Baadhi ya polisi wakiwa katika eneo la tukio Ukonga Mazizini wakidumisha ulinzi ili wananchi wasiendelee kuleta vurugu katika eneo hilo.


Kufuatia sintofahamu iliyokuwa inaendelea maeneo ya Mombasa Gongo la Mboto kati ya wananchi na jeshi la polisi na kupelekea baadhi ya raia kujeruhiwa na polisi kwa kile kinachodaiwa kuwa polisi walikuwa wanalipiza kisasi kufuatia kuuawa kwa askari mmoja wa kikosi cha 'Field Force Unit' (FFU)
Mkuu wa Wilaya ya Ilala Sophia Mjema ametembelea eneo hilo na kusikitishwa na kitendo cha jeshi la polisi kuchukua sheria mkononi na kujeruhi watu ambapo ameagiza wote waliohusika kufanya matukio hayo kuchukuliwa hatua za kisheria.

"Nimeambatana na RPC Salum Hamduni hivyo kwa wale walihusika hatua zitachukuliwa, na wale waliojeruhiwa watatibiwa, pia tumewachukua baadhi ya wananchi ambao wamehaidi kutoa ushirikiano hivyo  tutalifanyia uchunguzi na kutenda haki" Alisema DC Mjema.
Mkuu wa wilaya ya Ilala bi. Sophia Mjema akiongea na wananchi wa eneo la Ukonga Mazizini na kusikiliza kero zao baada ya kudai kupigwa na kupokonywa mali zao na watu wanaodhaniwa kuwa ni askari wa FFU.
DC Mjema amewataka wananchi wote walioharibiwa mali zao wajiorodheshe na serikali ya wilaya italifanyia kazi, huku akisisitiza hakukuwa na sababu ya kuchukua sheria mkononi wakati kulikuwa na mbadala wa kulichunguza suala hilo na kulipatia utatuzi.

Mkuu huyo wa wilaya ya ilala amewaomba wananchi watulie na waendelee na shughuli zao kwani hilo siyo jambo kubwa la kupelekea watu wauane na wavuruge amani ya nchi.

Sintofamhamu hiyo imedumu kwa siku tatu kufuatia kifo cha askari wa kikosi cha FFU ambapo inadaiwa aliuawa na wananchi jambo lililopelekea vurugu hizo, baina ya jeshi la polisi na wananchi.



LOWASA AMTEMBELEA LISSU



Waziri Mkuu wa zamani na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Edward Lowassa leo Oktoba 24 amemtembelea na kumjulia hali Mwanasheria Mkuu wa CHADEMA, Tundu Lissu ambaye anaendelea kupatiwa matibu Nairobi nchini Kenya.
Katika safari hiyo, Lowassa alikuwa ameandamana na mke wake, Mama Reginal Lowassa na wameonekana kwenye picha wakiwa na furaha na Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu.
Viongozi mbalimbali wa chama hicho wamekuwa wakiendelea kumtembelea na kumjulia hali kiongozi huyo, ambapo hivi karibuni Mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche na Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi

TUNATARAJIA KUPAA ZAIDI MWIJAGE


Image result for PHOTO OF CHARLES MWIJAGE
TANZANIA imesema haiwezi kutegemea ushuru wa forodha pekee kulinda bidhaa za ndani, hivyo ubora ni jambo la msingi ili ziweze kumudu ushindani wa kibiashara ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).
Kwa mujibu wa taarifa ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, kwa kuwa Tanzania ni mwanachama wa EAC na SADC, takribani nchi 22 zina haki ya kuingiza bidhaa nchini bila ukomo na bila kutozwa ushuru wa forodha.
Waziri mwenye dhamana na wizara hiyo, Charles Mwijage amesema, ili Tanzania ifanikwe kwenye masoko ya kimataifa na kufikia lengo la kuwa nchi yenye uchumi wa kati wa viwanda, inapaswa kuingiza matumizi ya viwango katika nyanja zote za uzalishaji, biashara na utoaji huduma.
Alisema, ingawa matumizi ya viwango nchini si ya kiwango cha juu kulinganisha na kasi ya kimataifa, Shirika la Viwango Tanzania (TBS) limetayarisha viwango vya kitaifa kwa lengo la kuchochea ukuaji uchumi na maendeleo ya jamii.
TBS ni miongoni mwa mashirika 162 ya viwango duniani ambayo ni wanachama wa Shirika la Viwango la Kimataifa (ISO). Hata hivyo, Mkurugenzi Mkuu wa TBS, Profesa Egid Mubofu amesema, utayarishaji wa viwango vya kitaifa unazingatia Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025, ambayo pamoja na mambo mengine inataka hadi kufikia mwaka 2025 Tanzania iwe nchi ya uchumi wa kati wa viwanda na kiwango kikubwa cha maendeleo ya watu.
Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji anayeshughulikia viwanda na biashara, Profesa Adolf Mkenda amesema, mbali na TBS viwango pia vinatazamwa na Tume ya Ushindani (FCC) na mamlaka nyingine za udhibiti na usimamizi ikiwemo Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) wanapaswa kuhakikisha Tanzania inatekeleza kikamilifu azma ya kujenga uchumi wa viwanda.
FCC ni chombo huru cha serikali kilichoanzishwa kwa Sheria ya Bunge Namba 8 ya Mwaka 2003 ili kuhamasisha usawa kwenye ushindani wa kibishara sanjari na kumlinda mlaji na mtumiaji wa bidhaa.
Aidha TFDA ni wakala wa Serikali chini ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia , Wazee na Watoto wenye wajibu wa kusimamia ubora na usalama wa chakula, dawa, vipodozi na vifaa tiba ili kulinda afya za wananchi.
Ilianzishwa kupitia kifungu 4(1) cha Sheria ya Chakula, Dawa na Vipodozi, na ilianza kazi rasmi Julai Mosi, 2003. Alisema, shughuli za mamlaka hizo ni muhimu zaidi wakati huu kwa sababu Serikali, kupitia Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano, imeamua kujenga uchumi wa viwanda.
Alisema, ili kuuza bidhaa kwenye soko la dunia, suala la usalama na ubora ni lazima lizingatiwe kwa kiwango cha juu. Profesa Mkenda alisema, kama bidhaa za viwandani nchini hazitakidhi viwango vya ubora na usalama, wananchi wataendelea kupenda bidhaa zinazoagizwa kutoka nje ya nchi hivyo kudhoofisha uzalishaji wa ndani.
Profesa Mkenda alisema pia kwamba, kuna haja ya kuzuia uingizwaji wa bidhaa zisizo na viwango na bidhaa bandia kutoka nje ya nchi kwa kuwa zitaleta ushindani usio wa haki kwa wazalishaji wa ndani.
“Bidhaa hizi zisizo na viwango na zile bandia zinapoingia nchini zinadhoofisha sana uzalishaji wa ndani kwa kuleta ushindani usio wa haki na kudhulumu walaji. Lazima tukubali kwamba bidhaa bora, salama na zisizo bandia kutoka nje zitaendelea kuingia nchini.
Baadhi ya bidhaa hizo zitatoka nchi za Jumuiya ya Afrika ya Mashariki na nchi za SADC, na hivyo zitaingia nchini bila kutozwa ushuru wa forodha na bila kuwekewa ukomo”alisema.
Alisema, uzalishaji wa ndani lazima ukukidhi viwango vya kimataifa, hivyo mamlaka za udhibiti na usimamizi zina wajibu wa kufanikisha hilo ili bidha za Tanzania zihimili ushindani ndani na kwenye masoko ya nje.
“Lazima tukubali kuwa ushindani wa haki ni jambo jema. Ushindani wa haki humnufaisha mlaji kwa kumpa bidhaa bora na salama kwa bei ahueni. Ushindani pia hulazimisha wazalishaji wengine kuacha kubweteka na badala yake kuongeza ubunifu na ubora wa bidhaa zao.
Kwa maana hiyo ushindani ni jambo bora sana” alisema Profesa Mkenda. Mkurugenzi wa Udhibiti Ubora wa TBS, Mhandisi Tumaini Mtitu amesema, bidhaa zisizo na viwango vya ubora husababisha ushindani usio sawa katika soko, zinadhuru afya za walaji au watumiaji wa bidhaa na huchafua mazingira kwa namna tofauti.
“Nembo ya ubora ya TBS ndiyo inayopaswa kutumika kuonesha kuwa bidhaa hii au ile imethibitishwa ubora kwa sababu inatolewa na shirika lenye dhamana ya kudhibiti ubora wa huduma na bidhaa zinazozalishwa na viwanda vya ndani na ndilo linaloviandaa viwango hivyo kwa ngazi ya taifa” alisema Mtitu. Alisema, hata bidhaa zinazoingizwa katika soko la ndani kutoka nje ya Tanzania hukaguliwa ubora ili kujiridhisha kuwa zinakidhi viwango vya kimataifa.

