NYARANDU AIKIMBIA CCM NA KUACHIA JIMBO LA SINGIDA MASHARIKI

Image result for NYALANDU

Nimeamua kujiuzulu nafasi yangu ya Ujumbe wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi CCM, pamoja na nafasi zote za Uongozi ndani ya Chama kuanzia leo, Oktoba 30, 2017, halikadhalika asubuhi ya leo nimemwandikia Spika wa Bunge, Mh. Job Ndugai, barua ya kujiuzulu nafasi yangu ya Ubunge wa Jimbo la Singida Kaskazini kupitia tiketi ya CCM, nafasi ambayo nimeitumikia kwa vipindi vinne mfululizo tangu nilipochaguliwa kwa mara ya kwanza mnamo mwaka 2000 hadi Sasa.

Aidha, Nimechukua uamuzi huo kutokana na kutorishwa kwangu na mwenendo wa hali ya Kisiasa nchini, ikiwa ni pamoja na ukiukwaji wa haki za kibinadamu, ongezeko la vitendo vya dhuluma wanavyofanyiwa baadhi ya watanzania wenzetu, na kutokuwepo kwa mipaka ya wazi kati ya Mihimili ya dola (Serikali, Bunge, na Mahakama) kunakofanya utendaji kazi wa Kibunge wa Kutunga Sheria na wa Kuisimamia Serikali kutokuwa na uhuru uliainishwa na kuwekwa bayana kikatiba.

vilevile, Naamini kwamba bila Tanzania kupata Katiba Mpya Sasa, hakuna namna yeyote ya kuifanya mihimili ya dola isiingiliane na kuwepo kwa ukomo wa wazi na kujitegemea kwa dhahiri kwa mihimili ya Serikali, Bunge na mahakama ambayo ndio chimbuko la Uongozi Bora wa nchi, na kuonesha kwa uwazi kuwa madaraka yote yatokana na wananchi wenyewe, na kwamba Serikali ni ya Watu kwajili ya Watu.

Mimi Naondoka na kukiacha Chama Cha Mapinduzi CCM, nikiwa nimekitumikia kuanzia ngazi ya Uenyekiti wa UVCCM Mkoa, Ujumbe wa Kamati za Siasa Wilaya na Mkoa, Ujumbe wa Kamati ya Wabunge Wote wa CCM na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM TAIFA,  kwani nimejiridhisha kuwa kwa mwenendo wa hali ya kisiasa, kiuongozi na kiuchumi uliyopo Tanzania Sasa, CCM imepoteza mwelekeo wake wa kuisimamia Serikali kama ilivyokuwa hapo awali. Aidha, Naamini kuwa, kama ilivyotokea kwa mihimili ya Bunge na Mahakama kutokuwa na uhuru kamili, bila kuingiliwa kiutendaji kwa namna Moja au nyigine, CCM nayo imekuwa Chini ya miguu ya dola badala ya chama kushika hatamu na kuikosoa Serikali inapobidi kama yalivyokuwa maono ya Baba wa Taifa mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

Hivyo basi, kwa dhamira yangu, na kwa uamuzi wangu mwenyewe, nikiwa na haki ya kikatiba, natangaza kikuhama Chama Cha Mapinduzi CCM leo hii, na nitaomba ikiwapendeza wanachama wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA, basi waniruhusu kuingia mlangoni mwao, niwe mwanachama, ili kuungana na CHADEMA na watanzania wote wanaopenda kuleta mabadiliko ya kisiasa na kiuchumi nchini kwa kupitia mfumo wa ki demokrasia na uhuru wa mawazo.

vilevile, nimemua kujiuzulu kiti Cha Ubunge, Jimbo la Singida Kaskazini kuruhusu kufanyika kwa uchaguzi mwingine ili wananchi wapate fursa ya kuchagua itikadiwanayoona inawafaa kwa majira na nyakati hizi zenye changamoto lukuki nchini Tanzania.
Ni imani yangu, kamwe hayatakuwa ya bure maneno haya, wala uamuzi huu niufanyao mbele ya Watanzania leo ili kwamba, sote kama TAIFA tuingie kwenye mjadala wa kuijenga upya misingi ya nchi yetu. Ni maombi yangu kwa MUNGU kuwa Haki itamalaki Tanzania.Upendo, amani na mshikamano  wa watu wa imani zote za dini, mitazamo yote ya kiitikadi za Kisiasa, na makabila yote nchini uimarike. Tushindane ki sera na kuruhusu tofauti za mawazo, lakini tubaki kama ndugu, na Taifa lililo imara na nchi yenye Adili.

                                             mungu awabariki wote

                                                                   LAZARO NYARANDU


SOMA HOTUBA YA ZITTO KABWE



Uchumi wa Nchi Unaanguka, Katiba ya Nchi Inakanyagwa, Utumieni Uchaguzi Huu Kuionyesha Serikali Mnayakataa Mambo Haya.Sehemu ya Hotuba ya Kiongozi wa Chama katika Mkutano wa Ufunguzi wa Kampeni za Udiwani - Kijichi]

Ndugu Watanzania,Ndugu Wanatemeke
Ndugu Wanakijichi

Pamoja na masuala haya ya uchaguzi mdogo hapa Kijichi ninaomba nizungumzie masuala machache ya kitaifa. Nafanya hivi kwa sababu baada ya siku thelathini kutoka leo hatutakuwa tena na nafasi ya kuzungumza majukwaani kama viongozi wa vyama vya siasa kwa sababu ya zuio lisilo la kikatiba ambalo limewekwa na Rais dhidi ya mikutano ya hadhara. Hivyo, sisi tumeamua kutumia majukwaa haya ya kampeni za uchaguzi mdogo kuzungumzia mambo ya kitaifa pia.

Tutaitumia mikutano hii ya kampeni kuelezea hali mbaya ya uchumi wa nchi yetu, pamoja na kuminywa kwa haki za wananchi na kusiginwa kwa Katiba ya Taifa letu.

Haki: Nitaanza na hili la haki za wananchi, nyie mtakuwa mashahidi juu ya jambo hili la kuvunjwa kwa haki za wananchi, kwa sababu ya muda nitatoa mifano minne kama ifuatavyo: 

1. Utawala huu wa awamu ya 5 ndio utawala unaovunja haki za watu kwa kiwango kikubwa sana ambacho hakijawahi kuonekana nchini, ndani ya muda wake mfupi wa miaka miwili ya utawala huu, magazeti zaidi ya matatu yameshafungiwa sasa, magazeti yote hayo yalionekana kuwa mwiba kwa Serikali kwa kuhoji na kuandika mambo mbalimbali juu ya hali ya Nchi yetu. Si hilo tu, bado kuna zuio lisilo la kikatiba la Rais juu ya mikutano ya hadhara, huku mamia ya watu wakiwa wameshtakiwa, na wengine kuhukumiwa vifungo na faini, kwa kutumia sheria mbaya ya mitandao ya mitandao ya kijamii, kwa sababu tu ya kutoa maoni yao ambayo yako kinyume na Serikali. Yote haya ni rekodi mpya ya uvunjivu wa haki za wananchi nchini mnayopaswa kuikataa.

2. Ni ndani ya kipindi hiki cha Serikali ya awamu ya 5, ndipo utu umekosekana kabisa nchini, wananchi wanavunjiwa nyumba zao walizozijenga kwa jasho lao bila hata kulipwa fidia, huku hata mahakama zetu pamoja na Katiba ya nchi kutokuheshimiwa kwa Serikali kuvunja hata nyumba ambazo mahakama imeweka zuio, nyie Wanakijichi ni mashuhuda wa hili, ndugu zenu wa Kimara wamedhalilishwa kwa kuvunjiwa nyumba zao bila fidia na kurudishwa kwenye umasikini. Hali hiyo si Dar tu hapa, wananchi wanavunjiwa nyumba zao bila fidia mikoa mbalimbali nchini, hivi karibuni ni Tabora. Mnao wajibu wa kuwafuta machozi hawa, kwa kuhakikisha mnakikataa chama tawala.

3. Ni kipindi hiki pia ndio tumeshuhudia watu wanaouwawa hovyo hovyo hovyo tu, nanyi ni mashahidi hapa Dar, kila siku inaokototwa miili tu ya watu kule ufukweni Coco Beach, wakiwa wameuawa. Serikali haijawahi kusema chochote juu ya miili hiyo inayookotwa, tuna serikali isiyojali uhai wa watu wake. Si hilo tu, mbunge mwenzangu Tundu Lissu amepigwa risasi zaidi ya 30 zaidi ya mwezi mmoja sasa, mmesikia mtu yoyote amekamatwa kwa tukio hilo? Na msidhani wanaoathirika ni watu wa Upinzani tu, la hasha, aliyekuwa Mwenyekiti wa CCM wa Wilaya ya Kasulu amepotea tangu mwezi julai, mama mpaka leo hajapatikana. Kuinyima kura CCM ni kuonyesha uhai wa hawa watu una maana kwenu, ni kuonyesha mnajali.

4. Serikali hii imekataa kuwapa haki yenu ya kuwa na mchakato mpya wa Katiba Mpya, mchakato utakaoanzia kwenye maoni ya Tume ya Jaji Warioba, maoni yenu wananchi. Rais anasema kwa kiburi kuwa hakuwaahidi Katiba, na wapambe wake wanazunguka huku na huku kupinga uwepo wa mchakato wa Katiba mpya. Kukikataa chama tawala kwenye uchaguzi huu ni kukiambia kuwa mamlaka ya uongozi ni yenu nyie wananchi, na kwamba mnataka mchakato wenu wa Katiba uendelee.

Hiyo ni mifano michache tu ya ubinywaji wa haki kinyume kabisa na Katiba ya nchi yetu, Katiba ambayo Rais aliapa kuilinda. Wananchi wa Kijichi hampaswi kumchagua mtu atokanaye na chama tawala, chama kinachovunja Katiba na kuminya haki za wananchi namna hiyo kama tulivyoonyesha.

Uchumi: Hali ya uchumi wa Nchi ni mbaya sana, ni mbaya mno kinyume kabisa na takwimu zinazotolewa na kuonyesha kuwa kasi ya ukuaji wa uchumi kuwa kubwa kwa kiwango cha 7%. Mie ni mchumi, pamoja na wachumi wengi wenzangu tunajua kuwa shughuli za uchumi zimedorora, na nyie wananchi ni mashahidi juu ya hali mbaya ya uchumi wa nchi, hili ni jambo la dhahiri kabisa. 

Oktoba 10, 2017 Serikali yenyewe kupitia Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) ilitoa taarifa yake juu ya hali ya uchumi wa nchi yetu, taarifa iliyoonyesha kuwa hali ya uchumi wa nchi si nzuri kabisa, kukiwa na dalili zote za uchumi wa nchi yetu kusinyaa na kudidimia, mfumuko wa bei ukionyesha kupanda na thamani ya shilingi kudidimia.

Taarifa hiyo inaonyesha namna hali ya uchumi wetu inavyozidi kuwa mbaya zaidi kwa wananchi wa hali ya chini, mfumuko wa bei umepanda mno tangu kuanza kwa utekelezaji wa bajeti ya 2017/18, ongezeko ambalo limechangiwa zaidi na kupanda kwa bei ya bidhaa za chakula (bidhaa ambazo wananchi wengi zaidi mnazitumia).

Baadhi ya bidhaa za vyakula zilizochangia ongezeko hilo ni dagaa asilimia 7.6, matunda makavu kama nazi kwa (3.1), viazi vitamu kwa (3.0), mchele (1.5) na ndizi (1.5). Bidhaa nyingine zilizochangia ni mkaa kwa asilimia 4.0, dizeli (2.4) na petroli (0.6). Ukizitazama bidhaa zote hizi ni zile ambazo zinatumiwa zaidi na wananchi wa kawaida kabisa, nyie watu wa Kijichi. CCM wameamua kuwadumbukiza kwenye umasikini.

Pamoja na kupanda kwa bei za vyakula, taarifa ile ilionyesha kuwa thamani ya sarafu ya Tanzania imeshuka, uwezo wa Tsh. 100 kununua bidhaa umeshuka hadi Tsh. 92.18. Maana yake ni kuwa kama mwaka 2016 shilingi 100,000 ilikupa bidhaa za shilingi 100,000. Mwaka huu 2017 shilingi 100,000 inakupa bidhaa za shilingi 92,000. Kwa hiyo ili upate bidhaa za shilingi laki moja inakubidi uongeze shilingi elfu 8 zaidi. Hali hii inawaumiza mno nyie wananchi.

Wakati Rais wa sasa akiingia madarakani bei ya sukari ilikuwa ninshilingi 1800 mpaka 2000, kwa sasa bei ya sukari ni shilingi 2800 hadi 3000. Gharama za maisha yenu zimepanda mno, Serikali hii imeshindwa kabisa kusimamia uchumi wa nchi.

Lakini msidhani ni uchumi wenu tu nyie watu wa chini ndio mbaya, hapana, ni nchi nzima, jana tulitoa taarifa ya uchambuzi wa takwimu za uchumi wa Serikali inayoonyesha kuwa hali ni mbaya nchi nzima, uzalishaji wa viwanda ukishuka kwa 50%, ujazo wa fedha ukishuka kwa 51%, mikopo kwa sekta binafsi ikishuka kwa 23%, mapato ya bidhaa za forodha yakiwa ni shilingi bilioni 300 tu kutoka bilioni 500 iliyotarajiwa.

Sekta ya Kilimo imeshuka mpaka kiwango cha kabla ya Uhuru, kwani kasi ya ukuaji wa sekta ya Kilimo mwaka 2016 ilikuwa 1.6% tu. Wakulima wa Korosho hawajapewa pembejeo, hivyo uzalishaji wa zao linalotuingia mapato ya Kigeni zaidi nchini utashuka msimu huu wa mavuno, Tumbaku (zao la pili Kwa kuingiza Fedha za kigeni) tayari wakulima wanalia, mazao ya choroko na kunde bei imeshuka kwa zaidi ya 500%, Pamba uzalishaji umeshuka Kwa 63% kati ya mwaka 2015 na 2017 (miaka miwili ya utawala wa awamu ya 5), na mauzo Nje ya dhahabu kuanza kushuka na hivyo kupelekea shilingi kushuka thamani na hivyo mfumuko wa bei kupanda Kwa kasi. 

Kiufupi, ukuaji wa pato la taifa umesinyaa katika robo ya pili ya mwaka huu, ikiwa ni - 0.6, ukuaji hasi ukionyesha kusinyaa kwa uchumi. Tunazo dalili zote za kuanguka kwa uchumi wa nchi.Wanakijichi, mna sababu tena ya kuendelea kukichagua chama kilichowafikisha kwenye hali hiyo? Mnataka uchumi wa nchi ushuke zaidi? Mnataka watu wetu waokotwe zaidi Coco Beach? Mnataka magazeti zaidi yafungiwe? Mnataka bei ya sukari na vyakula vingine ipande zaidi? Kama hamtaki hilo mnao wajibu wa kumpuuza mgombea wa CCM, na kumchagua mgombea wa ACT Wazalendo, ndugu Edgar Mkosamali ili asaidiane nanyi kutatua kero zenu kama alivyojieleza hapa. Mkifanya hivyo mtakuwa pia mmeiambia Serikali irelebishe masuala haya ya Kitaifa.
Ahsanteni kwa kunisikiliza
Kabwe Z. Ruyagwa Zitto
Kiongozi wa Chama - ACT Wazalendo 
Oktoba 29, 2017
Kijichi 
Dar es salaam

