UTAFITI:VIFO VYA WANAUME NI VINGI ZAIDI YA VYA WANAWAKE


.


“MATOKEO ya utafiti huu yanatuonesha mahali tulipo na changamoto mbalimbali kuhusu ubora, utunzaji na utumiaji wa takwimu za vifo katika hospitali zetu. “Vile vile taarifa hii inaainisha vyanzo na sababu mbalimbali za vifo kwa wananchi tunaowahudumia katika hospitali zetu.
Ninaamini kuwa ripoti hii itaibua mjadala chanya na mawazo mapya ili kuboresha takwimu zetu za afya.” Yalikuwa maneno ya utangulizi ya Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Paul Ntinika alipomwakilisha Mkuu wa Mkoa, Amos Makala kwenye ufunguzi wa warsha kuhusu sababu za vifo katika hospitali za Tanzania. Huu ni utafiti uliofanywa na Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu nchini (NIMR).
Kwa mujibu wa Mtafiti Mkuu Kiongozi kutoka NIMR, Dk Leonard Moera, utafiti huu ulifanyika Julai 2015 hadi Juni 2016. Malengo yake yalikuwa ni kuainisha matukio ya vifo katika hospitali za nchini ili kutambua ongezeko la maradhi yanayoathiri jamii.
Ulichunguza pia uwepo, upatikanaji na ubora wa takwimu za vifo hospitalini. Dk Moera anasema utafiti huu ulihusisha hospitali 11, ikiwemo Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, hospitali za rufaa za mikoa na kanda, hospitali maalumu na za wilaya.
Hospitali ambazo takwimu hazikupatikana ni pamoja na Hospitali ya Wilaya ya Chunya iliyopo mkoani Mbeya. Mfuko wa Dunia wa kupambana na Ukimwi, Kifua kikuu na Malaria kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto ndiyo waliowezesha kufanyika kwa utafiti huu muhimu.
Mkuu wa wilaya anasema, kama ilivyoainishwa katika mpango mkakati wa sekta ya afya namba IV, serikali inachukua hatua mahususi kuboresha mfumo wa utoaji wa taarifa za afya ili kukidhi mahitaji ya ufuatiliaji wa huduma za afya.
Dhamira ya serikali ni kutumia mfumo wa kielektroniki katika ukusanyaji, uchanganuzi na matumizi ya takwimu. “Kwa utaratibu huu, ni matumaini yetu tutaongeza ubora wa takwimu tunazozalisha katika mfumo wetu wa tarifa.
Pamoja na hilo, serikali itatilia mkazo mafunzo ya watumishi na kuwakumbusha umuhimu wa kufuata miongozo ya kitaifa na kimataifa katika kuainisha vyanzo vya maradhi na vifo,” anasema Ntinika.
Mkuu huyo wa wilaya anaipongeza ripoti ya utafiti wa NIMRI akisema ni ya aina yake nchini kwa kuwa inaainisha upatikanaji na viwango au sababu za vifo vilivyotokea katika hospitali za Tanzania kwa kipindi cha miaka kumi kuanzia mwaka 2006 hadi 2015.
“Matokeo ya utafiti huu yanaonesha kuwa maradhi yanayoongoza katika kusababisha vifo nchini ni malaria, magonjwa ya mfumo wa kupumua, Ukimwi, upungufu wa damu na magonjwa ya moyo na mfumo wa damu,” anasema.
Hata hivyo, vifo vinavyotokana na malaria, Ukimwi pamoja na Kifua Kikuu vimepungua sana. Kwa mfano, vifo kutokana na malaria vimepungua kwa asilimia 47. Vifo vitokanavyo na Ukimwi vimepungua kwa asilimia 28 na kifua kikuu kwa asilimia 26 kutoka mwaka 2006 hadi 2015.
Pamoja na kupungua huko, takwimu za utafiti huu zinaonesha kuwa bado malaria ni ugonjwa unaoongoza kwa vifo vingi nchini huku Ukimwi ukishika nafasi ya tatu nyuma ya magonjwa ya mfumo wa kupumua.
Takwimu zinaonesha kuwa katika kipindi hicho (2006-2015), kati ya vifo 247,976 vilivyotokea, malaria iliongoza kwa asilimia 12.8, magonjwa ya mfumo wa kupumua asilimia 10.1, Ukimwi asiliamia 8.0, upungufu wa damu asilimia 7.8 na magonjwa ya moyo na mfumuko wa damu asilimia 6.3.
Pia kumekuwepo ongezeko kubwa la vifo kwa asilimia 128 vinavyosababishwa na magonjwa yanayoathiri kundi la watoto wachanga hasa wenye umri wa chini ya mwezi mmoja.
Kwa upande mwingine, vifo vinavyotokana na magonjwa yasiyoambukiza na ajali vimeongezeka. Katika miaka ya hivi karibuni, vifo vitokanavyo na ajali vimeongezeka kwa asilimia 16, saratani asilimia 24, kiharusi asilimia 27 na kisukari asilimia 11. Inaelezwa kuna dalili kuwa magonjwa haya yataendelea kuongezeka katika siku za usoni. “Hii ni ishara kuwa mafanikio yetu kupunguza magonjwa yasiyoambukiza yanaathiriwa na ongezeko la magonjwa yasiyoambukiza,” anasema Ntinika.
Ntinika anasema, “Kupungua kwa vifo kutokana na magonjwa makubwa ni dhahiri kuwa mikakati yetu katika magonjwa haya inafanikiwa. Hapa nawapongeza watumishi wote wa afya katika ngazi mbalimbali kwa mafanikiao haya makubwa.” Hata hivyo, anasema, baada ya kupitia na kuichambua ripoti hii amegundua kuwa watu wanakufa kwa magonjwa yanayozuilika.
“Ikiwa ni kweli kwamba malaria, Ukimwi, magonjwa ya mfumo wa kupumua, magonjwa yasiyoambukiza na ajali huua maelfu ya watu wetu, hii inatoa taswira kuwa tunayo kazi kubwa ya kufanya kuzuia vifo hivyo.
Mikakati mseto inahitajika kupambana na magonjwa ya makundi yote hayo,” anasema Ntinika. Utafiti unaonesha vifo vingi vimetokea katika hospitali za Dar es Salaam, Morogoro na Mwanza.
Idadi kubwa ya vifo ni katika kundi la wanaume. Mikoa inayoongoza kwa kuwa na vifo vingi kwenye kundi la wanaume kuliko wanawake ni Mara, Kilimanjaro, Kigoma, Pwani, Ruvuma na Rukwa.
Mtafiti mkuu kiongozi kutoka NIMR, Dk Moera anasema uzembe wa kutowahi matibabu ni chanzo cha wanaume nchini kukabiliwa na wimbi la vifo zaidi ya wanawake. Sababu ya vifo vingi vya wanaume ni utayari mdogo wa kwenda kuchunguza afya zao tofauti na ilivyo kwa wanawake.
“Wanaume ni wazito kwenda katika vituo vya tiba. Hata pale mtu anapojisikia tofauti ya mwili yaani maumivu ya kichwa au chochote mara nyingi ni watu wa kuhisi labda ni uchovu, na wakati mwingine utakwenda duka la dawa kutafuta dawa za kutuliza maumivu tu. “Hivyo mpaka unakwenda kwenye kituo cha tiba, tayari ugonjwa ulikwisha kuwa sugu mwilini hivyo kupona inakuwa vigumu,” anasema Dk Moera.
Anawasihi wanaume kubadili mitazamo na kupenda kuchunguza afya mara kwa mara hasa kutokana na kuwa mfumo wa maisha yao ni wa kukumbana na misukosuko mingi katika mazingira tofauti yakiwemo yaliyo hatari.
Utafiti pia unasema mikoa ya Mbeya, Iringa na Ruvuma bado inaongoza kwa vifo vitokanavyo na Ukimwi, hali inayoonesha kuwa bado kuna kazi kubwa ya kupunguza maambukizi ya Virusi vya Ukimwi (VVU).
Mkuu wa wilaya anasema taarifa ya utafiti huu ni muhimu sana kwa ajili ya kufanya uamuzi na kuandaa mipango kwa kutegemea ushahidi wa kitaalamu. Bila takwimu za uhakika si rahisi kujua ukubwa wa matatizo na changamoto za utoaji huduma za afya. “Bila takwimu sahihi, tutajikuta tunashughulika na matatizo yenye umuhimu mdogo na hivyo kutotumia rasilimali zetu ipasavyo.
Ni muhimu timu za menejimenti za mikoa za afya na hospitali zote kufanyia kazi mapendekezo ya ripoti hii ili kuboresha takwimu katika hospitali zetu,” anasisitiza Ntinika. Kaimu Mkurugenzi wa wa NIMR Mbeya, Dk Nyanda Elius na Mganga Mkuu Mkoa wa Rukwa, Dk Boniface Kasululu wanahimiza wadau wa afya kutumia taarifa za utafiti huo katika utekelezaji wao wa kila siku. Uwapo wa takwimu ni dira ya ufumbuzi wa jambo lolote. Ili takwimu zipatikane, ni muhimu utafiti ufanyike na uje na mapendekezo ya kufanyia kazi

HALI YA LISSU YAIMARIKA AANZA KUFANYA MAZOEZI





HALI ya Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (Chadema) anayepatiwa matibabu katika hospitali jijini Nairobi nchini Kenya baada ya kushambuliwa kwa risasi imeelezwa kuimarika huku akiwa ameanza kufanya mazoezi.
Aidha, gharama za matibabu yake yote kuanzia aliposhambuliwa hadi Oktoba 12, mwaka huu, anapoendelea na matibabu nchini Nairobi zimefikia jumla ya Sh milioni 412.4. Hata hivyo, Chadema imesema wanaiachia familia suala la kuwa wasemaji wa Lissu, lakini ikasisitiza kuwa atapelekwa nje ya nchi kwa ajili ya awamu ya tatu ya matibabu yake.
Kadhalika imesema kuanzia sasa inaanza kutoa sauti na picha za Lissu katika mitandao mbalimbali ya kijamii ili kuwaonesha Watanzania kuhusu hali halisi ya mgonjwa waliyekuwa wakimuombea.
Mwenyekiti wa Taifa wa Chadema, Freeman Mbowe alisema hayo jana Dar es Salaam wakati akizungumzia hali halisi ya Lissu na kuongeza kuwa wakati wa matibabu yake, ameweza kufanyiwa upasuaji wa aina tofautitofauti mara 17 huku akiwa amepewa damu nyingi kuliko wagonjwa waliowahi kutibiwa katika hospitali hiyo.
Kuhusu hali ya Lissu, Mbowe alisema kwa muda wote tangu alipofikishwa hospitalini hapo, alikuwa katika chumba cha uangalizi maalumu (ICU) akihudumiwa na madaktari 12, lakini wiki iliyopita ametoka na mashine zote alizokuwa akitumia zimeondolewa mwilini mwake.
“Kwa sasa mwili wake unaweza kusukuma damu peke yake, viungo vyote viko timamu ikiwemo figo, hatumii mashine ya oksijeni, mirija ya chakula pia haitumii tena,” alieleza Mbowe na kuongeza kuwa juzi kwa mara ya kwanza alikaa mwenyewe kwani viungo vyote vimeungwa.
Alisema Lissu pia anaweza kutembea katika kiti cha kubeba wagonjwa na wiki iliyopita aliweza kuliona jua kwa mara ya kwanza tangu aliposhambuliwa mjini Dodoma. Mbowe alisema Hospitali ya Nairobi ni ya pili iliyokuwa ikiendelea kutoa matibabu kwa Lissu, baada ya ile ya Dodoma siku ya shambulio na kwamba baada ya wiki moja kuanzia sasa, atamaliza matibabu ya awamu ya pili na kusudio ni awamu ya tatu ambayo atapelekwa nje ya Tanzania wa ajili ya uponyaji zaidi.
“Awamu ya tatu ambayo ni ya muda mrefu zaidi ya uponyaji atapelekwa nje ya nchi ambako kwa sasa hatuwezi kusema ni nchi gani kwa sababu za kiusalama,” alieleza Mbowe akisisitiza kuwa chama hicho bado kinaiomba serikali kuruhusu wachunguzi wa nje ili kufuatilia waliohusika katika shambulio hilo.
Kuhusu dereva wa Lissu, alisema chama hakijamficha na hajawahi kukimbia na kwamba Jeshi la Polisi linaweza kumpata popote pale alipo. Kuhusu kuiachia familia suala la Lissu, alieleza kuwa chama hicho kimefanya kazi na familia kwa muda wote waliokuwa wakimuuguza Lissu, lakini kwa awamu ya tatu ya matibabu yake wanaiachia ifanye maamuzi ya ndani.
“Jukumu la kuwa wasemaji wa suala la Lissu tunalikabidhi kwa familia, kwa sababu mgonjwa ameimarika anaweza kufanya uamuzi hivyo tumeona tusiingie mpaka uvunguni, bali tukasimu kwa familia ambayo ina haki,” alisema na kufafanua kuwa chama hakijivui wajibu, bali watawajibika nyuma ya familia.
Kuhusu gharama za matibabu, alisema fedha hizo zimetokana na michango mbali mbali kutoka kwa Watanzania wote wenye itikadi njema, wabunge, wanachama wa chama hicho, Watanzania waishio nje ya nchi pamoja na wafanyabiashara. Hata hivyo, aliwaomba Watanzania kuendelea kumchangia Lissu ili apate matibabu katika awamu yake ya tatu atakapokuwa nje ya nchi

MAHINDI YA ZAMBIA YAINGIA KWA WINGI MKOA RUKWA





MAHINDI yanaendelea kuwadodea wakulima mkoani Rukwa baada ya wafanyabiashara na watu binafsi kuchangamkia mahindi kutoka nchini jirani ya Zambia yanayoingizwa mkoani humo kimagendo, yakiuzwa kwa bei ya kutupwa na kusifiwa kwa ubora na usafi wake.
Mahindi hayo ambayo inadaiwa yanaingizwa kwa wingi mkoani Rukwa kwa kupitia njia za panya wilayani Kalambo, yanauzwa kwa bei ya kutupwa ya Sh 20,000 kwa gunia lenye uzito wa kilo 100 na debe moja likiuzwa kwa Sh 3,000 huku yakisifiwa kuwa yanakidhi vigezo vya ubora na usafi kuliko yanayozalishwa mkoani humo.
Takwimu za hivi karibuni za hali ya uzalishaji zinaonesha kuwa Mkoa wa Rukwa umezalisha ziada ya ya tani 727,496.6 za chakula huku mahindi pekee yake yakiwa ni tani 453,049.2, huku Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) Kanda ya Sumbawanga wakipangiwa kununua tani 3,000 tu za mahindi katika msimu wa ununuzi wa mahindi ulioanza Agosti 7, mwaka huu na kumalizika Septemba 4, mwaka huu.
Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili hivi karibuni, umebaini kuwa shehena hiyo ya mahindi inavushwa kupitia njia za panya kutoka nchi jirani ya Zambia, ambako wafanyabiashara wanatumia kila aina ya usafiri wakiwemo punda, pikipiki na baiskeli kuyavusha na kuingia nayo wilayani Kalambo.
Uchunguzi umebaini kuwa wafanyabiashara wadogo wa mahindi kutoka Zambia na wengine kutoka nchini, wakifanikiwa kuyaingiza mahindi hayo mkoani Rukwa kupitia njia za panya wilayani Kalambo, wanachanganyika na wakazi wa humo ili wasibainike kuwa wametokea Zambia.
Kutokana na kufurika kwa mahindi hayo kutoka Zambia, yamesababisha mahindi yaliyovunwa msimu huu kuendelea kulundikana na kuwadodea wakulima, ambao kwa sasa hawawezi tena kuuza ngunia moja lenye uzito wa kilo 100 kwa Sh 35,000 kwa kuwa ya Zambia yanauzwa kwa bei ya kutupwa ya chini ya Sh 20,000.
Hivi karibuni, Mkurugenzi Mkuu wa Kituo cha Utafiti wa Kilimo cha Uyole mkoani Mbeya, Tulole Bucheyeki alikanusha taarifa zilizozagaa kuwa mahindi yanazaliwa mkoani Rukwa, yamekosa soko kutokana na kutokuwa na ubora stahiki kwa kuwa wakulima wanatumia mbegu bora za mahindi zilizofanyiwa utafiti na kituo hicho.
Aliwataka wakulima mkoani humo kuupuuza uzushi huo, isipokuwa wazingatie namna bora za uhifadhi ya mahindi wanapoyavuna kwa kuwa yana ubora sawa na yanayozalishwa katika nchi jirani.
Baadhi ya wafanyabiashara wadogo wa mahindi kwa nyakati tofauti, walilieleza gazeti hili kuwa mahindi ya Zambia yanayoingizwa nchini kimagendo yanachangamkiwa sana na walaji na wafanyabiashara kwa kuwa wanadai ni matamu na yamehifadhiwa katika hali ya usafi pia yanauzwa kwa bei ya kutupwa.
“Wafanyabiashara wa mahindi wamewageuzia kibao wakulima wa mkoa huu wanadai kuwa hawahifadhi mahindi katika hali ya ubora unaotakiwa kwamba yanakuwa na uchafu sasa wafanyabiashara wanaona shida kununua gunia la mahindi kwa bei ya shilingi 35,000 yakiwa machafu halafu waanze kupepeta.
“Wakati kuna mahindi kutoka nchi jirani ya Zambia licha ya kuuzwa kwa bei ya Sh 20,000 kwa gunia lenye uzito wa kilo 100 lakini pia yamehifadhiwa vizuri na ni masafi sana,” alisema John Mwanakulya ambaye ni mkazi wa mkoani Rukwa.
Kwa upande wao ‘walanguzi ‘ kutoka Zambia, kwa masharti ya kutoandikwa majina yao gazetini wakihofia kukamatwa, walidai kuwa wakulima wa Rukwa kwa sasa hawawezi kuuza mahindi yao Zambia hata kama watafanikiwa kuyapitisha kwa magendo kwa kuwa wakulima wa nchi hiyo wamevuna ziada kubwa ya mahindi msimu huu wa mavuno.
“Nchini kwetu (Zambia ) tunapata shida, soko la uhakika kwa mahindi tuliyovuna halipo ...sasa tumelazimika kwa namna yoyote ile kuyavusha na kuyauza huku kwa bei hii ndogo ili tuweze kukidhi mahitaji yetu muhimu nyumbani hatuuzi ili kupata faida “ alisema mmoja wa ‘walanguzi.’
Hata hivyo, hawakuwa tayari kueleza jinsi wanavyofaulu kuvuka mpaka na kuingia mkoani Rukwa wakiwa na shehena ya mahindi. Mbunge wa Jimbo la Nkasi Kaskazini, Ally Kessy (CCM) na Mbunge wa Jimbo la Kwela wilayani Sumbawanga, Ignas Malocha (CCM) walieleza kuwa wamejipanga kuonana na Waziri wa Kilimo ili wamfikishie kilio cha wakulima wa mahindi wa mkoa huo.
Mkazi wa Sumbawanga, Zeno Nkoswe alidai kuwa mahindi yamelundikana kwenye nyumba za wakulima, kiasi kwamba wanalazimika kulala juu ya magunia hayo badala ya vitandani, huku akiitaka serikali iingilie kati kwa kuwa msimu wa kilimo umeanza, hivyo itasababisha wakulima wasilime mahindi kwa kuwa bado wana ziada ya kutosha.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kalambo, Simon Ngagani aliitaka serikali kuona uwezekano wa kuipatia uwezo wa kifedha Wakala wa Hifadhi ya Taifa ya Chakula (NFRA) Kanda ya Sumbawanga ili wanunue ziada ya mahindi yaliyolundikana kwa wakulima mkoani humo, kisha iyauzie kwa Mpango wa Chakula Duniani (WFP).
Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga, Apolinary Macheta aliitaka serikali mkoani Rukwa, ialike wilaya na mikoa yenye uhaba wa chakula nchini, waje kununua mahindi kutoka kwa wakulima kwa bei ya ushindani.
“Wafanyabiashara wanaomiliki viwanda vinavyosindika nafaka yakiwemo mahindi waalikwe kuja mkoani hapa kununua ziada hiyo ya mahindi tena wakulima wapatie bure maghala ya serikali ili wahifadhi mahindi yao ili wafanyabiashara hawa waweze kuyanunua kwa urahisi na kwa haraka tena kwa bei ya ushindani hata ya Sh 500/- kwa kilo moja,” alieleza Macheta.
Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga, Dk Halfan Haule alisisitiza kuwa serikali haijakataza kuuza mahindi nje, ispokuwa inasisitiza kuuza unga ambao umeongezwa thamani.

WAAJIRI SERIKALINI KUBANWA ASEMA MKUCHIKA


WAZIRI wa Nchi, Ofi si ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Mkuchika amewaagiza waajiri wote wa serikali kuhakikisha wanatoa vielelezo vinavyotakiwa vya watumishi wao ndani ya siku 14 pale wanapoagizwa kufanya hivyo na Tume ya Utumishi wa Umma, kinyume cha hapo watawajibishwa.
Mkuchika alitoa agizo hilo jana alipotembelea Tume hiyo jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kujionea shughuli zinazofanywa. Aliwataka waajiri hao kuzingatia sheria kwa kuwa imeelezwa kuwa wamekuwa ndio chanzo cha kuchelewesha kesi za waajiriwa kwa kutokutoa ushirikiano kwa haraka.
“Waajiri zingatieni sheria, pale tume inapotaka kupata vielelezo inataka ijiridhishe. Kesi zinachukua muda mrefu kama hakuna vielelezo lazima zichelewe,” alisema Mkuchika. Kwa upande mwingine, aliwataka wafanyakazi wa tume hiyo kutekeleza majukumu yao ya kazi, huku wakijiepusha na rushwa kwa kuwa eneo wanalofanyia kazi lina ushawishi mkubwa.
Pia aliahidi kushughulikia changamoto mbalimbali zinazokabili tume hiyo zikiwemo za rasilimali fedha, watu na usafiri. Naye Kaimu Naibu Katibu wa Tume hiyo, Richard Odongo alisema tume hiyo inapokea na kushughulikia rufaa na malalamiko ya watumishi wa umma ambao hawajaridhika na mamlaka zao za nidhamu.

MVUA KUBWA ZINATARAJIA KUJA TMA



MAMLAKA ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), imewataka wachimbaji wa madini katika migodi midogo midogo kuwa makini kwani ongezeko la maji katika udongo linaweza kusababisha mmomonyoko wa ardhi na maporomoko migodini katika kipindi hiki cha mvua za msimu.
Mkurugenzi Mkuu wa TMA, Dk Agnes Kijazi alisema hayo jana alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu utabiri wa mvua za msimu wa Novemba mwaka huu hadi Aprili mwakani.
Pia imezitaka mamlaka za miji pamoja na wananchi, kuchukua tahadhari kwa kuhakikisha mifumo na njia za kupitisha maji zinafanya kazi katika kiwango cha kutosha ili kuepusha maji kutuama na kusababisha mafuriko na uharibifu wa miundombinu pamoja na upotevu wa maisha na mali.
Akizungumzia mwelekeo wa mvua za msimu, Dk Kijazi alisema kutakuwa na mvua za wastani hadi juu ya wastani katika maeneo mengi yanayopata msimu moja wa mvua kwa mwaka, na kwamba mvua kubwa inatarajiwa Januari mwakani.
“Msimu huu ni mahususi katika maeneo ya magharibi mwa nchi, kanda ya kati, nyanda za juu Kusini Magharibi, kusini mwa nchi, maeneo ya kusini mwa mkoa wa Morogoro pamoja na Ukanda wa Pwani ya Kusini.
Mvua inatarajiwa kuanza wiki ya kwanza ya Novemba na kuisha wiki ya nne ya Aprili, 2018,” alieleza Dk Kijazi. Alisema Kanda ya Kati kwenye mikoa ya Singida na Dodoma, mvua zinatarajiwa kuanza kati ya wiki ya kwanza na ya pili ya Desemba mwaka huu, zinatarajiwa kuwa za wastani hadi juu ya wastani katika maeneo mengi.
Kwa Nyanda za Juu Kusini Magharibi na maeneo ya Kusini mwa nchi, mvua zinatarajiwa kuanza wiki ya nne ya Novemba na wiki ya kwanza ya Desemba. Alisema Pwani ya Kusini kwenye mikoa ya Lindi na Mtwara mvua zinatarajiwa kuanza kati ya wiki ya nne ya Novemba na wiki ya kwanza ya Desemba.
Dk Kijazi aliwataka watumiaji wa taarifa za hali ya hewa ambao ni wakulima, wafugaji, mamlaka za wanyama pori, mamlaka za maji na afya waendelee kutafuta, kupata na kufuata ushauri wa wataalamu katika sekta husika.

TAKUKURU WAMKANYA JOSHUA NASARI





TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) imemuonya Mbunge wa Jimbo la Arumeru Mashariki, Joshua Nassari wa Chadema, ikimtaka aiache taasisi hiyo ifanye kazi kwa mujibu wa sheria na kamwe asiihusishe wala kuiingiza kwenye matukio ya kisiasa.
Taasisi hiyo imetoa tamko hilo, baada ya kushtushwa na kitendo cha mbunge huyo na wenzake, kila wanapowasilisha taarifa zao Takukuru, huzungumza na vyombo vya habari kuhusu yaliyojiri walipowasilisha taarifa hizo huku wakishinikiza hatua zichukuliwe haraka.
Hayo yalibainishwa na Mkurugenzi Mkuu wa taasisi hiyo, Kamishna wa Polisi, Valentino Mlowola wakati alipozungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana kuhusu taarifa mbalimbali zinazotolewa na mbunge huyo kuhusu ushahidi aliouwasilisha kwenye taasisi hiyo.
Kamishna Mlowola alisema mbunge huyo kwa takribani mara tatu alifika katika ofisi za Takukuru na kuwasilisha kile alichokiita ushahidi, lakini mara baada ya kuwasilisha taarifa hizo kwa Takukuru huitisha vyombo vya habari na kuelezea yale yaliyojadiliwa na taasisi hiyo.
“Hiki ni chombo kinachojiendesha kwa mujibu wa sheria, hakishinikizwi wala kuingiliwa na mtu yeyote. Na kinapokea kwa mujibu wa sheria na taratibu taarifa za siri au wazi kutoka kwa mtu yeyote, Nassari anachokiita ushahidi sisi tunakiita taarifa mpaka pale uchunguzi wetu utakapokamilika,” alisisitiza Mlowola.
Alisema Oktoba 2, mwaka huu, mbunge huyo akiambatana na Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema na Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa, wote wa Chadema, walifika katika ofisi za Takukuru na kuwasilisha taarifa zao kuhusu matukio ya rushwa yaliyotokea mkoani Arusha.
Alisema Oktoba 14 pamoja na Oktoba 16, mwaka huu, Nassari pia aliwasilisha tena maelezo yake kuhusu suala hilo la rushwa kwa Takukuru na kila alipoondoka alifanya mkutano na waandishi wa habari na kuelezea yaliyojiri wakati akiwasilisha taarifa hizo.
Mkuu wa Takukuru alisema kwa mshtuko taasisi hiyo ilishangaa kuona mbunge huyo na wenzake, wakifanya vikao na waandishi wa habari na kuzungumzia kwa undani yaliyojiri hadi yale ambayo hayakupaswa kuzungumzwa kutokana na kuharibu uchunguzi.
Alisema kazi ya Takukuru ni kupokea taarifa za rushwa na ubadhirifu na kuzifanyia uchunguzi wa kina na ikishathibitika kuwepo kwa tatizo, hufungua jalada na kuliwasilisha katika ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka kwa ajili ya hatua za kisheria kuchukuliwa.
“Kwetu sisi Nassari alikuwa mtoa taarifa na tuna jukumu la kumlinda kwa mujibu wa sheria, lakini safari hii yeye mwenyewe anaji expose mbele ya vyombo vya habari. Ninachoona Nassari anataka kulifanya suala hili kuwa la kisiasa badala ya kisheria,” alisema.
“…Namuonya ameshatupa taarifa atuache tufanye kazi kwa mujibu wa sheria. Na akiendelea tutamchukulia hatua za kisheria bila kuathiri taarifa alizotuletea,” alisisitiza. Alitoa onyo hilo pia kwa watu wengine, wanaofikiri kuwa wanaweza kuishinikiza Takukuru na kuingiza katika masuala ya kisiasa kuwa wakome, kwani inafanya kazi wa mujibu taratibu na sheria zilizopo.
Mbunge huyo hivi karibuni baada ya kuwasilisha taarifa yake kwa Takukuru, alizungumza na waandishi wa habari nje ya ofisi za taasisi hiyo Upanga na kubainisha wazi kuwa amewasilisha ushahidi mwingine kwa Takukuru kuhusu tuhuma za ununuzi wa madiwani wa Chama hicho.
Alidai aliwasilisha ushahidi huo ukiwa kwenye ‘flash’, ambayo amekuwa akizunguka nayo kila mahali. Madiwani wanane wa Chadema walijiuzulu hivi karibuni, wakieleza kumuunga mkono Rais John Magufuli kwa utendaji kazi wake, jambo ambalo Nassari anadai siyo kweli, bali walinunuliwa.
“Huu ni ushahidi wa tatu na kadri upelelezi ukiwa unaendelea nitaleta mwingine, hii ni kama filamu ya Isidingo,” alisema Nassari na kuongeza kuwa alitarajia Rais Magufuli angewachukulia hatua wateule wake wanaohusishwa katika sakata hilo ili kupisha uchunguzi ufanyike kwa uhuru

SERIKALI YA OMAN YAOMBA KUWEKEZA SEKTA YA VIWANDA



Mfalme wa Oman Mtukufu Sayyid Qaboos bin Said Al Said amemhakikishia Rais Dk John Magufuli kuwa nchi hiyo ipo tayari kuunga mkono juhudi za Serikali ya Awamu ya Tano kwa kuongeza uwekezaji katika viwanda, uzalishaji wa nishati, kuongeza thamani ya madini, kuendeleza sekta ya gesi na mafuta na kuendeleza ukanda wa uwekezaji wa Bagamoyo ili kukuza uchumi kwa kasi zaidi.
Ujumbe huu wa Mfalme wa Oman umewasilishwa kwa Rais Magufuli na Waziri wa Mafuta na Gesi wa Oman Dk Mohammed Hamad Al Rumhy aliyeongozana na Waziri wa Uwekezaji wa Oman Salem Ben Nasser Al Ismaily na Naibu Waziri wa Utalii Maitha Saif Majid, Ikulu Jijini Dar es Salaam.
Dk Rumhy ambaye ameongoza watu zaidi 300 waliokuja nchini kwa meli ya Mfalme wa Oman amesema ziara hii imelenga kuimarisha uhusiano kati ya Tanzania na Oman hususani katika masuala ya uchumi, ambapo Oman inabadilishana uzoefu na Tanzania kuhusu biashara ya mafuta na gesi, itajenga kiwanda kikubwa cha kuzalisha mbolea katika ukanda wa uwekezaji wa Bagamoyo, itajenga viwanda vya mazao na kununua mazao ya wakulima na itawekeza katika uchakataji wa madini ili kuongeza thamani.
“Mheshimiwa Rais tunataka kushirikiana nanyi kuendeleza ukanda wa uwekezaji wa Bagamoyo, tunataka Bagamoyo isiwe eneo la bandari tu, bali pia liwe ni eneo ambalo tutajenga viwanda mbalimbali, tuzalishe mbolea na tununue mazao ya wakulima na kuyasafirisha, sisi tupo tayari na kesho tunakwenda kuangalia eneo hilo ili kazi zianze mara moja,” amesema Dk Rumhy.
Kwa upande wake Rais Magufuli amemshukuru Mfalme wa Oman Mtukufu Sayyid Qaboos bin Said Al Said kwa kutuma ujumbe huo na amemhakikishia kuwa Tanzania ipo tayari kuendeleza na kukuza zaidi uhusiano wake na Oman.
Rais Magufuli amemtaka Dk Rumhy kufikisha ujumbe wake kwa Mfalme na wawekezaji wa Oman kuwa atafurahi kuona uwekezaji huo unaanza mara moja na kwamba Serikali itatoa ushirikiano wowote utakaohitajika kwa manufaa ya pande zote mbili.
“Dk Mohamed naomba ukamwambie Mfalme kuwa namshukuru kwa ujumbe huu na namkaribisha sana Tanzania, nimefurahi kuona mpo tayari kushirikiana nasi kujenga viwanda, kuzalisha mazao na kuendeleza ukanda wa uwekezaji wa Bagamoyo, sisi tupo tayari hata leo, njooni tushirikiane kwa sababu nyinyi ni ndugu zetu na tutafanya uwekezaji kwa faida yetu sote,” amesema Rais Magufuli.
Aidha, Rais Magufuli ametaka Oman iongeze ushirikiano na Tanzania katika masuala ya utalii na usafiri wa anga, kuwekeza katika usindikaji wa nyama na uvuvi na ushirikiano katika kubadilishana wataalamu wa nyanja mbalimbali wakiwemo walimu wa lugha ya Kiswahili na Kiarabu.
Amemshukuru Mfalme wa Oman kwa msaada kujenga visima vya maji 100 hapa nchini na amemuomba kuungana na Serikali katika safari yake ya kuhamia Dodoma kwa kujenga miundombinu itakayoweka kumbukumbu ya ushirikiano wa kindugu na kihistoria kati ya nchi hizi mbili.
Mazungumzo hayo yamehudhuriwa na Waziri wa Nishati Dk Medard Kalemani na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Dk Suzan Alphonce Kolimba

MAJINA 10,196 YA WANAFUNZI WA ELIMU YA JUU WAMEPATA MKOPO KWA AWAMU YA KWANZA



Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HESLB) imetoa orodha ya kwanza ya majina ya wanafunzi 10,196 kati ya wanafunzi 30,000 wanaotarajiwa kunufaika na mikopo ya elimu ya juu kwa mwaka mpya wa masomo 2017/2018.
Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi hiyo Abdul-Razaq Badru amewaambia waandishi wa habari katika mkutano uliofanyika ofisi kwake Mwenge jijiji Dar es salaam kuwa kufuatia hatua hiyo zaidi ya shilingi bilioni 34.6 tayari zimetengwa kwa ajili ya wanafunzi hao waliopitishwa.
Badru alibainisha kuwa kwa mwaka wa masomo wa 2017/2018 Serikali imetenga zaidi ya shilingi bilioni 108.8 kwa ajili ya wanafunzi hao wapya 30,000 wanaotarajiwa kujiunga na vyuo vikuu.
Kwa wanafunzi waliopata udahili katika chuo zaidi ya kimoja ambao wana sifa za kupata mkopo, Badru ameeleza kuwa wanafunzi hao watapatiwa mikopo baada ya “kuthibitishwa na vyuo watakavyojiunga kwa ajili ya masomo kwa mwaka huu wa masomo 2017/2018” Mkurugenzi huyo amewaeleza waandishi wa habari kuwa lengo la Ofisi yake ni kuhakikisha majina ya wanafunzi wote waliofanikiwa kupata mkopo yanatolewa kabla ya vyuo kufunguliwa mwishoni mwa Oktoba.
“Orodha ya kwanza tayari inapatikana katika tovuti ya bodi ya mikopo www.helsb.go.tz na itatumwa kwa vyuo husika. Orodha nyingine zitafuata kadri taratibu za udahili na uchambuzi zitakavyokuwa zinaendelea kukamilika” Badru alibainisha.
Badru amefafanua kuwa kwa wanafunzi waliofaulu mitihani yao na wanaoendelea na masomo watatumiwa fedha zao vyuoni kuanzia leo. “Kiasi cha shilingi bilioni 318.6 kitatolewa kwa wanafunzi 93,295 wanaoendelea na masomo kwa mwaka wa masomo 2017/2018.
Tayari serikali imeshatuma fedha hizo, ambapo bodi inahakikisha fedha zinafika vyuoni kabla ya kufunguliwa kwa vyuo ili kuwaondolea wanafunzi usumbufu,” aliongeza Badru. Wakati huo huo, Kaimu Mkurugenzi wa Upangaji na Utoaji Mikopo wa Bodi hiyo Dk Veronica Nyahende amesema kuwa majina ya wanafunzi wote waliokosea majina yao yatafanyiwa uchambuzi na zoezi hilo likikamilika majina yao yatatolewa.
“Kwa mwaka huu tuliingia kwenye mfumo mpya ambao ni wa mtandao ambapo mwombaji akikosea anaomba upya na kuweka viambatanisho vyote ili kuthibitisha uhalali wake hivyo mwaka huu hatukuwa na utaratibu wa kuwaita waje hapa makao makuu,” alieleza Dk Nyahende.
Awamu ya kwanza ya wanafunzi hao 10,196 waliopata mkopo imepatikana baada ya bodi ya mikopo kupokea na kuchambua awamu ya kwanza ya majina ya wanafunzi 32,495 waliopata udahili katika chuo kimoja. Ikumbukwe kuwa sifa kuu za kupata mkopo ni mwombaji awe amepata udahili katika taasisi ya elimu ya juu inayotambuliwa na serikali.

WAZIRI ATOA PONGEZI KWA NSSF NA PPF KWA UWEKEZAJI


WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa (pichani) amepongeza hatua ya mifuko ya hifadhi ya jamii nchini kuwekeza kwenye sekta ya viwanda huku akitoa mwito kwa jamii hususani vijana kuhakikisha wanaonesha uzalendo kwa kujitolea kwa vitendo kuunga mkono jitihada hizo zinazolenga kutatua tatizo la ajira na kuinua uchumi wa taifa.
Majaliwa alitoa pongezi hizo mwishoni mwa wiki mkoani hapa baada ya kuongoza upandaji wa miwa ikiwa ni ishara ya kuunga mkono mradi mkubwa wa ujenzi wa kiwanda cha sukari unaofahamika kama Mkulazi II, unaotekelezwa kwa ubia kati ya mifuko ya hifadhi ya jamii ya NSSF na PPF kupitia Kampuni Hodhi ya Mkulazi Holding unaofanyika katika Gereza la Mbigiri, Dakawa wilayani Mvomero mkoani Morogoro.
“Pamoja na kutoa pongezi kwa mifuko yetu ya hifadhi ya jamii hapa nchini kwa kuitikia vema wito wa Serikali ya Awamu ya Tano katika uwekezaji wa viwanda vyenye tija kwa taifa, kipekee nitoe wito kwa jamii hususani vijana kuhakikisha wanaunga mkono jitihada hizi kwa kujitolea ujuzi na maarifa katika kufanikisha azma hii ya serikali inayolenga kuwanasua kutoka kwenye uhaba wa ajira,” alieleza

SERA YA MPIRA YANUKIA


WAZIRI wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe amewataka wadau wa michezo watumie fursa waliyopewa kuhakikisha wanapitisha sera nzuri ya michezo ili ipelekwe bungeni mapema kwa ajili ya kutungwa sheria.
Hayo aliyasema jana wakati akifungua mkutano wa wadau wa michezo wa kupitisha Sera ya Michezo uliofanyika kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. “Mimi sitakaa hapa baada ya kufungua ila mnatakiwa mbishane na baadaye mtoke na kitu kizuri ambacho kitasaidia michezo yetu kuwa ya kulipwa,” alisema Dk Mwakyembe.
Dk Mwakyembe alisema michezo ni ajira yenye fedha nyingi duniani na kumtolea mfano mchezaji ghali duniani kwa sasa, Neymar wa PSG ya Ufaransa na kusema fedha anayolipwa kwa mwezi inaweza kuendesha wizara tano kwa mwaka.
Neymar alihamia PSG kutoka Barcelona ya Hispania kwa ada ya dola za Marekani milioni 263. Pia aligusa kwenye ngumi na kueleza kuwa anafurahi kuona mabondia wakicheza nje na kuchukua mataji makubwa na kumtolea mfano Ibrahim Class na kuahidi atahakikisha anatetea mkanda wake wa dunia wa GBC nchini.
“Sera itamke namna wanamichezo, serikali na vyama vitakavyonufaika na kulinda timu za taifa,” aliongeza Dk Mwakyembe. Kwa muda mrefu wadau wa michezo wamekuwa akidai Sera ya Michezo baada ya kutofanyiwa marekebisho kwa miaka mingi. Mara ya mwisho sera ya Michezo ilifanyiwa marekebisho mwaka 1995.
Kwa maana hiyo mambo mengi yaliyokuwa kwenye sera hiyo yamepitwa na wakati. Wadau waliokuwepo kupitia sera hiyo ni viongozi wa vyama mbalimbali vya michezo nchini na wakufunzi wa michezo kutoka vyuo vikuu.

Awali kabla ya kufungua mkutano huo, Dk Mwakyembe alifanya ukaguzi wa Uwanja wa Taifa ambao unafanyiwa marekebisho na Kampuni ya michezo ya kubahatisha ya SportPesa.


MAHAKAMA Kuu Kanda ya Dar es Salaam imepanga Oktoba 19 hadi 23 mwaka huu kuanza kusikiliza kesi ya mauaji bila kukusudia ya aliyekuwa nguli wa fi lamu nchini, Steven Kanumba inayomkabili mwigizaji wa fi lamu maarufu nchini, Elizabeth Michael “Lulu” (pichani).
Lulu aliye nje kwa dhamana atapanda kizimbani mahakamani hapo baada ya kusomewa maelezo ya awali karibu miaka miwili na nusu iliyopita. Msanii huyo anakabiliwa na kesi hiyo akidaiwa kumuua Kanumba bila kukusudia kinyume cha Kifungu cha 195 cha Kanuni za Adhabu.
Inadaiwa Lulu alimuua Kanumba bila ya kukusudia Aprili 7, 2012 nyumbani kwa marehemu huyo Sinza Vatican, Dar es Salaam. Kwa mujibu wa ratiba ya vikao vya kesi za mauaji ya bila kukusudia iliyotolewa na Mahakama Kuu Dar es Salaam jana, kesi hiyo itasikilizwa siku hizo na Jaji Sam Rumanyika. Kesi hiyo inaanza kusikilizwa baada ya kupangiwa Jaji kufuatia upelelezi kukamilika.
Mara ya kwanza Lulu alipandishwa kizimbani Aprili 11, 2012 mbele ya Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Jijini Dar es Salaam wakati huo, Augustina Mbando ambapo alisomewa mashitaka ya mauaji.
Hata hivyo, Februari 18, 2014 akisomewa maelezo ya awali Lulu alikiri mahakamani kuwa na uhusiano wa kimapenzi na Kanumba na pia kusema kulikuwepo ugomvi baina yao siku ya tukio la kifo cha mwigizaji huyo.
Lulu aliachiwa kwa dhamana Januari 29, 2013 baada ya kesi hiyo kubadilishwa hati ya mashitaka kutoka kwenye kesi ya mauaji kwenda mauaji ya bila kukusudia ambapo badiliko hilo lilimpa nafasi ya kupata dhamana.
Katika kesi ya msingi namba 125 ya mwaka 2012, inadaiwa Aprili 7, 2012 Sinza Vatican Lulu alimuua Kanumba bila kukusudia. Lulu alipelekwa rumande gereza la Segerea hadi mashitaka yalipobadilishwa akapata dhamana.

UHURU KENYATTA APINGA SERIKALI YA MSETO







www.kwanguleo.blogspot.com

RAIS wa Kenya, Uhuru Kenyatta na Naibu wake, William Ruto wamesisitiza hakuna mgogoro wa kisiasa nchini humo na hawahitaji mtu kutoka nje kwenda kusuluhisha.
Wamesema pia kwamba, hakutakuwa na majadiliano kwa lengo la kuundwa kwa Serikali ya mseto. “Tunamwambia rafiki yetu Raila (Odinga), hatutajali umetembelea majiji mangapi. Hakutakuwa na majadiliano tena kuhusu serikali ya mseto, mjadala pekee utakuwa na Wakenya kwa kupiga kura,” alisema Ruto.
Walitoa msimamo huo kwenye mikutano ya kampeni kwenye maeneo la Kenol katika Kaunti ya Murang’a na Ndumberi katika Kaunti ya Kiambu. Wakati wa mkutano Kenol, Kenyatta alisema nchi hiyo haihitaji wasuluhishi kwa sababu haipo kwenye mgogoro.
“Hatutaki usuluhishi au kukutanishwa. Kofi Annan hayupo Kenya. Apande ndege arudi (Odinga) nchini kuomba kura,” alisema na kumtuhumu mpinzani wake kuwa anatafuta kuungwa mkono na jumuiya ya kimataifa kwa kujenga mtazamo kuwa demokrasia nchini humo imeoza.
Kenyatta alisema wazungu hawawezi kuitawala nchi hivyo, kama Raila anautaka urais arudi kwa Wakenya. Wakati wa mkutano wa kampeni kwenye eneo la Ndumberi, Kenyatta alisema Kenya inaongozwa kwa kuzingatia sheria na Katiba ambayo haina ibara inayohusu serikali inayotokana na majadiliano.
“Kwenye Katiba yetu hakuna ibara inayoruhusu watu wa nje kusimamia mambo ya taifa letu. Chini ya Katiba yetu ni Wakenya tu wenye haki kuamua akina nani wawe viongozi wao,” alisema na kuongeza kuwa Raila anataka kutumia mlango wa nyuma apate madaraka, lakini Wakenya hawatamruhusu.
“Hakuna mtu, jeshi au nchi inayoweza kumpa mtu uongozi wa nchi. Mtu pekee anayeweza kutoa hiyo fursa ni Mungu kupitia Wakenya,” alisema na kumtuhumu mpinzani wake kuwa anachafua sifa ya nchi hiyo nje ya nchi.
“Kama wanataka (nchi za nje) kumsaidia, msaada bora wanaoweza kumpa ni kumkatia tiketi ya ndege arudi Kenya aanze kampeni ili watu wa Kenya waamue Oktoba 26,” alisema Kenyatta kwenye mkutano wa Ndumberi.
“Watu kama Kofi Annan wanakaribishwa Kenya kama watalii na si kuingilia siasa za Wakenya,” alisema kwenye mkutano huo. Kwa mujibu wa Kenyatta na Ruto, Wakenya ndiyo wenye mamlaka ya kuchagua viongozi wao kwa kupiga kura lakini kuna mtu anataka kupata madaraka bila kuzingatia taratibu za Katiba.

WAZIRI MKUU ASEMA WAKUU WA EAC WABANA MAWAZIRI


Majaliwa, wakuu EAC wabana mawaziri

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa ameungana na viongozi wengine wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kukemea rushwa na uroho wa madaraka, akiwataka mawaziri wa Tanzania watumie madaraka yao kwa manufaa ya Taifa na kamwe wasiyatumie kama fursa ya kujitajirisha wao binafsi.
Kauli hiyo imekuja siku chache baada ya Rais wa Rwanda, Paul Kagame naye kuwaagiza kuwa, kazi kubwa waliyonayo mbele yao ni kuijenga Rwanda na kwamba hatavumilia mawaziri wazembe, watakaojinufaisha kwa fedha za umma na kutumia vibaya madaraka waliyopewa.
Aliyasema hayo saa chache baada ya kuwaapisha jijini Kigali, Rwanda na na kusisitiza kuwa, wanachotaka Wanyarwanda ni maendeleo, hivyo wawe tayari kufanya kazi kwa juhudi na maarifa. Alikuwa ametoka kutangaza baraza jipya, baada ya kuchaguliwa kuiongoza Rwanda katika awamu ya tatu.
Amekuwa madarakani tangu mwaka 2000, na kabla ya hapo, kwa miaka sita alikuwa Makamu wa Rais na Waziri wa Ulinzi. Akisisitiza uchapakazi, alisema anataka viongozi hao wawe wabunifu, lakini pia wawe na ushirikiano na mshikamano, lengo likiwa kuwaharakishia Wanyarwanda maendeleo na ustawi wa nchi yao kwa ujumla.
Kauli kama hizo zimekuwa zikitolewa pia na Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta, Yoweri Museveni wa Uganda, Pierre Nkurunziza wa Burundi na Salva Kiir wa Sudan Kusini, wakilenga kuzifanya nchi za EAC kuwa mfano wa kuigwa katika mapambano dhidi ya rushwa, lakini pia kuwa na kasi katika kujiletea maendeleo.
KAULI YA MAJALIWA
Aliyasema hayo jana alipozungumza na baadhi ya Mawaziri, Manaibu na Makatibu Wakuu katika kikao kilichofanyika jijini Dar es Salaam, muda mfupi kabla ya kusafiri kwenda Canada kwa ziara ya kikazi.
Alisema Rais, Dk John Magufuli anayeongoza mapambano dhidi ya rushwa, amesisitiza kwamba amewateua ili wafanye kazi na kamwe wasitumie madaraka waliyopewa kwa maslahi yao binafsi.
“Madaraka haya ya Uwaziri si fursa ya kujipatia utajiri, tunatakiwa tufanye kazi kwa weledi, uadilifu, bidii na uaminifu mkubwa ili kuondoa kero za wananchi kwa wakati.” Alisema Mawaziri na Manaibu Waziri wazingatie Katiba ya nchi, Kanuni, Taratibu na Miongozo mbalimbali ya Serikali katika utekelezaji wa majikumu yao ya kila siku.
Waziri Mkuu amesema Mawaziri hao wanatakiwa wasimamie utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa miaka kuanzia mwaka 2016/2017 hadi 2020/2021. Pia utekelezaji wa ahadi zote zilizopo kwenye Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015 pamoja na ahadi alizozitoa Rais Dkt Magufuli wakati wa kampeni za uchaguzi.
Amewaagiza Mawaziri wahakikishe wanakwenda kufanya ufuatiliaji wa tathmini ya utekelezaji wa mipango mbalimbali ya maendeleo inayohusu sekta zao. Pia amewataka Mawaziri hao wakasimamie kikamilifu ukusanyaji wa mapato na kuanzisha vyanzo vipya vya ukusanyaji pamoja na kudhibiti mianya ya upotevu.
Hata hivyo Waziri Mkuu amewataka Mawaziri hao wakapunguze urasimu katika utekelezaji wa malengo ya Serikali kwa sababu wananchi wanahitaji kuhudumiwa kwa wakati. Mawaziri waliohudhuria kikao hicho ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais –TAMISEMI Suileiman Jaffo na Manaibu wake, Joseph Kandege na George Kakunda, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu na Naibu wake, Dk Faustine Ndungulile.
Wengine ni Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Isack Kamwelwe na Naibu wake, Jumaa Aweso, Waziri wa Viwanda na Biashara, Charles Mwijabe na Naibu wake, Stella Manyanya, Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Hamisi Kigwangalla na naibu wake, Josephat Hasunga, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako na naibu wake, William Ole Nasha, Naibu waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega na Makatibu Wakuu wa Wizara hizo.
Wakatihuohuo, Waziri Mkuu aliondoka nchini jana kwenda nchini Canada kwa shughuli za kikazi. Akiwa Canada, anatarajiwa kufanya mazungumzo na viongozi waandamizi wa sekta mbalimbali za kipaumbele. Canada ni moja ya nchi zenye ushirikano wa muda mrefu na Tanzania katika nyanja za kisiasa, kijamii na kiuchumi.