MHE:LUKUVI ATOLEA UFAFANUZI WA BOMOA BOMOA


Image result for PHOTO OF WILLIAM LUKUVI
SERIKALI imewaondoa hofu wananchi juu ya tishio la bomoabomoa ya nchi nzima kwa waliojenga bila kuwa na vibali vya ujenzi, ikisisitiza si wote watakaohusika, bali `matapeli’ na wavamizi wa maeneo ya watu wengine.
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi ameongeza kuwa, wananchi waliojengwa kwenye maeneo yasiyopimwa na wasio na vibali vya ujenzi, hawatabolewa nyumba zao, kama umma ulivyopotoshwa.
Lukuvi alisema hayo Ikulu jijini Dar es Salaam jana wakati wa hafla ya kuwatunuku vyeti wajumbe walioteuliwa na Rais John Magufuli kuchunguza biashara ya madini. Kwa mujibu wa Lukuvi, alilazimika kufafanua hivyo baada ya jana baadhi ya vyombo vya habari, hususani magazeti, kumnukuu vibaya kwa kuandika kuwa wananchi waliojenga kwenye maeneo yasiyopimwa na bila kuwa na vibali watabolewa nyumba zao.
“Asilimia 85 ya wananchi wanaishi kwenye makazi holela katika maeneo ambayo hayakupimwa. Serikali hatutabomoa nyumba zao ila tunachokifanya ni kurasimisha makazi yao ili waishi mahali salama, wapate huduma za kijamii na waweze kulipa kodi kwa serikali,” alieleza Waziri Lukuvi.
Lukuvi alisema nyumba zitakazobolewa ni zile zilizojengwa kwenye viwanja walivyoporwa wananchi wanyonge na masikini. Alisema Serikali haitafumbia macho watu wenye nguvu ya pesa, wanaoshirikiana na baadhi ya watumishi wasio waaminifu wizarani na kwenye halmashauri, kunyang’anya viwanja vya wananchi masikini na kubadilisha umiliki wa viwanja hivyo.

MILLION 200 ZAKUSANYWA MNADA WA NG'OMBE


Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Luhaga Mpina akiongea na waandishi wa habari kuhusu opareshei ondoa Mifugo leo katika ofisi za wizara hiyo jijini Dar es Salaam,Pembeni yake ni Naibu Waziri Abdalah ulega, kulia ni Katibu Mkuu wa Wizara hiyo katika sekta ya Mifugo Dkt Maria Mashingo na kushoto ni Katibu Mkuu sekta ya Uvuvi Dkt. Yohana Budeba

Kupitia Amri ya Mahakama iliyoamuru kupigwa mnada kwa ng’ombe waliovamia toka nchi jirani ya Kenya, Serikali imekusanya zaidi ya Shilingi Milioni 200 baada ya ng’ombe hao kupigwa mnada katika wilaya ya Mwanga mwishoni mwa wiki.
Akiongea na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo, Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Luhaga Mpiga amesema Wizara yake imejipanga na kuendelea na Oparesheni maalum ya kukamata na kuondoa mifugo yote inayovamia  kutoka nchi jirani kupitia mikoa ya mipakani kama Katavi, Kigoma, Tanga, Mara,Ruvuma, na Arusha na kuagiza wakuu wa Mikoa na Wilaya hizo kuendesha Opresheni hizo Maalum ndani ya siku saba.
“Mimi , Naibu Waziri wangu, makatibu wakuu na wataalam tunaingia tena katika opareshi hiyo maalum kesho.” Alisisitiza Mpina
Aidha, Mpina alisema kuwa serikali haipo tayari kuingia gharama ya kutibu magonjwa yanayoletwa na mifugo wanaovamia kutoka nchi jirani ambao kwa namna moja au nyingine huleta uharibifu wa mazingira kwa kukata miti ovyo, kusababisha mmomonyoko wa udongo na kuchangia kwa kiasi kikubwa migogoro ya wakulima na wafugaji.
Mpina alisema, watu wenye nia mbaya wasihusishe Opareni hii na mahusiano ya nchi hizi mbili akitolea mfano mahusiano ya Kenya na Tanzania katika Jumuiya ya Afrika Mashariki kuwa yapo kisheria.
Akizungumzia suala ya mifugo ya Tanzania kuwa na chapa Mpina alisema, suala hili linashughulikiwa na ifikapo Desemba mwaka huu litakuwa limekamilika na hivyo kurahisha oparesheni hizi za kuondoa mifugo vamizi.

KANUMBA ALINITOLEA PANGA LULU ANENA

Image result for PHOTO OF ELIZABETH MICHAEL


MSANII wa filamu nchini, Elizabeth Michael maarufu kama Lulu ameanza kujitetea katika Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam akieleza alichokuwa akifanyiwa na marehemu Steven Kanumba.
Akitoa utetezi wake katika kesi hiyo ya kuua bila kukusudia, Lulu amesema Kanumba alikuwa akilewa na kumpiga na kwamba Kanumba aliwahi alimpiga kwa panga mapajani na akapelekwa Hospitali ya Mwananyamala.
“Sijasababisha kifo cha Kanumba kwa namna yoyote ile. Umbo langu lilikuwa dogo hivyo mimi ndiyo nilikuwa nashambuliwa. Kama marehemu asingeanguka labda angenidhuru. Kanumba alikuwa kama mlezi wangu, tulianza mahusiano miezi minne kabla ya kifo chake,” amesema Lulu.
“Nilikuwa nataka kutoka ila marehemu (Kanumba) alinikataza, alikuwa hataki nitoke, nilipomwambia natoka na marafiki zangu alinikimbiza na taulo na mimi nilikuwa naogopa kupigwa, mara nyingi alikuwa ananipiga kila akilewa na sio kwa akili zake.  Alipoona simu yangu inaita akahisi ni simu ya mwanaume akasema kwa nini naongea na simu ya mwanaume mbele yake? Marehemu akaingia uvunguni akatoa panga akasema leo nakuua huku akinipiga na panga kwenye mapaja”, ameelezea Lulu.
Lulu ameendelea kusimulia…. “Marehemu alianguka mwenyewe na kujigonga kwa nguvu na kuinuka akitapatapa, nilimwambia Seth kuwa Kanumba amedondoka na akajaribu kumuamsha hakuamka,  akasema anaenda kumuita daktari, alivyosema anaenda kumuita daktari na mimi nikaondoka nikiogopa anaweza akaamka akaanza kunipiga.  Niliondoka nikawasha gari kuelekea Coco Beach kutuliza akili”.
Muigizaji huyo ameendelea kusimulia kwamba … “Nilivyofika Coco Beach meseji zilianza kusambaa kuniuliza kuwa nasikia Kanumba amefariki, nikampigia Kidume ambaye ni rafiki yake Kanumba kumuuliza Kanumba yupo hospitali gani niende kumuona, akaniambia wewe usije hospitali, niambie uko wapi, tukakubaliana tuonane Bamaga.  Tulivyokutana Bamaga alikuwa kama anataka kuongea na mimi ghafla wakaja askari kunikamata,” ameeleza Lulu.
Baada YA Muigizaji, Elizabeth Michael ‘Lulu’kuanza kujitetea katika Mahakama Kuu Kanda ya Dar, kwa tuhuma za kusababisha kifo cha Steven Kanumba bila kukusudia, msanii huyo amekana kuhusika na kifo hicho.
Lulu ameeleza siku ya tukio, Kanumba alikuwa amelewa na yeye Lulu alitaka kutoka na marafiki zake lakini alimkataza, baada ya Kanumba kuona simu ya Lulu imeita alizani anaongea na mwanamme mwingine huku ambapo alichukua panga na kumkimbiza nalo. Kanumba alianguka na Lulu kuchukua gari na kukimbilia Coco Beach ambapo baadaye alikamatwa na polisi maeneo ya Bamaga.
Jaji wa Mahakama Kuu, Samu Rumanyika amemtwanga maswali Lulu kama ifuatavyo;
Jaji Sam Rumanyika: Kipindi unaendesha gari ulikuwa na leseni halali?
Lulu: Ndiyo.
Jaji: Tufafanulie uhalali wake.
Lulu: Nilikuwa sina.
Lulu: Baada ya kukamatwa nilipelekwa kituo cha polisi Oysterbay nilikuwa nikihojiwa nikiwa sijui kama Kanumba amefariki.
Lulu ameeleza hayo leo Jumatatu akijitetea katika kesi ya kuua bila kukusudia inayomkabili.

VIINGILIO VYA MECHI YA SIMBA NA YANGA HIVI APA

Image result for PHOTO OF SIMBA FC VS YANGA FC

Mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara kati ya Young Africans na Simba utafanyika Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam kama ilivyotangazwa awali. Hakuna mabadiliko.
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), limetangaza viingilio katika mchezo huo kwamba watazamaji watakaohitaji kukaa katika Jukwaa Kuu watalipia Sh 20,000 na Mzunguko ni Sh 10,000.