MEYA MWANZA AWEKWA NDANI

Related image
Tukio hilo limetokea baada ya kubainika katika salamu za Meya kwa Rais Magufuli, kulikuwa na maelezo ya ufisadi wa kiwanda hicho kilichopo Nyakato Ilemela jijini Mwanza.
Wanaotajwa kufanya ufisadi huo ni mkurugenzi wa Jiji hilo, Kiomoni Kibamba na viongozi wengine wa mkoa huo.
Pia viwanda vya kampuni hiyo vimekuwa vikituhumiwa kuwanyanyasa wafanyakazi wake wengine wakitimuliwa kazi bila kulipwa stahiki zao.
Baada ya kamati ya Ulinzi na usalama mkoa wa Mwanza chini ya John Mongella kubaini kwamba Meya huyo anataka kumwaga ukweli mbele ya rais, inadaiwa aliliagiza jeshi la Polisi kumkamata kiongozi huyo ambaye kwa kipindi kifupi ameonekana akifichua uchafu unaofanyika katika jiji la Mwanza.

VIONGOZI WA DINI WASHAURIWA KUJENGA UZALENDO

Image result for PHOTO OF HARRISON MWAKYEMBE
SERIKALI imewataka viongozi wa madhehebu ya dini nchini, kuwajengea waumini wao moyo wa uzalendo kwa nchi yao kupitia mafundisho na mahubiri yao.Hayo yalisemwa Dar es Salaam jana na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe alipokutana na viongozi wa madhehebu ya dini nchini, kujadili mada iliyosema ‘Imani na Uzalendo Kuelekea Uchumi wa Viwanda’ ikiwa ni sehemu ya kampeni ya kujenga uzalendo na utaifa kwa Watanzania.

Mwakyembe aliwakumbusha viongozi hao wa dini kuwa uzalendo ni hali ya mtu kuwa na uchungu na taifa lake katika kuliletea maendeleo ya kiuchumi, kisiasa na kulitetea.Kutokana na dhana hiyo ya uzalendo, Serikali imewasisitiza viongozi wa dini kupitia mafundisho yao kuwakumbusha waumini wao kutekeleza mambo kumi kama sehemu ya imani yao, lakini kwa ustawi na maslahi ya taifa.Mambo hayo kumi ni pamoja na wajibu wa kila muumini kulipa kodi, kuzingatia usafi na utunzaji wa mazingira, kufanya kazi kwa bidii kwa kuwa Watanzania wana sifa nzuri ya kuchapa kazi, wanapokuwa nje ya nchi tofauti na wanapokuwa hapa nchini.
“Mambo mengine ambayo tunawaomba muwakumbushe waumini wenu ni uadilifu, kutii mamlaka, kulinda rasilimali za nchi kwa moyo, nguvu na akili zote, kupinga rushwa na matumizi ya dawa za kulevya pamoja na kuzingatia uaminifu kwa kujieupesha na vitendo vya wizi,” alieleza Dk Mwakyembe.
Waziri Mwakyembe aliwaambia viongozi wa dini kuwa wana jukumu kubwa la kuirejesha jamii ya Watanzania kwenye mstari, kwa kusisitiza uzalendo na utaifa ili taifa liwe na amani na utulivu na liweze kufikia malengo ya kuwa na uchumi wa viwanda.

“Matatizo makubwa katika nchi huanza polepole na tusipoziba ufa tutajenga ukuta. Msichoke kuhubiri amani kwenye nyumba zenu za ibada ili amani tuliyonayo tangu tupate uhuru iendelee kudumu, ,” alieleza Mwakyembe.

WAPINZANI WATAKIWA KUWAACHIA WATU 30 WALIOWAKAMATA CONGO

Umoja wa mataifa umetoa wito wa kuachiwa mara moja kwa watu 30, wa chama kikuu cha upinzani katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, kutoka korokoroni.Wanachama wa vyama vikuu viwili vya Union for Democracy na wenzao wa Social Progress, walikamatwa siku ya Jumapili katika mji wa Lubumbashi, ulioko Kusini mashariki mwa nchi hiyo, baada ya polisi kuvunja mkutano waliokuwa nao.Utawala wa Rais, Joseph Kabila, umepiga marufuku mkutano wa aina yoyote wa kisiasa, pamoja na maandamano ya upinzani, tangu muda wake wa kuhudumu kama Rais kisheri, ulipomalizika mwaka mmoja uliopita.
Tume ya uchaguzi nchini humo, imesema kuwa, haitakuwa rahisi kuandaa uchaguzi mkuu wa Urais, kabla ya mwezi Aprili mwaka ujao wa 2019.Chama kingine cha upinzani- Union for the Congolese Nation, kimesema kwamba, kitajiondoa katika serikali ya ugawanaji mamlaka, kuhusiana na kucheleweshwa kwa uchaguzi mkuu.Maandamano ya mara kwa mara ya upinzani nchini humo umekabiliwa vikali na utawala wa Rais Joseph Kabila.

WAANDISHI WA HABARI WACHAPWA VIBOKO

Waandishi wa Habari wacharazwa bakora Geita

 Daniel Limbe mwenyekiti wa chama cha waandishi wa habari geita
Waandishi wa habari wanne mkoani Geita wameshambuliwa kwa bakora na kuwekwa sero na askari wa jeshi la polisi mkoani humo wakati wakitekeleza majukumu yao baada ya wanafunzi wa shule ya sekondari Geita kufanya vurugu shuleni.
Inaelezwa kuwa waandishi hao wamekutwa na maswahibu hayo  Oktoba 21,2017 ambapo mbali na kupigwa kamera ya mwandishi wa habari Esther Sumira wa Azam Tv imeharibiwa.
Mwenyekiti wa Klabu ya waandishi wa habari mkoa wa Geita Daniel Limbe amewataja miongoni mwa waandishi wa habari waliokumbwa na kadhia hiyo kuwa ni Esther Sumira ( Azam Tv) ,Editha Edward (Mtanzania,Rehema Matowo(Mwananchi) na Emmanuel Ibrahim (Clouds Media).
Taarifa zinasema hakuna uhusiano mzuri baina ya jeshi la polisi mkoa wa Geita na waandishi wa habari.
Chama cha Waandishi wa habari mkoa wa Geita (GPC) kinalaani vikali tukio la waandishi wa habari kushambuliwa kwa kipigo na jeshi la polisi wakati wakitekeleza majukumu yao kwenye vurugu zilizotokea jana kwenye shule ya sekondari Geita(Geseco).Vurugu hizo ambazo wanafunzi walikuwa wakishinikiza Bodi ya shule kuhakikisha inakwenda kufanya mazungumzo ya haraka na jeshi la polisi ili kuwatoa mahabusu wanafunzi watano waliokuwa wakishikiliwa kwa madai ya kumjeruhi kwa kipigo mwanafunzi mwenzao wa kidato cha tano,walitumia mawe kuponda majengo ya shule na kutishia kuichoma moto shule hiyo iwapo hatua za makusudi za wenzao kulejea shuleni hazitafanikiwa.
Baada ya vurugu hizo waandishi walifika eneo la tukio kwa ajili ya kutimiza wajibu wao ambapo Mwandishi wa gazeti Habari Leo,Editha Edward,alikumbana na kichapo cha askari polisi waliofika kutuliza ghasia zilizokuwa zimejitokeza shuleni hapo licha ya kujitambulisha kuwa yeye ni mwandishi wa habari.
Wengine waliokumbana na Kadhia hiyo ni Rehema Matowo, mwandishi wa gazeti la Mwananchi ambaye alinyang’anywa simu yake na kuwekwa chini ya ulinzi kwa muda kwenye chumba cha walinzi wa shule hiyo kabla ya kumrejeshea simu yake na kumwachia huru huku akitakiwa aondoke eneo hilo.
Hata hivyo Mwandishi wa Azam Tv Ester Sumira,alinyang’anywa kamera yake na walimu wa shule hiyo kwa muda wa zaidi ya dakika 20 wakimtaka kutochukua picha za vurugu zilizokuwa zikiendelea eneo hilo.
Na Mwandishi wa Cloud Tv,Emmanuel Ibrahimu alikumbana na msukosuko baada ya polisi kuzuilia pikipiki yake na kusababisha kushindwa kutekeleza majukumu yake ya kazi.
Kutokana na vitendo hivyo visivyokuwa vya kiungwana ambavyo vinakiuka misingi ya utawala Bora na Haki za Binadamu,Chama cha waandishi wa habari mkoa wa Geita kinaendelea kulaani vikali na tunaziomba taasisi zingine kama UTPC,MCT, TEF na wadau wote kulaani vitendo hivi vya kihuni ambavyo vinaendelea kutamalaki kila uchwao na kuharibu taswira nzima ya Utawala bora nchini.