SERIKALI YAONGEZA UMRI WA KUSTAAFU



SERIKALI ya Tanzania iko katika mchakato utakaowezesha kuongeza muda wa kustaafu kwa watumishi wenye elimu ya ngazi ya uprofesa, watafi ti na wataalamu wengine ili kuwapa muda zaidi wa kutumia taaluma zao kwa manufaa ya taifa.
Aidha, imesema inalifanyia kazi suala ya watumishi walioondolewa kazini kwa kukosa sifa ikiwemo kutokuwa na vyeti vya kidato cha nne kama ambavyo sheria inavyohitaji na kulipatia suluhu kwa kuwa wengi hawana mshahara.
Imesema watumishi wengi wa umma hulipwa mshahara kwa kufanya kazi kwa kati ya asilimia 30 hadi 50 huku ikiwa ni wachache sana wanaoweza kulipwa kwa kufanya kazi kwa asilimia 100, jambo ambalo litasimamiwa kikamilifu.
Kadhalika imesisitiza itaendelea kuwachukulia hatua za kisheria watu wanaoghushi sifa za kitaaluma na taarifa binafsi wakati wa kuomba kazi, kwa kuwa baadhi ya waomba ajira wameendelea kufanya hivyo.
Waziri wa Nchi, Ofi si ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Mkuchika alisema hayo jana jijini Dar es Salaam alipokuwa akipokea taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya Ofi si za Sekretarieti ya Ajira katika utumishi wa umma iliyowasilishwa kwake na Katibu wa Sekretarieti hiyo, Xavier Daudi.
Kuhusu wastaafu, Mkuchika alisema katika vyuo vikuu mbalimbali nchini wapo maprofesa na watafi ti wengi ambao umri wao wa kustaafu umefi ka ama unakaribia kufi ka huku wakiwa bado na nguvu ya kuweza kuendelea kulitumikia Taifa.
“Wataalamu hao wanatakiwa kustaafu wakiwa na miaka 60 kwa mujibu wa sheria, lakini serikali iko katika mchakato kuongeza muda wao angalau hadi miaka 65 kwa kuwa yapo maeneo ambayo ni lazima kuongeza muda wa kustaafu,” alisema Mkuchika.
Alitoa mfano wa taaluma hizo kuwa ni pamoja na wasomi wa ngazi ya uprofesa, watafi ti ambao wengi hufi kia kuwa wabobezi katika maeneo hayo wakiwa na miaka kati ya 50 huku wakitakiwa kutumia kwa miaka 10 kabla ya kustaafu, jambo ambalo huonekana bado wakiwa na nguvu.
Nchi nyingine za Afrika Mashariki za Uganda, Rwanda na Burundi wastani wa umri wa kustaafu ni miaka 60, ukiachilia mbali Kenya ambayo ni miaka 55 na ilikuwa imeanzisha mchakato wa kwenda miaka 60.
Mkuchika alisema Serikali imeanzisha vyuo mbalimbali vikuu na suala hilo la kustaafu kwa watumishi hao litaangaliwa ili utaalamu walio nao uweze kuandelea kuangaliwa. Kuhusu watumishi walioondolewa kwa kukosa vyeti vya kidato cha nne, alisema kuanzia mwaka 2004, sheria ya ajira iliainisha mtumishi kuwa na sifa ya cheti ya kidato cha nne, lakini wapo watumishi ambao walikuwa wakitumika kwa bila kuwa na vyeti hivyo wakati wa kukaguliwa kwa vyeti.
Mkuchika alihoji, Ofi si za Sekretarieti ya ajira katika utumishi wa umma iwapo wapo watumishi wa aina hiyo, wanaagwa vipi na kwamba washirikiane kulipatia suala hilo ufumbuzi ama Halmashauri ziwape nauli waweze kurudi makwao kwa kuwa maisha ni magumu na hawana mshahara.
Akijibu suala hilo, Naibu Katibu, Ofi si ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Suzan Mlau aliahidi kulifanyia kazi suala hilo kwa kuwa watumishi hao wanakwenda ofi sini, lakini hakuna wanachokifanya zaidi wanakaa tuu.
Akizungumzia nidhamu kazini, Mkuchika amewataka watumishi wa Ofi si hiyo kwa ujumla kufanya kazi kwa kuwa ni kioo cha serikali, na atasimamia kwa hakika utendaji na muda wa kazi kwa kuwa wapo wananchi wanaofi ka katika ofi si hizo na kushindwa kupata huduma huku jengo hilo likilipiwa pango la Sh milioni 34 kila mwezi.
Awali, akisoma taarifa ya Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma, Daudi alisema tangu kuanzishwa kwa ofi si hiyo 2010, imeweza kupokea maombi 472,516 huku ikiwa imewapangia vituo vya kazi waombaji 23,676.
Hata hivyo, alisema ukosefu wa teknolojia za kisasa nchini inawafanya wadau kutumia vibaya mitandao hususani ya kijamii na kuamua kuandaa matangazo ya uongo ya ajira na kujifanya ni sekretarieti imetangaza kwa kutumia mitandao ya kijamii na kupotosha umm

DKT. NDUNGULILE AFANYA ZIARA KUJIRIDHISHA NA HALI YA UPATIKANAJI WA DAWA

Naibu Waziri wa Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndungulile wa kwanza kushoto akisikiliza maelezo jinsi ya dawa zinavyoagizwa MSD kutoka kwa Mfamasia wa Hospitali ya Mwananyamala Bw. Marco Sallingu kulia wakati wa ziara yake katika vituo vinavyotoa huduma ya afya leo jijini Dar es salaam.
Naibu Waziri wa Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndungulile wa pili kulia akiangalia dawa ziliozopo katika stoo za wa Hospitali ya Mwananyamala wakati wa ziara yake katika vituo vinavyotoa huduma ya afya leo jijini Dar es salaam.
Naibu Waziri wa Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndungulile wa kwanza kushoto akisikiliza maelezo jinsi ya dawa zinavyoagizwa MSD kutoka kwa Mfamasia wa Hospitali ya Sinza Palestina Bi. Doris Messanga kulia wakati wa ziara yake katika vituo vinavyotoa huduma ya afya leo jijini Dar es salaam.
Naibu Waziri wa Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndungulile wa katikati waliosimama akiongea na wagonjwa wakati wa ziara yake Hospitalini Sinza Palestina alipotembelea vituo vinavyotoa huduma ya afya leo jijini Dar es salaam.
Naibu Waziri wa Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndungulile wa tatu kulia akiangalia nyaraka zinazoonesha jinsi ya dawa zinavyoagizwa MSD katika Zahanati ya Mwenge wakati wa ziara yake katika vituo vinavyotoa huduma ya afya leo jijini Dar es salaam.
Naibu Waziri wa Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndungulile wa kwanza kulia akiangalia dawa ziliozopo katika stoo za Zahanati ya Mwenge wakati wa ziara yake katika vituo vinavyotoa huduma ya afya leo jijini Dar es salaam.

…………………

NA WAMJW-DAR ES SALAAM

Naibu Waziri wa Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndungulile amefanya ziara kwenye baadhi ya vituo vitoavyo huduma za afya kwa ajili ya kujiridhisha na hali ya upatikanaji wa dawa jijini Dar es salaam.

Akizungumza lengo la ziara hiyo Dkt. Ndungulile amesema kuwa ameamua kufanya hivyo ili kuungana na Mhe. Rais wa wamau ya tano Dkt. John Pombe Magufuli pamoja na Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa la kutatua tatizo la dawa katika vituo vinavyotoa huduma za afya mpaka kufikia 2020.

“Mpaka kufikia hivi sasa katika bajeti ya mwaka wa fedha 2017/2018 Serikali imetenga shilingi Bilioni 262 kwa ajili ya kutatua tatizo la uhaba wa dawa nchini kutoka shilingi bilioni 31 katika mwaka wa fedha 2015/2016 “ alifafanua Dkt. Ndungulile.

Aidha Dkt. Ndungulile amesema kuwa katika ziara hiyo amegundua kwamba vituo vinavyotoa huduma ya afya vina dawa zote muhimu isipokuwa kuna upungufu wa vifaa tiba ambapo tatizo hilo litafanyiwa kazi mara moja .

Mbali na hayo Dkt. Ndungulile aliwataka waganga wakuu na Wafamasia wa vituo vinavyotoa huduma za Afya kuboresha upokeaji ,utunzaji wa dawa pindi zinapoingia kwenye stoo zao na usimamizi mzuri wa dawa hizo.

“Vituo vinavyotoa huduma za afya lazima ziwe na kamati za afya ambazo zitashiriki katika kupokea dawa pindi zinapotoka MSD badala yake zinapokelewa na mtu mmoja aidha mfamasia au mtumishi mwingine wa kitengo cha dawa” alisema Dkt. Ndungulile.

Dkt. Ndungulile leo amefanya ziara yake ya kutaka kujiridhisha na hali ya upatikanaji wa dawa katika Hospitali ya Mwananyamala,Hospitali ya Sinza na Zahanati ya Mwenge za jijini Dar es salaam.