NILIPEWA KADI NYEKUNDU KIMAKOSA NEYMAR ASEMA


Image result for PHOTO OF NEYMAR JR IN PSG


Mshambuliaji wa Paris Saint-Germain, Neymar amedai kuwa kutolewa dimbani kwa kadi mbili za njano dhidi ya Marseille haikuwa haki.
Zikiwa zimebaki dakika tatu alipewa onyo kwa majibu yake baada ya kufanyiwa faulo na Lucas Ocampos, na Mbrazili huyo aliamrishwa kutoka dimbani timu yake ikiwa nyuma kwa mabao 2-1.
Mpira wa adhabu uliopigwa na Edinson Cavani dakika za majeruhi uliwawezesha miamba hao wa Ligue 1 kupata sare, lakini Neymar amekiri kuwa alikasirishwa na hatua zilizochukuliwa dhidi yake katika uwanja wa Velodrome.
Neymar, 25, amekiambia Esporte Interativo: "Nadhani mambo yalikuzwa, naam. Haikuwa haki. Mchezo wote nimekuwa nikichezewa rafu. Nina alama tele mwilini mwangu.
"Nilijaribu kuendelea kucheza baada ya kufanyiwa faulo. Lakini nilikerwa zaidi na maamuzi ya refa kwa kunitoa nje."
Licha ya sare hiyo, PSG ipo mbele kwa pointi nne dhidi ya timu inayoshika nafasi ya pili Ligue 1

RONALDO ASHINDA TUZO ZA FIFA AKIWABWAGA MESSI NA NEYMAR JR

Staa wa Ureno, Cristiano Ronaldo amefanikiwa kutwaa Tuzo ya Mchezaji Bora wa Fifa kwa mwaka 2017 kwa mara ya pili mfululizo tangu kureshwa kwa utaratibu wa tuzo huo, mwaka jana.
Ronaldo amekabidhiwa tuzo hiyo jijini London kulipofanyika sherehe za utoaji wa tuzo hiyo ambapo amewapiga bao Lionel Messi wa Barcelona na Neymar PSG.
Tuzo hiyo ambayo iliwepo miaka ya nyuma ilipotea baada ya kuungana na ile ya Ballond’Or lakini mwaka jana Fifa iliamua kujiweka pembeni na kuendelea kuratibu tuzo zake kama zamani huku wale wengine nao wakiendelea na tuzo yao.
Wakati Ronaldo akikabidhiwa tuzo hiyo, kocha wake wa Real Madrid, Zinedine Zidane yeye amepewa tuzo ya Kocha Bora wa Mwaka

HIVI HAPA VICHWA VYA MAGAZETI YA MICHEZO LEO OCTOBA 24









PROFFESOR FLORENS LUOGA GAVANA MPYA BENKI KUU


Rais Dk John Magufuli amteua Profesa Florens Luoga kuwa Gavana wa Benki Kuu Tanzania. Amtaka Gavana wa sasa Beno Ndulu kuanza utaratibu wa kukabidhi ofisi haraka.
Rais Magufuli alifanya uteuzi huo wakati wakati wa kutunuku vyeti vya pongezi maalum wajumbe wote waliohusika kuchunguza kiwango, aina na thamani ya madini katika makinikia.
Kabla ya uteuzi huo, Profesa Luoga alikuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Mamlaka ya Mapato ya Tanzania (TRA). Akihutubia Taifa baada ya kuwatunuku wajumbe hao, Rais Magufuli amewaonya watu wanaopotosha takwimu rasmi za serikali na kutoa za uongo.
Kutokana na tabia hiyo ya baadhi ya watu, Rais amemwagiza Waziri wa Katiba pamoja na vyombo vya dola kuwachukulia hatua watu wanaopotosha takwimu wakati ukweli wanaujua.
"Vita ya kupigania rasilimali za nchi ni ngumu sana, ninapata shida kubwa kutokana na kuongoza vita hii, inaniumiza sana lakini nimetumwa na Watanzania kuifanya kazi hii kwa moyo wangu wote" Rais Dk John Magufuli Rais Magufuli amewashutumu watu wanaopinga juhudi za serikali za kutetea rasilimali za nchi akisema wanapigania matumbo yao "Wanaopinga juhudi za serikali za kupigania rasilimali za nchi wanatetea pesa walizoahidiwa na wezi wa rasilimali zetu" Rais Dk John Magufuli, Ikulu, Dar es Salaam.
Rais Magufuli ashukuru vyama vya upinzani kwa kuruhusu wanachama wao kuwepo katika kamati za madini kwa sababu maendeleo hayana vyama. Asema fedha zikiongezeka hata ruzuku za vyama zitaongezeka