MAHAKAMA KENYA YASHIDWA KUSIKILIZA KESHI YA KUIHIRISHWA KWA UCHAGUZI

Mahakama ya Juu Kenya yashindwa kusikiliza kesi ya kuahirishwa kwa uchaguzi kutokana na ukosefu wa majaji wa kutosha mahakamani.Jaji Mkuu David Maraga amesema baadhi ya majaji wapo nje ya nchi na wengine hawangeweza kufika mahakamani kwa sababu mbalimbali.Kesi hiyo ilikuwa imewasilishwa na wapiga kura watatu wakisema Tume ya Uchaguzi haiko tayari kuandaa uchaguzi huru na wa haki kesho.Jaji Mkuu amekuwa mahakamani na Jaji Isaac Lenaola pekee.Naibu Jaji Mkuu Philomena Mwilu hakuweza kufika kortini baada ya kupigwa risasi kwa dereva wake jana jioni.Jaji Ibrahim, ambaye amekuwa akiugua, yuko nje ya nchi.Majaji Smokin Wanjala na Jacktone Ojwang hawakuweza kufika kortini pia.Jaji Njoki Ndung’u alikuwa amesafiri nje ya jiji la Nairobi na hakuweza kupata usafiri wa kumuwezesha kufika mahakamani kwa wakati.“Sisi wawili hatuwezi kufikisha idadi inayohitajika ya majaji mahakamani kwa mujibu wa kifungu 162 (2) cha Katiba. Kesi imeahirishwa hadi wakati mwingine,” ametangaza Jaji Maraga.
Wakili wa raia hao watatu waliokuwa wamewasilisha kesi hiyo, Harun Ndubi, ameshutumu hatua ya majaji kukosa kufika kortini akisema ni jambo la kushangaza.“Wakitoweka wakati tunawahitaji kutekeleza jukumu hili muhimu, unashangaa iwapo wanafuata kiapo walichokula,” amesema.Seneta wa Siaya James Orengo aliyewakilisha Raila Odinga mahakamani wakati wa kesi ya kupinga matokeo ya uchaguzi wa tarehe 8 Agosti amesema kilichotokea leo ni “mapinduzi ya katiba”.“Haya yamekuwa yakifanyika, hata katika tume ya uchaguzi. Stakadhabi zilizowasilishwa na tume kujibu kesi zimewasilishwa na naibu mwenyekiti na wala si mwenyekiti. Ni wazi kwamba tume ya uchaguzi inafanya kazi bila mchango wa mwenyekiti. Wafula Chebukati amekuwa abiria,” amesema.
“Taasisi ambayo imelemazwa na Jubilee kwanza ni IEBC. Na tume iliyosalia haina uwezo wa kuandaa uchaguzi.”Bw Orengo amesema anaamini ukosefu wa majaji wa kutosha mahakamani haufai kushangaza wengi na kudokeza kwamba uamuzi wa kutangaza leo kuwa Siku ya Mapumziko ulilenga kuvuruga shughuli za mahakama.“Kuna jaribio la kuhujumu taasisi za serikali zikiwemo taasisi huru kama vile tume ya uchaguzi na Mahakama ya Juu,” amesema.

