KANISA KATOLIKI LATOA TAMKO KULAANI VURUGU NA MAUAJI



SeeBait
Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu. 

Dar es Salaam. Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), limelaani shambulizi la hivi karibuni lililotekelezwa na watu wasiojulikana dhidi ya Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu.

Mbunge huyo aliyejeruhiwa Septemba 7 kwa kupigwa risasi tano mjini Dodoma, hivi sasa anaendelea na matibabu katika Hospitali ya Aga Khan, jijini Nairobi nchini Kenya.

Baraza pia limeungana na Watanzania kulaani kwa nguvu zote matendo yote ya vurugu, mauaji na uvunjifu wa amani nchini.

Tamko la baraza hilo lililosainiwa na Makamu wa Rais wa TEC, Askofu Beatus Kinyaiya limetolewa baada ya kikao cha kawaida cha baraza kilichofanyika kwa siku mbili Septemba 9 na 10 jijini Dar es Salaam.

“Katika Taifa letu sasa tunashuhudia matendo ya mauaji ya watu wasio na hatia kama ilivyokuwa kule Mkuranga, Rufiji na Kibiti, utekwaji wa watu na kuteswa, utekaji wa watoto, ulipuaji wa ofisi za watu na hivi karibuni shambulio la mbunge Lissu,” limesema baraza katika tamko hilo.

Imeelezwa vurugu na mashambulizi ya aina yoyote ile yanalifedhehesha Taifa kwa kuwa matendo hayo ni dhambi, uhalifu na si utamaduni wa Mtanzania, hivyo vyombo vinavyohusika havina budi kuyakomesha mara moja.

No comments: