Wamiliki wa Kampuni ya ACACIA wakubali kulipa pesa za Tanzania baada ya Mazungumzo.
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli
amekutana na kufanya mazungumzo na Mwenyekiti wa Kampuni ya Barrick Gold
Corporation ambayo ni mmiliki mkubwa wa kampuni ya Acacia Mining
Limited Prof. John L. Thornton na kukubaliana kuwa kampuni hiyo ipo
tayari kufanya mazungumzo na Serikali ya Tanzania ili kulipa fedha
ambazo Tanzania imezipoteza kutokana na kampuni hiyo kuendesha shughuli
zake hapa nchini.
Prof. John L. Thornton ambaye amesafiri kwa
ndege binafsi kutoka nchini Canada hadi Tanzania amekutana na Mhe. Rais
Magufuli leo Juni 14, 2017 Ikulu Jijini Dar es Salaam na mazungumzo yao
yamehudhuriwa na Balozi wa Canada hapa nchini Mhe. Ian Myles na Waziri
wa Sheria na Katiba Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi.
Baada ya
Mazungumzo hayo Prof. John L. Thornton amesema kampuni yake ipo tayari
kufanya mazungumzo na Tanzania yatakayozingatia maslahi ya pande zote
mbili na pia ipo tayari kulipa fedha zote ambazo inapaswa kulipa kwa
Tanzania.
Kwa upande wake Mhe. Rais Magufuli amesema Serikali
inakaribisha mazungumzo hayo na itaunda jopo la wataalamu watakaofanya
majadiliano na kampuni ya Barrick Gold Corporation ili kufikia
makubaliano ya kulipwa fedha zinazodaiwa na namna kampuni hiyo
itakavyoendesha shughuli zake nchini maslahi ya pande zote mbili.
Mhe.
Rais Magufuli amesema pamoja na kukubali kulipa fedha zinazodaiwa Prof.
John L. Thornton amekubali kushirikiana na Tanzania kujenga mtambo wa
kuchenjulia dhahabu (smelter) hapa nchini.
Wakati huo huo, Mhe.
Rais Magufuli amevionya vyombo vya habari vinavyowataja Marais wastaafu
Mhe. Benjamin William Mkapa na Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete na kuwahusisha
na taarifa za kamati mbili za uchunguzi wa madini yaliyo katika
makontena yenye mchanga wa madini (Makinikia) ambao ripoti zimekabidhiwa
kwake na kamati hizo.
“Nimesoma ripoti zote mbili hakuna mahali
ambapo Mzee Mkapa na Mzee Kikwete wametajwa, vyombo vya habari viache
kuwachafua hawa wazee, wamefanya kazi kubwa ya kulitumikia Taifa letu,
viwaache wapumzike” amesema Mhe. Rais Magufuli.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
14 Juni, 2017
No comments:
Post a Comment