Haki za kidemokrasia zimezidi kuonyesha kutoheshimiwa kaitka eneo la
Afrika Mashariki ambapo Kenya, Tanzania na Rwanda zimeshuka viwango
katika ripoti mpya juu ya hali ya uhuru duniani (global status of
freedom).
KenyaUtafiti uliofanywa na taasisi binafsi ya Freedom House lenye makazi yake Washington, ambalo sio la kisiasa wala serikali, linaeleza kasoro zilizojitokeza katika mchakato wa uchaguzi wa urais Kenya.
Ripoti hiyo imeeleza kuwa uchaguzi ulikuwa na utata, ambao “marudio ya uchaguzi yalioamrishwa na mahakama yalifanyika bila ya kuwepo mageuzi ya msingi, matukio ya vurugu za kisiasa na kususiwa kwa uchaguzi huo na mgombea mkuu wa upinzani, Raila Odinga.
“Mambo haya yanatia dosari ushindi wa Rais Uhuru Kenyatta, ambapo alidai kupata kura asilimia 98 ya kura zote pamoja na kuwepo mahudhurio ya chini ya wapiga kura,” ripoti hiyo imesema.
Taasisi hiyo imeipa Kenya asilimia 48 kati ya 100 --- ikionyesha demokrasia imeshuka kutoka asilimia 51 vile ilivyokuwa imeripotiwa mwaka 2017. Hali hiyo inaifanya Kenya kuwa kati ya nchi 58 zinazoelezwa kuwa “hazina uhuru kamili.”
Tanzania
Taasisi hiyo ya Freedom House pia imeripoti kushuka kwa haki za kidemokrasia nchini Tanzania, ambayo ilikuwa iko juu kidogo kuliko Kenya.
Tanzania, ambayo imepewa asilimia 52 katika ripoti hiyo mpya na asilimia 58 katika utafiti wa mwaka 2017, imewekwa katika kikundi cha nchi “zisizo na uhuru kamili.”
“Serikali ya Rais John Magufuli – ambaye alichukua madaraka mwaka 2015 kama ni mwanachama pekee wa chama tawala nchini – alianzisha ukandamizaji wa wapinzani, kuwafunga wanasiasa wa upinzani, akifunga vyombo vya habari na kuwakamata wananchi ambao wanatoa maoni yao ya kukosoa katika mitandao ya kijamii,” utafiti huo wa mwaka 2018 umeeleza.
Uganda
Uganda imeonyesha mabadiliko kwa kupanda daraja kutoka “kutokuwepo uhuru kabisa” kwenda “zisizo na uhuru kamili” japokuwa hivi sasa imepewa daraja la asilimia 37 ambayo bado iko chini kuliko Kenya na Tanzania.
Taasisi ya Freedom House inafanya tathmini yake ya uhuru nchini Uganda kwa kigezo cha “kuamka kwa sekta ya habari na utayari wa waandishi wa habari, mitandao ya jamii na wananchi kutoa maoni yao.”
Hata hivyo, ripoti hiyo imeongeza kuwa “hali ya kisiasa imeendelea kuwa kandamizi chini ya utawala wa muda mrefu wa Rais Yoweri Museveni.
Rwanda
Rwanda imeorodheshwa kati ya nchi 49 ambazo “haziko huru.” Imepewa asilimia 23 – ambayo imeshuka kidogo kutoka asilimia 25 ambayo ilipata mwaka jana katika ripoti ya Freedom House. Utafiti mpya hautoi maelezo juu ya daraja waliopewa Rwanda.
Nchi nyingine
Burundi, Somalia na Sudan Kusini pia zimeelezwa kuwa “haziko huru” katika ripoti hiyo.
Sudan Kusini imepewa daraja ya pili kutoka chini—pointi mbili--- kati ya nchi 195 ambazo tafiti hiyo ilifanywa na Freedom House. Somalia inaunafuu kidogo, ambapo inanukta saba. Burundi, pia imegubikwa na migogoro ya ndani lakini sio kwa kiwango ambacho Somalia na Sudan Kusini imeathiriwa na migogoro hiyo, imepata daraja ya asilimia 19.