na Profesa Ndulu ambaye amemsifu kuwa amefanya kazi nzuri na atastaafu Januari.
Ndullu ambaye amekuwa Gavana wa BoT tangu mwaka 2008 anatarajiwa kumaliza muda wake wa kuiongoza taasisi hiyo Januari mwakani. Rais Magufuli akizungumza baada ya kutoa vyeti hivyo alisema atamteua gavana kutoka baadhi ya wajumbe wa kamati ya mashauriano kuhusu madini kutokana na kuridhishwa na kazi yao.
Huo ni uteuzi wa pili kwa Profesa Luoga, kwani Julai 11 mwaka huu Rais Magufuli alimteua kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Mamlaka ya Mapato ya Tanzania (TRA).
Profesa Luoga ambaye pia ni Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) anayeshughulikia Taaluma, alichukua nafasi ya Bernard Mchomvu ambaye bodi yake ilivunjwa na uteuzi wake kutenguliwa na Rais Magufuli.
Kuteuliwa kwa Profesa Luoga kutamfanya kuwa Gavana wa saba wa BoT tangu ilipoanza kazi Juni 14, mwaka 1966, ikiwa ni mwaka mmoja baada ya kuundwa kwa Sheria ya Benki ya Tanzania mwaka 1965.
Gavana wa kwanza alikuwa Edwin Mtei aliyeiongoza BoT hadi mwaka 1974 na nafasi yake kuchukuliwa na Charles Nyirabu aliyeongoza hadi mwaka 1989. Kuanzia mwaka 1989-1993, BoT iliongozwa na Gilman Rutihinda aliyemwachia Dk Idris Rashidi aliyedumu hadi mwaka 1998. Kuanzia mwaka huo, iliongozwa na Dk Daudi Ballali.
Na kuanzia Januari 8, mwaka 2008 BoT ilikuwa chini ya Profesa Ndulu. MAJUKUMU BOT Ikiwa ni benki ya kitaifa inayosimamia masuala ya kibenki na kifedha nchini Tanzania, miongoni mwa majukumu yake ni utoaji wa fedha za Tanzania, Shilingi ya Tanzania.
Imepewa pia majukumu mbalimbali yanayohusiana na usimamizi wa fedha nchini, yakiwemo; kuhakikisha uwepo wa akiba ya fedha za kigeni kwa lengo la kusaidia kuimarisha uchumi, na akiba hiyo kutumika wakati wa mkwamo wa kiuchumi nchini.
Aidha, ina jukumu la kchochea ukuaji wa soko la fedha nchini, kulinda na kuendeleza taasisi za kifedha zinazosimamiwa vema, lakini pia jukumu jingine ni kuhakikisha uwiano imara kati ya fedha ya Tanzania na pesa za kigeni.
ASISITIZA KODI, AKERWA
Aidha, Rais Magufuli alisema Serikali yake inawapenda wafanyabiashara na akawataka wafanyabiashara wazawa kuchangamkia fursa mbalimbali za kiuchumi zilizopo nchini hivi sasa, lakini akawataka walipe kodi ili nchi ipate fedha za kuendesha miradi yake mbalimbali.
Alisema nchi hivi sasa inakusanya mapato mengi inayoyatumia kutekeleza miradi yake kinyume na upotoshaji mkubwa unaofanywa na baadhi ya watu, wasomi na wanasiasa ambao wanaobeza kazi zinazofanywa na Serikali wakidai takwimu za uchumi ambazo Serikali inadai makusanyo yake yanapanda, ni za kupikwa na haziakisi uhalisia.
“Utakuta mtu anasema makusanyo yameshuka, hivi kama makusanyo yangeshuka tungeweza kujenga reli ya kisasa kwa gharama ya Shilingi trilioni 7 kutoka Dar es Salaam hadi Dodoma yenye urefu wa Kilomita 726?
Serikali ambayo haina mapato inaweza kununua ndege sita mpya kwa mpigo?” “Kama hatukusanyi mapato tungetangaza zabuni ya mradi wa kuzalisha umeme wa Stiegler’s Gorge ambao utazalisha Megawati 2,100? au kuongeza bajeti ya afya kutoka Shilingi bilioni 31 hadi Shilingi bilioni 269?
Kama huna pesa utatangazaje zabuni ya ununuzi wa meli mpya Ziwa Victoria au kusambaza umeme kwenye vijiji 4,000?,” alihoji Rais Magufuli. Alielezea kusikitishwa na taarifa iliyochapishwa na Gazeti la Tanzania Daima la juzi kuwa asilimia 67 ya Watanzania wanatumia dawa za kupunguza makali ya virusi vya Ukimwi (ARV’s).
Alisema upotoshaji wa aina hiyo una madhara makubwa kwa taifa kwa kuwa wawekezaji hawawezi kuja kuwekeza kwenye taifa la watu wagonjwa. Alisema lengo la watu wanaopotosha taarifa za serikali ni kutaka kuwatoa wananchi kutoka kwenye mjadala wa maendeleo ya nchi ili waanze kujadili matatizo ya watu hao.
Hivyo ameagiza Sheria ya Takwimu ya Mwaka 2015 ianze kutumika dhidi ya watu wanaopotosha takwimu za serikali. ATUNUKU VYETI Kwa kuthamini uzalendo, mchango na kazi ngumu iliyofanywa na kamati alizoziunda za kuchunguza biashara ya madini nchini, Rais Magufuli aliwatunuku vyeti vya shukrani na pongezi wajumbe 28 wa kamati hizo.
Alisema wajumbe hao walijitolea maisha yao kwa kufanya kazi hatari ya kumnyang’anya mtu mabilioni. Alisema wakati wanaanza kufuatilia suala la madini, walijua ni aina gani ya watu wanaoshughulika nao.
“Mimi mwenyewe nilipata mtikisiko, lakini nikasema niko kwa ajili ya Watanzania na ninachokifanya ni kwa faida yao. Walipogundua tuna taarifa zao zote za mawasiliano waliyokuwa wakiyafanya, akaunti zao za nje na kila kibaya walichofanya, waliamua kuja haraka kwenye mazungumzo, tulikuwa na ushahidi wote, walikuja kwanza nane, baadaye wakaongezeka wakafika 14 na baadaye 30, hii inaonesha dozi tulizokuwa tukiwapa ziliwatosha,” alieleza Rais Magufuli.
Alisema vyeti alivyowatunuku ni kumbukumbu ya maisha yao kwa kuwa wamewawakilisha Watanzania vizuri na wameonesha uzalendo wa kweli kwa taifa. Alitaka dhana ya uzalendo kwa nchi iendelee kuimarishwa kwa kuwa wajumbe wa kamati hizo wameonesha wao ni Watanzania wa kweli.
VIONGOZI WA DINI, WANASIASA
Akizungumza kwa niaba ya viongozi wa dini, Mufti Mkuu wa Tanzania Shehe Abubakar Zuberi, alimtaka Rais Magufuli asiogope lawama, aendelee kuwatumikia Watanzania. Alisema hata Mungu analaumiwa, mitume walilaumiwa, watu wema wanalaumiwa, hivyo Rais asikate tamaa, athamini anachokifanya kwa ajili ya taifa kwa kuwa yeye ni lulu kwa Watanzania.
Mwenyekiti wa Taifa wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba aliyeongea kwa niaba ya viongozi wa vyama vya siasa alitoa rai kuwa Watanzania watakaoingia kwenye bodi ya pamoja itakayoundwa wajali uzalendo na maslahi ya taifa na wasikubali kudanganywa.
Lipumba ambaye kitaaluma ni mchumi, alisema kwenye mambo yanayohusu maslahi ya taifa, Watanzania lazima wawe wamoja na kuweka kando tofauti za vyama. Alisema wanamshukuru Rais kwa hatua anazochukua za kunusuru rasilimali za taifa kwa kuwa wapinzani walikuwa wakilipigia kelele jambo hilo kwa muda mrefu.
MAJADILIANO YA TANZANITE, ALMASI
Ili kuhakikisha taifa linanufaika na rasilimali za madini, Rais Magufuli alimwagiza Waziri wa Sheria na Katiba, Profesa Palamagamba Kabudi na kamati yake ya majadiliano kuanza mara moja mazungumzo na Kampuni ya Tanzanite One inayochimba madini ya Tanzanite pamoja na kampuni inayochimba almasi.
Naye Waziri Kabudi alimhakikishia Rais Magufuli kuwa atalifanyia kazi agizo hilo mara moja na amenukuu msemo wa watu wa kabila la Waha usemao; “Mchuzi wa mbwa mwitu hunywewa ungali wa moto,” akimaanisha kuwa hatachelewa kulifanyia kazi agizo hilo la Rais.
Waziri wa Madini, Angellah Kairuki alisema Wizara hiyo itadhibiti utoroshwaji wa madini, lakini pia itasimamia utekelezaji wa makubaliano yote yaliyofikiwa ili kuleta tija kwenye sekta ya madini.
Kairuki alisema sekta ya madini inachangia asilimia 4.2 tu kwenye Pato la Taifa kiasi ambacho alisema ni kidogo. Alisema Wizara hiyo itahakikisha madini yanaongezewa thamani kabla ya kuuzwa nje ya nchi, lakini pia wataendelea kushirikiana na wajumbe wa kamati za Rais.
AKAUNTI ZA NJE
Rais Magufuli pia alisema Sheria ya Fedha ya mwaka 1992 inayozuia uwekaji wa fedha nje imekuwa haitumiki, hivyo kusababisha kampuni kufungua akaunti kwenye nchi ambako hawalipi kodi.
Rais alisema pamoja na kuwepo kwa sheria hiyo, BoT ilishindwa kuzuia mambo hayo yasitendeke. Wafanyabiashara wa ndani Ili kuhakikisha Watanzania wanachangamkia fursa za biashara ikiwemo ya madini, Rais Magufuli alikiagiza Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kuwasaidia wanyabiashara waweze kuwekeza kwa uhakika.
Alisema yeye na serikali yake wanawaunga mkono wafanyabiashara na akawataka wautumie muda huu wa uongozi wake vizuri kwa kuwekeza kwenye miradi ikiwemo madini na mafuta.