TCU YATANGAZA MUDA WA KUANZA MASOMO ELIMY YA JUU

Kaimu Katibu Mtendaji wa Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) Profesa Eleuther Mwageni amesema wanafunzi ambao tayari wamekidhi vigezo na kupitishwa kujiunga na elimu ya juu wanatakiwa kuripoti chuoni ili kuanza masomo ifikapo Oktoba 30
“Tarehe ya Kalenda ya masomo haijabadilika iko palepale ambayo ni Oktoba 30 wanafunzi wanatakiwa kuanza masomo ya elimu ya juu kwa mwaka 2017/2018”, amesema Mwageni.
Aidha Prof. Mwageni ameeleza kuwa zaidi ya wanafunzi 450,000 tayari wameshapata vyuo hivyo kinachosubiriwa katika awamu ya tatu ni kupitisha wanafunzi wengine 12,000 ili kufikia malengo ambayo ni wanafunzi 57,000.
Awamu ya tatu ambayo ilianza Oktoba 18 hadi 22 imefikia hatua nzuri ambapo vyuo vinawasilisha TCU majina ya waombaji ambao vimewapitisha ili tume iweze kujiridhisha kisha wanafunzi waliochaguliwa katika awamu hiyo wajiunge na vyuo na waanze masomo kwa wakati.

Baadhi ya polisi wakiwa katika eneo la tukio Ukonga Mazizini wakidumisha ulinzi ili wananchi wasiendelee kuleta vurugu katika eneo hilo.


Kufuatia sintofahamu iliyokuwa inaendelea maeneo ya Mombasa Gongo la Mboto kati ya wananchi na jeshi la polisi na kupelekea baadhi ya raia kujeruhiwa na polisi kwa kile kinachodaiwa kuwa polisi walikuwa wanalipiza kisasi kufuatia kuuawa kwa askari mmoja wa kikosi cha 'Field Force Unit' (FFU)
Mkuu wa Wilaya ya Ilala Sophia Mjema ametembelea eneo hilo na kusikitishwa na kitendo cha jeshi la polisi kuchukua sheria mkononi na kujeruhi watu ambapo ameagiza wote waliohusika kufanya matukio hayo kuchukuliwa hatua za kisheria.

"Nimeambatana na RPC Salum Hamduni hivyo kwa wale walihusika hatua zitachukuliwa, na wale waliojeruhiwa watatibiwa, pia tumewachukua baadhi ya wananchi ambao wamehaidi kutoa ushirikiano hivyo  tutalifanyia uchunguzi na kutenda haki" Alisema DC Mjema.
Mkuu wa wilaya ya Ilala bi. Sophia Mjema akiongea na wananchi wa eneo la Ukonga Mazizini na kusikiliza kero zao baada ya kudai kupigwa na kupokonywa mali zao na watu wanaodhaniwa kuwa ni askari wa FFU.
DC Mjema amewataka wananchi wote walioharibiwa mali zao wajiorodheshe na serikali ya wilaya italifanyia kazi, huku akisisitiza hakukuwa na sababu ya kuchukua sheria mkononi wakati kulikuwa na mbadala wa kulichunguza suala hilo na kulipatia utatuzi.

Mkuu huyo wa wilaya ya ilala amewaomba wananchi watulie na waendelee na shughuli zao kwani hilo siyo jambo kubwa la kupelekea watu wauane na wavuruge amani ya nchi.

Sintofamhamu hiyo imedumu kwa siku tatu kufuatia kifo cha askari wa kikosi cha FFU ambapo inadaiwa aliuawa na wananchi jambo lililopelekea vurugu hizo, baina ya jeshi la polisi na wananchi.